MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Michezo Villa Squad yaiduwaza Simba
BOOKMARK THIS PAGE
Villa Squad yaiduwaza Simba  Send to a friend
Sunday, 05 February 2012 09:53

Jessca Nangawe na Kalunde Jamal
VILLA Squad jana waliwaduwaza vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam baada ya kuinyuka bao 1-0 katika mechi ambayo Wekundu hao wa Msimbazi hawataisahau kwani pamoja na wapinzani wao hao kubaki nane tu uwanjani, walishindwa kukomboa bao hilo.

Shujaa wa ushindi huo wa tatu kwa Villa alikuwa mshambuliaji Nsa Job aliyefunga bao hilo pekee kwa shuti akimaliza pasi nzuri ya Cosmas Lewis katika dakika ya 40.

Siku ilikuwa mbaya zaidi kwa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, pale mshambuliaji wao wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi aliposhindwa kutumbukiza wavuni kiki ya penalti ya utata ambayo ingeweza kuipa Simba uongozi.

Penalti hiyo ilitolewa baada kiungo Mwinyi Kazimoto kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mlinzi wa Villa, Mohamed Suleiman na Okwi kushindwa kufunga baada ya kipa wa Villa Daud Mwasongwe kuicheza.

Kilikuwa kipigo cha pili kwa vinara hao msimu huu, huku kocha wao Milovan Cirkovin akitoka uwanjani bila kuamini macho yake zaidi la kuwaangushia mzigo wa lawama wachezaji wake.

Mara baada ya baada ya mchezo huo kulizuka fujo miongoni mwa mashabiki na kupelekea polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kurejesha amani.

Cirkovic alikiriki kipigo na kusema wachezaji wake walicheza chini ya kiwango, huku pia akilalamika muda kiduchu wa nyongeza ulitolewana mwamuzi baada ya kumalizika dakika 90.

Cirkovic alisema mwamuzi, Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam ambaye alionekana wazi kushindwa kulimudu pambano hilo, hakuwa sahihi kuongeza muda mdogo kwa vile mchezo ulisimama mara kwa mara.

Simba ilifanya mashambulizi mengi langoni mwa Villa huku ikikosa mabao katika dakika za 23 (Uhuru Seleman) na Patrick Mafisango katika dakika ya 38 aliposhindwa kumalizia krosi ya Uhuru Seleman.

Villa nao wangeweza kubadilisha matokeo kama wangetumia vizuri nafasi nzuri walizopata kipindi cha kwanza kupitia kwa Cosmas Lewis na Malika Ndaule waliotengenezewa nafasi na Nsa Job.

Mambo yalikuwa mabaya kwa Villa katika dakika ya 64 baada ya Ciprian Lukindo kuonyesha kadi ya pili ya njano kwa kosa la kumpiga beki wa Simba Kelvin Yondan, huku pia Cosmas Lewis akionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kosa la kujiangusha.

Kufuatia kubaki wachache uwanjani, timu ya Villa ilicheza mchezo wa kujiamia kwa muda wote uliobaki, huku washambuliaji wa Simba wakikosa mbinu za kuipenya ngome hiyo.

Kocha wa Villa, Habib Kondo alisema ameridhishwa na matokeo, lakini akalalamika kadi walizopewa wachezaji wake wawili na kusema ziliwavunja moyo wa kufanya mashambulizi na hivyo kulazimika kulinda lango.
"Muhimu kwetu ni pointi tatu ambazo tumeshazipata," alisema Kondo ambaye kwa ushindi huo timu yake imefikisha pointi 13 na kusogea nafasi moja juu.

Pamoja na kupoteza mchezo huo, Simba bado inaendelea kung'ang'ania kileleni mwa msimamo ikifuatiwa na Yanga katika nafasi ya pili na Azam inayoshuka dimbani leo katika nafasi ya tatu.

Katika matokeo mengine, Rashid Mandawa wa Coastal Union alifunga bao pekee katika mechi dhidi ya Moro United kwenye Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji na kuwafikisha Wagosi hao pointi 17.

Aidha, maafande wa Ruvu Shooting na Polisi Dodoma walimaliza dakika 90 kwa sare ya bila kufungana katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner