
| Vigogo wamiminika kupata dawa Lolindo | Send to a friend |
| Sunday, 06 March 2011 10:26 |
|
MAELFU ya watu, wakiwemo vigogo wa serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa nchini, wamefurika katika Kijiji cha Samunge, Sale, wilayani Ngorongoro kupata 'dawa ya maajabu ya Mungu' inayodaiwa kutibu magonjwa mengi sugu ikiwamo Ukimwi. Helkopta za wafanyabiashara na magari zaidi ya 1,000 yakiwamo magari ya Serikali, binafsi na mashirika ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya ya Afrika Mashariki, yamefurika katika kijiji hicho kilichopo umbali ya takriban kilometa 400 kutoka jijini Arusha. Baadhi ya wabunge na vigogo wa serikali na vyama vya siasa na watendaji wa mashirika mbalimbali ya kimataifa, waliliambia Mwananchi Jumapili kwa sharti ya kutotajwa majina kwamba walikwenda kupata tiba kwa mchungaji huyo. “Mimi nipo hapa tangu juzi, nimepata dawa na kuna watu wangu wanahangaika kupaita. Nina imani watapata leo na baadaye narudi jimboni kwangu,” alisema Mbunge huyo wa jimbo moja mkoani Arusha. Kigogo mwingine wa jeshi la polisi, alisema alifika kupata tiba hiyo kwa ajili ya tatizo la kisukari na shinikizo la damu na kwamba tangu anywe dawa hiyo anajisikia vizuri. “Mimi nilikuja huku baada ya kupewa taarifa kuwa bosi wangu alikuja huku na baada ya tiba hiyo ameshapona,”alisema afisa huyo wa polisi. Dawa hiyo inatolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile (76), ambaye anasema alionyeshwa Mungu katika ndoto ili aitumie kutibu watu tangu mwaka 1991. Mchungaji Mwasapile ambaye alifanya mahojiano na Mwananchi Jumapili nyumbani kwake wakati akiendendelea kutoa dawa kwa wagonjwa wake, anasema aliendelea kuota ndoto hiyo hadi Agosti 26, 2011 alipoanza rasmi kuitumia dawa hiyo kutibu watu. Anasema dawa hiyo inatokana na mti aina ya mugariga na yeye pekee ndiye anaweza kukupatia na kunywa kikombe kimoja tu na kwamba baada ya kunywa inaanza kazi ya kutibu maradhi sugu kama ukimwi, kisukari, pumu na saratani. Mchungaji Mwasapile anasema gharama ya dawa hiyo ni Sh500 tu na dozi yake ni kikombe kimoja(hairuhusiwi kurudia kuinywa). “Mungu aliniotesha kutoa dawa hii kwa Sh500. Aliponiambia hata mimi nilishangaa. Kwanza aliniambia niwape watu wapone saratani, kisukari, pumu na magonjwa mengine na baadaye akanionyesha kuwa dawa hii niwape hata wagonjwa wa ukimwi nao watapona,“ anasema Mwasapile. Anasema Mungu amemwonyesha kuwa watu wa mataifa mbalimbali, watakuja Tanzania katika Kijiji cha Samunge kunywa dawa hiyo na watapona. Hata hivyo, anasema sasa anakabiliana na changamoto ya wingi wa watu wanaofika kupata dawa hiyo. "Sasa ninahitaji dawa zaidi ya kuchemsha, maji mengi sana na usafiri wa kufuata dawa nyingi kwa wakati na eneo la kutolea matibabu kwa sababu hapa nilipo hapatoshi kwa umati mkubwa uokuja," alisema. “Naomba Serikali inisaidie kupata usafiri wa vijana kwenda kuleta dawa porini kwani ni nyingi sana, pia vyombo vya kuchemshia dawa na vikombe vya kutolea dawa pamoja na kuboresha barabara ya kuja hapa kwani ni mbaya sana,” anasema Mchungaji Mwasapile. Mchungaji Mwasapile anasema hajawahi kutangaza mahala popote tangu alipoanza kutoa dawa hiyo, ila wananchi waliopona waliwaeleza ndugu na jamaa zao ambao walikwenda kwake nao walipopona waliwaeleza wengine. “Haya ni maajabu ya Mungu na wenye imani na Mungu wanapona, wanakuja kuniambia tunashukuru tumepona na tunaendelea vizuri,” anasema Mchungaji huyo. Kutokana na wingi wa watu, kuanzia juzi (Ijumaa) askari wa Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakishirikiana na mgambo, waliweka ulinzi kulinda usalama na kuhakikisha watu wanapata dawa bila kutokea vurugu. Mamia ya wagonjwa ambao baadhi yao walifikishwa kijijini hapo wakiwa wamebebwa katika magodoro na machela, mara baada ya kunywa dawa hiyo walisema wamepata nafuu. Mapema juzi, nusura watu wavunje nyumba ya tembe ya mchungaji huyo kutokana na vurugu za kugombea dawa hatua ambayo kuanzia jana, ilisababisha watu kupewa dawa wakiwa katika magari yao. Baadhi ya wananchi kutoka mikoa ya Dodoma, Kagera, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Zanzibar na jijini Dar es Salaam waliofika katika eneo hilo kupata huduma hiyo waliomba Serikali isaidie kuweka utaratibu utakaosaidia dawa hiyo kupatikana kwa utaratibu mzuri. Wilson Maina, Abdalah Athuman na Fadhila Omar walisema, wamekaa siku tatu juzi katika eneo hilo, lakini bado hawajapata dawa kutokana na utaratibu ambao unahitaji kutumia nguvu kuipata dawa. Fadhila anayetoka mkoani Dodoma alisema alifika hapo tangu Jumatano iliyopita , mpaka juzi alikuwa hajapata tiba kwa sababu utaratibu mgumu wa kupata dawa hiyo. “Wameanza kutoa dawa kwa wenye magari pekee, sisi wengine magari yameondoka hatujui tutapata lini dawa na katika eneo hili hakuna chakula,” anasema Fadhila. Naye Maina aliyesema kuwa ametokea Arusha alieleza kuwa aliimba Serikali isaidie kuweka utaratibu mzuri wa kupatikana dawa hiyo kwa kuongeza ulinzi. Kwa mujibu wa Maina, maeneo mengine yanayohitajika kuboreshwa hasa la kutolewa dawa na huduma zingine ikiwamo vyoo na malazi. “Watu wanalala chini, hakuna vyoo, wala hoteli. Pia barabara ya kufika hapa ni mbovu sana. Tunaaomba Serikali itambue mchango wa babu huyu ili asaidiwe watu wengi zaidi kwa urahisi,” alisema Maina. Makundi ya wafanyabiashara wa kiasia na wengine kutoka nje ya nchi wakiwa na magari yao pia walifika kwa mchungaji huyo anayejulikana kwa jina la babu na juzi walikuwa kwenye foleni ya kupatiwa dawa. “Sisi tumekuja kupata dawa tu hapa, mimi ninasukari wenzangu wengine BP, wengine pumu,”alisema mkurugenzi mmoja wa kampuni kubwa ya usafirishaji jijini Arusha mwenye asili ya kiasia. Hadi kufikia juzi mchana mengi ya magari yalikuwa yakielekea katika kijiji hicho na gharama za usafiri kwa magari ya kukodi kutoka jijini Arusha sasa ni kati ya Sh 80,000 na 100,000 huku mabasi ya kawaida yakitoza kati ya Sh40,000 na 65,000. Amani Msemo ambaye ni dereva wa gari la Kampuni ya Utalii ya Big Expedition ya Arusha anasema amekodishwa na wananchi kufika katika kijiji hicho kwa kila mmoja kulipa 80,000 na gari lake linabeba takriban abiria 10. “Magari ya kampuni yetu matatu yamekodishwa na kuna magari ya makampuni mengine ya utalii zaidi ya 200 yapo hapa yamekodiwa,”anasema Msemo. Kuna magari basi ynayotoka mikoa mingine yanayosafirisha wagonjwa kwenda katika kijiji kupata tiba hiyo. Akizungumzia Mchungaji huyo kupitia TBC juzi usiku, Naibu Waziri wa Afya, Lucy Nkya alisema Serikali inafuatilia dawa za zake na kwamba kwa kuwa ni za miti shamba zitachunguzwa, zikithibitishwa kuwa hazina madhara kwa watumiaji haziwezi kuzuiwa. Hata hivyo, Naibu waziri huyo aliwaonya wagonjwa wanaopata matibabu ya HIV, kuacha kutumia matibabu ya kitalaamu na kutumia dawa za mchungaji huyo pekee. Lakini baadhi ya watu waliokuwa wamepimwa hospitalini na kuonekana kuwa na maambukizi ya HIV walieleza jana na juzi kuwa baada ya kupata dawa hizo wanasikia ahueni. Mmoja wa wagonjwa hao alisema kesho anatarajia kwenda hospitalini kupima afya kujua maendeleo yake. “Mimi nilikuwa na HIV nimekunywa dawa ya mchungaji sasa najisikia vizuri. Kabla ya hapo nilikuwa nashindwa kutembea, nikapelekwa na ndugu zangu kwa babu (mchungaji) sasa nahisi kupona kabisa. Nitapima kesho, lakini kuna mwanakikundi mwenzagu amepona kabisa baada ya kutumia dawa hizo,”anasema Lyimo. Msaidizi wa mchungaji huyo, Marko Nedula alisema kutokana na wingi wa watu, tayari Askofu wa KKKT jimbo la Arusha, Thomas Lazier aliwatembelea na ameahidi kusaidia upanuzi wa eneo la kutolea dawa. “Juzi Askofu alikuja, tumefanya naye vikao na ametuahidi kuwa atasaidia ujenzi wa eneo zuri la kutoa huduma nasi tuna imani tutafanikiwa,” alisema Nedula. Katika hatua nyingine, Anthony Mayunga anaripoti kutoka Serengeti kuwa huduma ya mchungaji huyo imeongeza hamasa ya watu kupima afya zao kujua hali zao ili wakiwa nao wawahi kupata dawa hiyo. Kutoka Wilayani Serengeti habari zimesema wakazi wa Mugumu na viunga vyake wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupimia virusi vya Ukimwi, ili kwenda kupata dawa hiyo wilayani Loliondo. Mwananchi Jumapili ilibaini kuwa vituo vya Imara na hospitali teule ya Nyerere vinafurika watu wa rika mbalimbali wanaokwenda kupima maambukizi ya HIV ili kujua afya zao. “Watu wanaokuja kupima maamvukizi ya virusi vya ukimwi wameongeza ghafla. Wengi wao wanasema wanataka kujua kama wameambukiswa VVU wawahi kwa mchungaji kupata dawa,”alisema mmoja wa wahudumu wa afya katika hospitlia ya Nyerere. Kauli ya Mkuu wa Mkoa Moses Mashalla anaripoti kutoka Arusha anaripokuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Isdori Shirima, ameunga mkono huduma ya mchungaji huyo.Shirima alisema Serikali mkoani Arusha haina tatizo na huduma hiyo maadamu haihatarishi usalama wa raia na mali zao. “Serikali mkoani Arusha haina tatizo na mchungaji huyo maadamu hahatarishi usalama wa raia na mali zao,”alisema Shirima. Shirima ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Arusha, alismea kuzuia tiba hiyo ni kuwanyima haki wananchi wanaoamini kuwa wanaweza kupona kwa dawa hiyo. |
| Last Updated on Sunday, 06 March 2011 16:38 |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani















Comments
SO MUNGU ANAMAKUSUDI NA SS TANZANIA. ILA TU VIONGOZI MSITUBANIE KAMA KAWAIDA YENU
naiyomba serikali ikamlinde babu kwani watu wengine haswa wenye kuhubiri injili wamebaki viti tupu je watapata wapi tene waumini wa kila siku? jamani naiyomba serikali yetu na naamini mungu ameipenda nchi yetu sana kutokana na amani , utulivu uliyopo chini ya rais wetu mpendwa, maoni yangu nikwamba babu yetu apate ulinzi sana, asijekorofishwa na wagonjwa akatoweka,hakik a wagonjwa watalia sana
hakika viongozi wetu wameguswa sana na hali hii hivyo namwombwa mheshimiwa rais wetu atoe ulinzi makini kwa babu