MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Habari Ushindi wa Shein wazua vurugu Z'bar
BOOKMARK THIS PAGE
Ushindi wa Shein wazua vurugu Z'bar  Send to a friend
Sunday, 11 July 2010 10:12

* Wafuasi wa Dk Bilal watishia kumuunga mkono Maalim Seif, yeye amkaribisha
 Na  Waandishi Wetu
UTEUZI wa Dk Ali Mohammed Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM umepokelewa kwa vurugu visiwani (Zanzibar) na baadhi ya wanachama wa chama hicho wakipinga uteuzi huo.

Wakati huko Zanzibar hali ikiwa tete, baadhi ya wakazi wa Tanzania Bara wameuunga mkono uteuzi huo wakisema utamaliza siasa za chuki visiwani.

Mara baada ya kupata taarifa za uteuzi huo kutoka mjini Dodoma, wanachama hao waliokuwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja walipandwa hasira na wengine kutamka wazi kuwa hawatamuunga mkono Dk Shein katika kampeni za uchaguzi mkuu .

Baadhi yao wakiwa katika maeneo ya starehe, kama vilabu vya pombe, walivunja chupa ukutani kuonyesha hasira zao kupinga kutoteuliwa Dk Mohammed Gharib Bilal au Shamsi Vuai Nahodha katika nafasi hiyo.

Maeneo ambayo watu hao walikuwapo huku wakifuatilia mkutano wa Dodoma ni pamoja na mitaa ya Maisara, Gofu, Kwa-Raju, Ghymkana na Hoteli ya Bwawani ambayo mwishoni mwa wiki hujaa wageni wanaoenda kwa ajili ya starehe.
 
“Hatujafurahi hata kidogo, lakini hatuna la kufanya na hii kuvunja chupa ni kuonyesha hasira zetu kwa sababu chaguo la Wazanzibari tokea uchukuaji wa fomu za urais wa CCM ni Dk Bilal,” alisema Kijana mmoja.
 
Juzi Halmashauari kuu ya CCM, ilimtangaza Dk Shein kuwa mshindi baada ya kupata kura 117 na kuwashinda wapinzani wake Nahodha aliyepata kura 33 na Dk Bilal ambaye alipewa nafasi kubwa ya kupitishwa akaambulia kura 55.

Mjini Dodoma mara baada ya kutangzwa matokeoa hayo, wafuasia Dk Bilal na Vuai walikchukia, baadhi yao walitupa kofia na mashati ya CCM nje ya ofisi za chama makao makuu na kuahidi kutoshiriki katika kampeni za kumnadi Shein.

Wana CCM, hao zaidi ya 200 ambao waliondoka jana asubuhi mjini hapa na kurejea Zanzibar, walisema wamechoka kuchaguliwa Rais wa Zanzibar na viongozi wa CCM Tanzania bara na sasa wanataka mabadiliko katika Katiba ya CCM, ili Rais wa Zanzibar achaguliwe na Wazanzibar wenyewe.

"Hatutaki..., huyo siyo mgombea wetu…, tumechoka kuchaguliwa Rais Zanzibar,” umati wa wanaCCM toka Zanzibar ulipiga kelele mara baada ya taarifa kuvuja kuwa Dk Bilal na Nahodha hawakuchaguliwa.

“CCM Zanzibar imekufa na sasa bora CUF ichukuwe nchi," walisema wanaCCM hao.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kada wa CCM  Zanzibar, Baraka Mohamed Shamte aliyewahi kuwa katibu wa CCM wilaya za Wete, Unguja mjini na Pangani mkoani Tanga, alisema hawakuridhika na matokeo ya kura za wajumbe wa halmashauri kuu, sasa wameamua watafanya mgomo baridi wa kususia shughuli za CCM na kampeni.

"Kwanza mgombea mwenyewe sisi hatumkubali, kwa vile hana kura Zanzibar,"alisema Shamte.


Hata hivyo, dalili za kutopata kura za kutosha kwa Bilal na Nahodha, zilianza kuonekana mara baada ya kuanza kikao cha halmashauri kuu ambapo wajumbe wengi wa bara walionesha wazi kutaka kupiga kura za kiitifaki na kumpa ushindi Shein.

Katika kuhesabu kura Dk Bilal alimteua Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango kumhesabia jambo ambalo liliwashangaza wengi.

Licha ya wafuasi wa Dk Bilal wengi wao wakiwa ni akina mama na vijana wa maskani mbalimbali, kwa takriban siku tatu walikuwa wakipiga kampeni nzito ya katika nyumba za kulala wageni hasa wajumbe wa NEC, hali ilibadilishwa ukumbini taarifa ya kuvuja taarifa za kamati kuu kuwa jina la Shein ndio liliongoza.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili katika mji wa Zanzibar ulibaini usiku mzima wa juzi na jana asubuhi vijiwe kadhaa vilikuwa kimya, kuashiria hali ya huzuni.

Vijiwe vya kahawa na maskani za CCM ikiwemo ya Kaka ya Kisonge ambayo hutawaliwa na shamra shamra wakati wa uteuzi wa mgombea urais vilikuwa kimya.
 
Mazingira ya ukimya katika maskani za CCM jana mjini hapa zilifuatiwa na kuwasili kimyakimya kundi la wana CCM waliosusa kikao ambalo lilikuwa likimuunga mkono Dk Bilal na Nahodha.
 
Baadhi ya wana CCM hao waliozungumza na gazeti hili mara baada ya kuwasilia kutoka Dodoma , walisema hawakuridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi na wanaimani kwamba, kuna njama zilizofanywa na CCM bara katika kuteua mtu ambaye wao wanamtaka.
 
Baraka Shamte ambaye ni mwana CCM alisema katiba ya CCM ni mizengwe na inahitaji mabadiliko ya haraka ili Wazanzibari wasichaguliwe kiongozi wao na watu kutoka Tanzania bara.
 
“Tumepokea uteuzi wa Shein shingo upande na baadhi yetu hatushiriki katika harakati zozote za kampeni ya uchaguzi kwa sababu sio chaguo letu. Lazima katiba ya chama ibadilishwe wazanzibari tusichaguliwe kiongozi,” alisema kwa hasira Shamte.
 
Alisema hata kama Dk Bilal atapewa nafasi nyingine ya juu kama vile makamu wa rais bado kiu yao haijamalizika kwa kuwa lengo lao ni kutaka awatumikie Wazanzibar na sio jamhuri ya muungano wa Tanzania.
 
Naye Said Hassan alisema utaratibu wa kuchagua rais ndani ya chama Zanzibar lazima limalizikie Zanzibar kwa vile, jambo hilo linawahusu Wazanzibari wenyewe.

Mmoja wa wafuasi hao ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema wanajipanga kuangalia mustakabali wao katika CCM na kwamba, ikiwezekana wanaweza kuondoka.
 
“Tuna masikitiko makubwa kwamba hatutaweza kuzungumza nanyi (waandishi) kwani tumepokea maagizo kuwa tusizungumze chochote kuhusiana na matokeo ya uchaguzi Dodoma. Hivi sasa tunakwenda zetu nyumbani tukiwa na huzuni kubwa,” alisema mfuasi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.   
 
Taarifa za awali zilizosambazwa kwa vyombo vya habari Zanzibar zinasema kundi hilo la wafuasi wa Dk Bilal lililotoka Dodoma lilipanga kunfanya mkutano na waandishi wa habari baada ya kuwasilia saa 9:30 bandarini, lakini baadhi yao walieleza kuwa wamepokea taarifa kutoka Dodoma kwamba, wasizungumze lolote.
 
Baadhi ya wafuasi hao walikataa kutii agizo hilo wakilalamika kuwa hawakutendewa haki na kutishia kukihama chama na kwamba, waandishi wa habari wahudhurie siku ya kurejesha kadi zao za CCM kwa chama watakachojiunga ambacho watakitaja baadaye.
 
Mashabiki hao walionekana wakiwa na hasira kubwa walidai hata sare za CCM walizivua mjini Dodoma mara baada ya kutangazwa Dk Shein.
 
“Tunaomba waandishi mtupe muda zaidi mtapata baadaye na tunaomba hizo kamera zenu kwanza wekeni chini kwa sababu hatutaki kupigwa picha.

"Chama kimetuangusha na kimetuvunja moyo sana wana CCM Zanzibar na tunajitayarisha kurudisha kadi za CCM, lakini kwanza hatusemi tutajiunga chama gani,” walisema mashabiki hao huku wengine wakiwa wamejifunika nyuso zao.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wazanzibar wakiwemo wana CCM wanaounga mkono maridhiano wamepokea kwa furaha uteuzi wa Dk Shein wakisema ni kiongozi pekee atakayeweza kuwaunganisha Wazanzibari.
 
“Tumefurahi sana na tumepokea uamuzi wa Nec kwa furaha ingawa wengine wamekasirika kama mnavyoona. Lakini sisi tumefurahi na tunaomba wana CCM wenzetu tuungane ili tujenge chama chetu, tusiwape mwanya wapinzani wetu,” alisema Omar Ali Haji.



 
 Kutoka Mwanza, Fredick Katulanda anaripoti kuwa baadhi ya wakazi wa mji huo wamesema kuteuliwa kwa Dk Shein kutamaliza makundi ndani ya CCM, hivyo kuifanya Zanzibar kuwa tulivu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa TCCIA Taifa, Amran Batenga alisema kuteuliwa kwa Shein kunaweza kumaliza makundi ambayo yamekuwa yakisumbua kila mara katika siasa za Zanzibar.
            
“Mimi naona ni uteuzi mzuri, wameteua mtu ambaye haoneshi kuwa na makundi, wameteua mtu kutoka Pemba, safi, nadhani CCM imedhamiria katika uchaguzi huu kukomesha Upemba na Uunguja,” alieleza Batenga.

Naye Mwita Frank alisema ameupokea uteuzi huo wa CCM kumteua Dk Shein kama ishara ya kushindwa na kuanguka kwa CUF kwa vile kila mwaka wa uchaguzi kimekuwa kikitumia nguvu ya wananchi wa Pemba kujinadi.

Naye, Jumanne Isaya alisema uteuzi huo wa CCM umepotea njia kwa vile utatoa nafasi ngumu ya CCM kuishinda CUF kutoka na uteuzi kuzaa makundi kwa vile Wazanzibari wanaamini kuwa Dk Shein ni changuo la bara na siyo lao Zanzibar

“Ni uteuzi mzuri kwa vile ni mtu makini, lakini kwa siasa za Zanzibar bado naona hawajatibu kitu, utazuka mvutano kwa sababu wao wanaamini kuwa uteuzi wake unashinikizo la CCM Bara na wala siyo la CCM Zanzibar” alieleza.

Kutoka mkoani Mara, Imeripotiwa kuteuliwa kwa Dk Shein kuwania nafasi ya urais kupitia CCM, kumepokelewa kwa hisia na mitazamo tofauti.
            
Akielezea uteuzi huo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mugumu wilayani Serengeti Padri Aloyce Magabe alisema CCM wametumia hekima kumteua Dk Shein kwa kuwa ni miongoni mwa viongozi waliolitumikia Taifa hili bila kukumbwa na tuhuma za ufisadi.
 
 "Huyu ni chaguo la watu na hata Mungu maana hajawahi kukutwa na tuhuma, amekuwa akishughulikia mambo kwa utulivu," alisema.

Padri Magabe ambaye ni mchambuzi wa mambo mbalimbali alisema ana imini kuwa Shein atuweza mzigo huo kwa kuwa tayari ana uzoefu kwa vipindi viwili
akimsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano na kwa kuwa anatoka Pemba basi.
          

Kutoka Bukoba imeripotiwa kwamba baadhi ya wazee wa mji wa Bukoba limeishauri kuwa kundi la mgombea aliyeshindwa kudhibitiwa ndani ya chama kwa vile linaweza kuendesha kampeni chafu ili kumharibia Dk Shein katika uchaguzi.

Walisema kundi la Dk Bilali linaweza kuibuka kutokana na ukweli kuwa lilikuwa na nguvu na lilishajiwekea matumaini ya kushinda katika mchakato huo hivyo huenda likawa na kinyongo.

Miongoni mwa wazee hao Justus Mutalemwa alisema matokeo yaliyompa ushindi Dk Shein yanaonyesha pia wapinzani wake walikuwa na nguvu hali aliyosema huenda ikaleta mazingira magumu ya kisiasa kisiwani humo.

Mathias Balige, mkazi wa Hamuembe mjini Bukoba alisema kulikuwa na mazingira ya wazi ya baadhi ya viongozi ndani ya chama kumbeba mgombea aliyeshinda.

 Alisema hali hiyo huenda ikazidi kuchochea chuki na kufanya kampeini za kumnadi mgombea huyo kutiwa dosari katika uchaguzi.
Balige alisema huenda ukatokea mgawanyiko mkubwa kuelekea katika kipindi cha kampeini.

Alipoulizwa kama mgombea huyo ataweza kuwaunganisha Wazanzibari na kuyavunja makundi yenye uhasama, alisema sio rahisi kumaliza nguvu ya makundi yenye uhasama kwa kuwa mtandao wa kundi lake umehusika kumpatia ushindi.
Wakati huo huo, Katibu Wakati huo huo; Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Dk Shein kwa kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM  kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

“Nampongeza Dk Shein kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi…hii inaonyesha imani waliyonayo wanachama wenzake wa CCM kwake na uongozi wake…binafsi nimepokea uteuzi wake kwa furaha kubwa sana,” alisema Seif ambaye atashindana na Dk Shein katika uchaguzi mkuu.

Katika taarifa yake, iliyotolewa na msaidizi wake, Ismail Jusa, Seif alisema anaamini Dk Shein ni mtu makini, msomi, mwenye uwezo, busara, hekima na asiyependa makuu.

Alisema kutokana na sifa hizo, anaamini Dk Shein ataweza kuondoa makundi ndani ya chama chake.
 
“Kupatikana kwa umoja ndani ya CCM kutamwezesha Dk Shein kushirikiana na sisi na vyama vingine vyote vya siasa ili, kwa pamoja, tujenge umoja mpana zaidi kwa Wazanzibari wote,” alisema.

Kiongozi huyo wa CUF alisema ametiwa moyo sana kwa kauli ya Dk Shein kuwa anaunga mkono  na  atatekeleza na kuendeleza maridhiano yaliyoanzishwa na Amani Karume na yeye (Seif).     

Alisema anaamini kwa hulka yake, Dk Shein na yeye kwa pamoja, wataweza kuleta siasa mpya za maelewano kwa Wazanzibari wote, zenye lengo la kuleta maendeleo makubwa na ya haraka.

Habari hii imeandaliwa na Salma Said - Zanzibar, Phinias Bashaya - Bukoba na Frederick Katulanda - Mwanza na Samuel Kamndaya  Dar.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Sunday, 11 July 2010 10:14
 

Comments 

 
0 #13 2010-11-02 11:10
hongera dr shein kwa kushinda
Quote
 
 
0 #12 2010-07-16 18:30
Wazanzibar mna haki huyo mzee kwanini asipumuzike? tangu enzi za Mkapa anauchu wa madaraka! nawaambia ukweli mkataeni maana hata security wake nyumbani kwake awezi hata kuweapa mabaki ya chakula mkimchagua mtalia amini nawaambia
Quote
 
 
0 #11 2010-07-16 13:07
KIGUMU CHAMA MAPINDUZI !
UTEUZI WA MGOMBEA WA URAIS SAFARI HII NI MWIBA KWA WALE WASIOITAKIA MEMA ZANZIBAR WANZANZIBARI WAMEBAGULIWA NA KUNYANYASWA KWA SABABU YA ASILI ZAO TU .

DKT BILALI ALIKUA NI MTU MAKINI NA WA KUHESHIMIKA ALIUNGANA NA GENGE LA KISHAMBA KINA SALMINI WAKAIHARIBU ZANZIBAR KWA CHUKI NA UBAGUZI TUNA MSHUKURU MOLA KARUME ALIWAPIGA NA CHINI WOTE WAKABAKI WASIJUE LA KUFANYA BILALI ALIRUDI CHUONI KUFUNDISHA ,SALMINI HAJULIKANI MBELE WALA NYUMA JUZI KAINGIA DODOMA NA SARE ZA CUF BLUE GUARD HATA ZA CCM ZILIMSHINDA KUVAA.

DKT BILALI HAKUWA NA NIA YA KULETA UONGOZI MWEMA ZNZ ALIKUA NA LENGO KUJA KULIPIZA KISASI KWA UONGOZI WA KARUME LAKINI KASAHAU KARUME NI MTOTO WA MJINI . BILAI MSHUKURU MOLA WAKUPA FAVOUR KUBWA JIANAGALIE AFYA YAKO KWANZA UMECHOKA KINOMA INABILI CCM WAKUSAIDIE TENA WAKUFANYIE SERVICE YA NGUVU MEDICAL ! UMEWAACHIA WAKATI MGUMU WAHUNI WA KISONGE NA WENGINE FAGIO LA CHUMA LINAKUJA SOMA WAKATI. MUNGU IBARIKI ZNZ.
Quote
 
 
0 #10 2010-07-15 17:18
HAta kama wunguja hawampendi Shein , inabidi wakubaliane na hali hiyo kwani kwa muda mrefu Zanzibar imepata viongozi wake wa juu kutoka Unguja na siyo Pemba, kwani Pemba inawtu wasomi wazuri tu na wenye nidhamu ya kazi na wito wa kufanya kazi kama Dr Shein.
Sifa kubwa ya Shein ni mtu ambaye hana makundi yeye yupo na anfuata katiba na mwongozo wa chama chake kwamba sasa tunataka nini natufanye nini ili tuweze kusonga mbele.
Zanzaibar wamepata kiongozi mzuri na mwadilifu na mwenye kuwatumikia wananchi hasa wazanzibar maana alivyokuwa makamu wa rais tumeona akiongoza kwa busara bila kusikia kelele wala ugomvi na mtu yeyote ndani ya ccm na nje ya ccm.
Quote
 
 
0 #9 2010-07-14 23:16
DK Sheni Mzee wangu mfupa aloshindwa fisi wewe huwezi.
Quote
 
 
+1 #8 2010-07-14 06:08
alichokifanya KIKWETE NI RUSHWA YA WAZI kwa mawazo yangu kwa maana unapompa cheo(kishawishi ) mtu kwa ajili ya kumnyamiza mtu ili asiende kinyume na unavyotaka wewe(faida binafsi na siyo kwa manufaa ya nchi)ni sawa na mtu mwingine yeyote anayempa polisi fedha ili aweze kutimiza malengo yake binafsi. kuna mazingira yaliyopelekea bilal kupewa cheo na kwani kama Bilal asingepewa cheo hicho kama asingeshiriki kwenye kinyanganyiro cha kugombea urais.kwahiyo kuna USHAHIDI WA KIMAZINGIRA UNAONYESHA KUWA RAIS KIKWETE KATOA RUSHWA(CHEO) KWA AJILI YA KUMNYAMAZISHA MUHUSIKA ASITIMIZE MALENGO MENGINE KINYUME NA MATARAJIO YAKE.
Quote
 
 
0 #7 2010-07-13 15:57
Lengo kuu la uongozi ,ni kuongoza kwa uadilifu , na kutatua shida za wanyonge, na raia wa kawaida , pia kuleta maendeleo mazuri ya taifa,
yoyote yule kiongozi aloyechaguliwa inatakiwa awajibike na mambo hayo.
kuleta mabadiliko, unafuu wa maisha upatikane, sio mengine, lakini viongozi wengi wa tanzania wao ni kujilimbikizia mali tu, kuiba fedha za umaa tu, kuanzia ngazi ya wakurugenzi hadi raisi mwenyewe,
jee hiii kweli tutafika?
mimi nafikiri Tanzania haita endelea hadi mwisho wa dunia itakuwa ni hivi hivi tu, watu kupishana ,urais, kaa miaka kumi yako hiyo, kula iba, nyanganya, ukimaliza akae mwengine ,na kundi lake nao wanyinufaishe wao na familia zao, hadi mwisho wa dunia.

Ukweli ni kuwa karibu Viongozi wote khutembea nchi za wenzetu huona yale mazuri , ya maaana na maendeleo . huwa hawayachukui wakaja kuwasaidia wananchi wao nao wafaidike, yaani ziara za nje ni shopping na kutembea tu.
kwa kweli awe Shein, awe bilal, wananchi wanachotaka ni kuwaondolea ugumu wa maisha, na kubuni njia za kuleta b maendeleo ya nchi.
Hao wote ni Viongozi, kila mmoja ana taaluma tofauti na zote taaluma zao ni muhimu na zinafaa, haina haja ya kuwabagua,
kama lengo ni maendeleo basi ni kushirikiana kuleta hayo maendeleo ya kweli,
nadhani inatosha tujengeni nchi wenzangu,
tusichague sanaaa, tushirikiane tujenge nchi
tusikae tuaakamini labda siku moja tanzania itakuwa kama ulaya hiyo katu.
wenzetu wanajituma viongozi wanawajibika, wankwenda mbele sii wizi na kwenda mbele
tuaache tujenge nchi
Quote
 
 
0 #6 2010-07-13 13:52
CCM ni chama makini, na pia kina mtizamo makini pia, hakuna asyejuwa kuwa jinsi wazanzibari walivyokuwa miaka 4 iliyopita, chuki wenyewe kwa wenyewe, hawazikani, wanachomana moto usiku, CUF hawapandi gari za abiria za wana CCM, halikadhalika CCM pia hawapandi gari za watu wa CUF,hata biashara hanunuwi mtu kitu ktk itikadi tofauti, sasa tumefikia makubaliano na tumeanza vizuri Alhamdulillah Karume na Seif wameanza kuyamaliza sasa CCM imeona mbali bila hivyo yangerudia yaleyale!!Na hao wanaodai wamechaguliwa mtu siye waliemtaka ni katika haox2!! Maana wanaitikadi kuwa Mpemba hawezi kutawala ZNZ kwa hiyo sasa ni rikodi mpya maana hata CUF au CCM akipata ni MPEMBA ndio kiongozi na mtashangaa huyo Shein atakavyopaa kwa kupata kura nyingi!
Quote
 
 
0 #5 2010-07-12 15:22
ndugu observer sikubaliani na kauli yako kwamba Dr BILAL amefanyiwa favor kwa kuteuliwa kua mgombea mwenza..
hii ni ccm kutaka kuwazima wazanzibar tu na sio jengine. KUMBUKA KWAMBA DR AMETUMWA NA WAZANZIBAR NA SIO MTU MWENYE UCHU WA MADARAKA BALI ALIKUA ANAITIKIA WITO, hata hivyo ni bora tufunike kombe mwanaharamu apite tusijaribu ku[NENO BAYA]noa mambo kwani sio jambo jema. yalopita sio ndwele na tugange yajayo.kamati kuu ya chama sio wapiga kura wapiga kura ni hao wananchi wanaolia kwa kupandikiziwa mtu.
ni jabu la busara kwa kikwete wala sio FAVOR kumteua dr bilal ili kutibu donda kwani bila ya ushirikiano wa pande zote mbili basi ushindi kwa ccm zanzibar utakua ndoto.na ninathubutu kusema Dr bilal ndie aliefanya FAVOR kwa ccm kwa kuridhia kua mgombea mwenza wala sio vice vercer
Quote
 
 
+1 #4 2010-07-12 13:06
kwa mtizamo wangu nisiyekwenda shule GABRIELI umeongea point.tena umeongea point, na nasisitiza umeongea point. kwa mtizamo mpana kama huo nahisi hata mwana CCM kutoka Tanganyika anastahili kukasirishwa na upatikanaji wa Sheni. misingi iliyotumika kumpata Sheni ndio iliyozoeleka kwa CCM kujipangiazia watu katika majimbo hata kama hawafai. aina zote za Rafu kuanzia kupindisha sheria hadi matumizi ya rushwa na nguvu kuhakikisha mtu anaeweza kulinda maslahi ya hao wala mali wachache anapata uongozi. na akishapitishwa eti na sisi tunamchagua hivyo hivyo hata kama hafai ilimradi amewekwa na CCM. imefika mahali maslahi ya wafanyakazi wanafaidi watu wachache na sisi tunaojiita masikini wa mungu ( sio wa kujitakia) tunaambiwa tuwe wabunifu kufanya biashara katika mazingira magumu yaliyojaa wizi na ujambazi, maradhi na ukame, riba kubwa na makodi ya kila aina tena bila ya hata mitaji wala masoko ya uhakika. mitaji kutoka katika rasilimali hizo alizotupa MUNGU wanabarikiwa wahindi na waswizaland kwa 15% zinazoishia mifukoni mwa wanaopandikizwa kututawala sio kutuongoza. lakini you can fool some people some time but you can't fool all the people all the time
Quote
 
 
-3 #3 2010-07-12 12:06
"Alisema hata kama Dk Bilal atapewa nafasi nyingine ya juu kama vile makamu wa rais bado kiu yao haijamalizika kwa kuwa lengo lao ni kutaka awatumikie Wazanzibar na sio jamhuri ya muungano wa Tanzania".

Inaonyesha jinsi gani hili kundi lilivyo na upeo mdogo wa kufikiri. Msitubabaishe hapa, Kwanza hata kumteua Bilal kuwa running mate wa JK ni favor na politically wise decision, si kwa kuwa ana the best VP qualifications. Ndio maana hakupewa nafasi ya kuongea.
Quote
 
 
-1 #2 2010-07-12 11:52
'Dk Shein ni mtu makini, msomi, mwenye uwezo, busara, hekima na asiyependa makuu". Kwa hili hakuna mtu atakaebisha. Tatizo ni kwamba kulikua na ufisadi kumteua na Wazanzibari hawakubali mfumo mzima wa utaritibu uliotumika kwenye uchaguzi. Wengi wanaamini kuna "foul play" na wengi wanauliza CCM bara wana haki gani ethically kumsimika kiongozi Zanzibar. Nafikiri Dr. Shein atakua na wakati mgumu kuondoa kansa ya makundi inayoitafuna CCM kitaifa. Kama hatapata ushirikiano, hataweza kamwe kutekeleza sera yoyote ile hata awe mtaaalmau kiasi gani. "mpeleke ngamia kisimani lakini huwezi kumlazimisha kunywa". Tumeshuhudia yaliyotokea Dodoma kumteua kibabe kiongozi wa visiwani. Hili litarudiwa kuwachuja na kuyaondoa majina wa viongozi bora walio chaguo la Watanganyika ili CCM ihakikishe inawarudisha vibaraka wao kupe mafisadi waendelee kulindana na kujinenepesha na damu ya walalahoi. Endeleeni kusali!
Quote
 
 
0 #1 2010-07-11 16:21
Hongera Dr. Shein; nadhani watanzania wenzangu ni vyema tukamuunga Mkono; si mtanzania? Kwani ni mkenya au mnataka Mkenya awe rais wa Zanzibar; mchagueni ili alete mahusiano mazuri kati yetu; wabara na wavisiwani. Wakati ndio huu ambapo watanzania wote tunatakiwa kuhamishia nguvu zetu katika kujenga muungano wetu; Dr Shein na wenzake wana kazi moja muhimu; kutuimarisha na kuhakikisha kuwa muungano wetu na Zanzibar unapewa kipaumbele mara milioni moja ukilinganisha na Africa ya Mashariki;
Hongera Dr. Shein na ndugu zangu wanzazibari na wabara tumuunge mkono kwa kuwa ni mwenzetu; wanaopinga mnataka awe rais wa wapi?
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner