|
Tanesco yadaiwa kusababisha hasara kiwanda cha saruji |
Send to a friend |
|
Sunday, 22 January 2012 09:40 |
|
Burhani Yakub,Tanga KAMPUNI ya Saruji ya Tanga, imekuwa ikipata hasara ya kati ya Sh80 milioni na Sh400 milioni kila mwezi kufuatia tatizo la kukatika ghafla kwa huduma za umeme mara kwa mara kunakoathiri mzunguko wa vinu vya kulainisha malighafi katika kiwanda chake.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hityo, Erik Westerberg katika taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa, kuhusu uzalishaji wa saruji katika kiwanda hicho.
Alisema kitendo cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukata mara kwa mara na kwa ghafla, kinaathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa saruji na hivyo kuisababisha kampuni hasara kubwa.
“Umeme hafifu wa Tanesco pamoja na kukatika ghafla mara kwa mara kwa nishati hiyo unaathiri kwa kiasi kikubwa mzunguko wa vinu vya kulainisha malighafi ambavyo kwa kawaida vinapaswa kuzunguka kwa saa 24 bila kuzimwa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema tatizo lingine linalokikabili kiwanda hicho ni upakuaji wa shehena ya malighafi katika Bandari ya Tanga ambayo kutokana na kina chake kuwa kifupi, kuna kuwa na ulazima wa kutumia matishari zinzosafirisha kwenda mahali kwenye maji marefu ambako meli kubwa zinakuwa zimetia nanga.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema saruji inayozalishwa na kampuni yake inaongoza kwa ubora katika nchi za Afrika Mashariki, jambo linalosababisha kuwapo kwa mahitaji makubwa.
“Tumeongeza uzalishaji kutoka tani 651,841 mwaka 2007 hadi kufikia tani 933,346 mwishoni mwa mwaka jana,”alisema Westerberg.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho,Gallawa aliwapongeza wawekezaji hao kwa kuimarisha kiwanda hicho na kukifanya kuwa miongoni mwa kampuni zinazolipa kodi kubwa nchini.
|