|
Na Angetile Osiah NILIPATWA na mshangao wakati niliposoma mintaarafu ya maisha ya waziri wetu wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Bi Sophia Simba katika mahojiano yake na gazeti la kila wiki la Raia Mwema. Nilishangaa kwa kuwa sikutegemea kiongozi kama yeye katima karne hii ambayo uongo ndiyo sera, kuwa mkweli kiasi hicho cha kuwa tayari kuanika kila kitu ambacho alidhani watu wanakitafsiri tofauti. Navyoelewa ni kwamba wengi wangetumia fursa hiyo ya kuweka mambo sawa kwa kuzungumza siasa za ajabu na pengine hata kusingizia kuwa yote mabaya yanayozungumzwa dhidi yake ni uongo na uzushi. Lakini Simba hakuwa hivyo. Aliamua kuweka hadharani yote ambayo yanazungumzwa vibaya dhidi yake na mengine ambayo yanakaribiana na ukweli, lakini yakizungumzwa kwa njia ambazo zinamchafua mtu.
Isingekuwa rahisi kwa kiongozi kama Simba kueleza bayana kwamba Kitwana Kondo alikuwa "boyfriend" wake, maana hiyo ingetafsiriwa katika picha pana zaidi kwamba kumbe huyo mama alikuwa akisababisha mwanamke mwenzake kukosa usingizi kwa ajili yake! Lakini pia aliweka bayana kitu ambacho kinaweza kuwa tafsiri mpya ya "boyfriend" maana alikiri bayana kuwa alizaa na Kitwana Kondo mtoto mmoja.
Labda tuachane na mwandani wake. Maana unaweza kujikuta unaingia kwenye kundi ambalo linamuelewa au kumuelezea Simba kwa maneno mabaya. Labda nizungumzie hili la Husna Mwilima, katibu mteule wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), ambaye hakumudu kufikisha hata mwaka mmoja kutokana na wale wanaotaka kumchafua Waziri Simba kusema "eti" alikuwa na tofauti naye.
Mama Simba akaweka bayana kwamba "akha" hakuwa na tofauti naye kwa sababu yeye ndiye aliyependekeza jina lake na kulipeleka kwenye Baraza la UWT ambalo lilimpitisha kuwa katibu mkuu. Naona kuwa pengine watu wanaona kuwa Waziri Simba, ambaye ni mwenyekiti wa moja huo, alikuwa na tofauti Husna ni kitendo chake cha kukiri kuwa alifanya makosa kumpendekeza mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Tandahimba. Katika makala hiyo, Waziri Simba anaeleza bayana kuwa alifanya makosa; kwanza kumteua Husna kwa kazi hiyo ambayo ilikuwa kubwa kwake kutokana na kiwango chake cha elimu; na pili kumteua Bi Husna bila ya kumshirikisha mtu mwingine yeyote.
Anaeleza mama huyo kuwa kazi ya katibu mkuu wa UWT ni kubwa sana kulinganisha na kiwango cha elimu cha Husna hivyo asingeweza kuimudu kazi hiyo ambayo iliwahi kufanywa na kina mama wengine wenye uwezo. Nilimsifu kwamba, aliweza kuweka kile anachoamini kuwa ni ukweli ili kuwaweka sawa wale wanaoona kuwa alikuwa na tofauti na mama huyo. Mtu anayehusika na utawala bora anapoona kuwa mtu fulani hamudu nafasi fulani, basi anakuwa ameangalia mambo mengi kiasi kwamba mtu mwingine ambaye utatataka umtumie huyo aliyetemwa utalazimika kufanya kazi ya ziada, hasa inapokuwa suala la kushika ofisi ya umma. UWT ni ya wanachama wa umoja huo tu ambao wanaweza kukubaliana hata mambo ambayo aliye nje anayaona kuwa hayafai. Kwa hiyo kiongozi kwenye jumuiya kama hiyo anatakiwa kuwa makini na utashi wa watu hao waliouweka kwenye katiba na sheria zao ili mambo yaende sawa.
Kwa hiyo ni rahisi zaidi kuongoza kwenye jumuiya kama hiyo kwa sababu utashi wao uko bayana na hauna utata. Lakini kuongoza wilaya ni kitu kigumu sana hasa ikizingatiwa kuwa utashi wa jamii iliyo kwenye wilaya hiyo hutofautiana sana. Mahitaji ya wilaya ni makubwa zaidi ya mahitaji ya jumuiya moja, hata iwe ya kitaifa. Matazamio ya wakazi wa wilaya ni makubwa zaidi ya yale ya wanachama wa jumuiya. Na utendaji wa kiongozi wa wilaya ni mgumu kuliko ule wa jumuiya moja.
Sijui Simba aliona ukosefu wa elimu ya kutosha ya Husna ungeathiri zaidi sehemu zaidi kwenye utendaji wake ndani ya UWT, lakini pengine udhaifu aliouona Waziri Simba ndio nguvu yake ya kuongoza wilaya. Watu tunatofautiana kimtazamo! Pengine alikuwa sahihi yule aliyesema "when one door is closed, many more are opened". Ndio maana Sophia Simba alipomuona Husna kuwa hana elimu ya kutosha kuwa mtendaji mkuu wa UWT, Rais Kikwete akagundua kuwa ana elimu ya kutosha kuwa mkuu wa wilaya! Simba alifunga mlango mmoja, mingine kibao ikafunguka!
|
Comments
UDC mbona huko nyuma alikuwa ni DC na alimudu, acheni Mama wa watu apige mziko si vizuri kuendelea kumsakama.
Mimi nashangaa kuona kuwa huyu Husna ndiyo kawa pekee, asiye soma na kapewa madaraka
Tuanzie huko nyuma marehemu diria alikuwa ni form six leaver alikuwa na madaraka ya kila aina
Wengine walikuwa wabunge wa kuteuliwa , mdogo wetu amina chifupi na form six yake ya tambaza sasa wewe aliye kuambia tanzania ni husna mwilima pekee sijui ni nani?
Sisi watoto wa mjini tunamjua kitwana Kondo, huyu akikushika mkono ukwami, sasa mama na uwaziri wko tuambie umesoma wapi mwenzetu?