MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Michezo Wachezaji Stars wajipa matumaini kushinda Algeria
BOOKMARK THIS PAGE
Wachezaji Stars wajipa matumaini kushinda Algeria  Send to a friend
Saturday, 28 August 2010 19:57



Jessca Nangawe

SIKU moja kabla ya timu ya Tanzania, Taifa Stars' kuondoka kwenda Algeria kurusha karata  ya kwanza ya kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2012, wachezaji walipita katika mchujo uliofanywa na kocha Jan Poulsem wameahidi kwenda kupambana ili kuiletea taifa ushindi na hatimaye kusonga mbele katika michuano hiyo.

Poulsen ambaye juzi aliwatema nyota saba wakiwemo Jerryson Tegete wa Yanga na Kelvin Yondani wa Simba waliokuwamo katika kikosi chake kwa madai ya kiufundi  na wengine kuwa majeruhi, aliwataka wachezaji hao kujituma na kuupa kipaumbele zaidi mchezo huo ambao utachezwa Septemba 3 mjini Algiers.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili, wachezaji hao wamezungumzia mchezo huo kwa hisia tofauti huku wengi wao wakieleza kuwa utakuwa mgumu na wenye ushindani kwani wanakutana na timu ngumu ambayo ipo mbele katika viwango vya mchezo huo tofauti na wao.

Wameeleza kuwa wanahitaji kuonyesha uwezo zaidi katika mchezo huo pamoja na ushirikiano baina yao ili waweze kufanya vizuri huku kila mmoja akionyesha ari ya kutaka ushindi.

"Lengo letu kama wengi tunavyotarajia ni kuiletea heshima Tanzania  kwa kutoka na matokeo ya kuridhisha kama inavyofahamika michuano hii ni migumu na yenye ushindani mkubwa, hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kutimiza kile tulichokusudia

"Kimsingi, tumejiandaa vyema kila mmoja wetu anatamani ushindi hivyo tunawaahidi Watanzania na mashabiki wote tutahakikisha tunaifunga Algeria katika mchezo huu ili tusonge mbele,"alisema nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa.

Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi alisema ushindi kwao ni lazima, lakini wana kazi kubwa ya kuiondoa Algeria kutokana na historia yake hivyo kuwaomba Watanzania wawaombee dua katika hilo ili wafanikiwe katika michuano hiyo.

Mshambuliaji mwingine, Mrisho Ngassa aliwataka wenzake kuweka mbele uzalendo na kushirikiana zaidi kutokana na ugumu wa mchezo ambao utachezwa Ijumaa usiku wakitambua kwamba wanakwenda kucheza  kama mabalozi, hivyo waupe kipaumbele na Watanzania wawaunge mkono.

Beki Stephano Mwasika alisema: "Jitihada, bidii na uelewano  ndivyo vitaivusha Tanzania."

Stars inaondoka keshokutwa, Jumanne kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar Airways kwenda Algiers, Algeria ikiwa na wachezaji 20 na itatupa karata yake ya kwanza Ijumaa Septemba 3.


Wakati huohuo, Doris anaripoti kuwa wadau wa soka wamesifu uamuzi wa kocha Poulsen kuwaacha wachezaji saba kutoka kikosi chake ambacho kitasafiri kwenda Algeria Jumanne.

Wachezaji  walioachwa ni Abdulhalim Humoud , Kelvin Yondani, Juma Kaseja, Juma Jabu na Uhuru Seleman wa Simba  na Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete kutoka Yanga.

Baadhi yao waliiambia Mwananchi Jumapili kuwa  Kaseja bado anasumbuliwa na maumivu ya mkono baada ya kuteguka mkono alioumia kwenye mazoezi  huku Chuji ambaye aliyekuwa akisumbuliwa na malaria  alielezwa na kocha kuwa amepona lakini hana mazoezi ya kutosha.

Wamewataka wachezaji waliobaki kuonyesha msimamo na kufanya kazi waliyotumwa kwa kutoridhika na viwango vyao badala yake waongeze juhudi zaidi na ndiyo itakuwa njia pekee kwa wengine waliobaki wajitume.

''Ni vizuri kwa sababu kocha ameonyesha kujiamini na nini anataka kiwepo katika kikosi hicho kama ameacha ni vyema inaonyesha ni wazi kwamba wameshindwa kwenda na kasi yake,''alisema John Maringo ambaye ni mdau wa soka.

''Hii itakuwa fundisho na kuacha lawama kwa sababu timu itakapofungwa watu wanamwangalia kocha kuwa hafai hii itawafanya wachezaji wengine waongeze bidii zaidi,''alisema Azim Shikanda.

Kikosi kamili cha Stars:

Makipa :  Shabani Kado (Mtibwa) na Jackson Chove (Azam ).

Mabeki : Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Stephano Mwasika (Yanga), Salum Kanoni (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka), Aggrey Morris nad Erasto Nyoni (Azam).

Viungo : Jabir Aziz, Selemani Kassim (Azam), Shaaban Nditi (Mtibwa), Nurdin Bakari, Abdi Kassim (Yanga ), Henry Joseph (Kongsving).

Washambuliaji: Danny Mrwanda (DT Long), Nizar Khalfan (Whitecaps), John Bocco, Mrisho Ngasa (Azam), Mussa Hassan Mgosi (Simba).

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?