MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Uchambuzi & Maoni Bwagamoyo:Madai ya Mwakyembe kupewa sumu yasipuuzwe
BOOKMARK THIS PAGE
Bwagamoyo:Madai ya Mwakyembe kupewa sumu yasipuuzwe  Send to a friend
Saturday, 14 January 2012 19:30


L. W. Nzela
KWAMBA inawezekana Mbunge wa Tanzania kuwekewa sumu na vyombo vya uchunguzi kukaa kimya au kuonekana kupuuzia inatisha. Kwamba, inawezekana Naibu Waziri wa Ujenzi kutegewa sumu mahali fulani ambayo ilikuwa na lengo la kummaliza inatisha.
Kwamba, inawezekana mtu huyo kujaribu kutegeshewa ajali mbaya ya gari na kunusurika nalo linatisha. Kwamba, mtu huyo huyo ambaye inadaiwa kutegeshewa sumu na kunusurika na gari aliwahi kulalamika hadharani kuwa kuna kikundi kilichotumwa kumuua na bado vyombo vya usalama viko kimya vikifanya “uchunguzi” usiokwisha.
Kwamba waziri huyo aliyedai kukoswakoswa na ajali ya gari, kuwindwa na mahasimu wake na ambaye inadaiwa amelishwa sumu ambayo ilikuwa immalize, ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge ambayo uchunguzi wake ulifichua kashfa ya zabuni ya kampuni ya Richmond na ufisadi mkubwa serikali inatisha zaidi.
Taarifa za Dk Harrison Mwakyembe kuugua  ghafla za zilitukuta wengi kwa ghafla. Lakini kilichoshtua zaidi siyo kwamba anaugua bali ugonjwa wenyewe wa ngozi ambao haukuweza kueleweka mara moja. Taarifa za mwanzo kabisa zilitoka mara baada ya taarifa kutoka ni kuwa Dk Mwakyembe alikuwa amepewa sumu ambayo ilishambulia ngozi yake. Hadi hivi sasa hayajatolewa maelezo yoyote ya kukanusha kuwa kilichomsibu Mwakyembe ambaye ilibidi akimbizwe India kwa matibabu siyo sumu.
Tangu amepelekwa kwenye matibabu hadi amerudi serikali wala vyombo vya usalama havijaweza kukanusha kuwa Mwakyembe hakupewa sumu. Ninaandika makala hii nikiamini kuwa ni kweli Mwakyembe alipewa sumu ambayo ilitaka kummaliza na wale waliomtegeshea sumu hiyo hadi hivi sasa bado wako huru na hakuna dalili yoyote kuwa wanaweza kukutwa na mkono mrefu wa haki.  Kwamba, inawezekana katika Tanzania wauaji wa kisiasa (assassins) wanaweza kujipenyeza na kumsogelea kwa karibu kiongozi wa umma na kumdhuru bila kugunduliwa inatisha zaidi kwa mtu yeyote ambaye anafuatilia siasa za nchi yetu.
Kifo cha Balali
Ili kuweza kufikiria hili labda nirudishe nyuma kidogo juu ya kile kinachotajwa kuwa ni kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Bw. Daudi Ballali miaka michache iliyopita. Baada ya sakata la EPA kuibuliwa na kina Dk Williboad Slaa na kuvaliwa njuga hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kuwajibishwa kwa wizi ule mkubwa kama Gavana wa Benki Kuu. Katika mazingira ya kushtua tuliambiwa tu kuwa Dk Ballali aliondoka Dodoma kwa ndege na kurudi Dar es Salaam na tunakumbuka vizuri aliporudi jijini alivyolaumu baadhi ya wafanyabiashara kuwa ndio walikuwa wanamlia njama.
Hatujui aliondoka lini nchini na kwa namna gani tunachojua ni kuwa siku chache baadaye tuliambiwa aliondoka nchini baada ya kuumwa tumbo na kukimbizwa “Marekani” kwa matibabu. Sote tulijua kuwa asingeweza kurudi nchini na kuwa shahidi muhimu dhidi ya wahalifu wa EPA. Tunaambiwa aliugua vibaya sana huko alikokuwa hadi mauti “yalipomfika”.  Tukiamini kuwa ni kweli Ballali alikufa tulivyoambiwa hatuna budi kujiuliza kama na yeye alikutwa na mkono mrefu wa wauaji wa kisiasa,  watu ambao wako tayari kumsogelea mtu yeyote na kumfanyizia hasa kama mtu yule anatishia maslahi yao. Kwamba, Gavana Ballali alikufa katika mazingira ya kutatanisha yenye kila alama ya kuuawa kwa sumu nalo latisha!
Kifo cha Amina Chifupa
Mojawapo ya vifo vya ajabu sana na ambavyo navyo vina alama za wauaji hawa wa kisiasa ni kifo cha Mbunge kijana na maarufu sana Amina Chifupa. Wengi tunakumbuka jinsi nyota ya binti yule ilivyokuwa inang’ara kila kukicha. Hata hivyo alijikuta kwenye matatizo siku ile alipoapa hadharani kuwa kesho yake angeenda mbele ya vyombo vya habari na kuwataja majina ya watu ambao wanahusika na madawa ya kulevya na hata baadhi ya watu ambao alihusiana nao kwa karibu (wengine waliamini kuwa waliowahi kuwa wapenzi wake).
Amina hakupewa nafasi ya kutokea hadharani tena baada ya familia yake “kumzuia”. Wengi wetu tulipiga kelele sana ili apewe uhuru wake lakini “wale wenye nguvu” walihakikisha Amina hatokei tena hadharani na kwa kweli kwa kadiri siku zilivyopita wingu la ukimya liligeuka wingu jeusi la mauti likimzunguka na baadhi yetu tulitambua wakati ule kuwa Amina asingeweza kurudi na kuzungumza akiwa hai. Na ni kweli mara ya mwisho taarifa ambazo watu walikuja kuzipata ni kuwa Amina amekimbizwa Lugalo ambako mauti yalimkuta. Wale waliotembelea na waliomuona siku chache kabla ya mauti wanasimulia jinsi alivyoonekana kumalizwa na kitu ambacho kilikuwa nje ya magonjwa ya kawaida.
Kifo cha Salome Mbatia
Kifo kingine kilichotokea katika mazingira ya utata mkubwa ni cha aliyewahi kuwa Mhazina wa CCM Bi. Salome Mbatia. Naweza kujaribu kuelezea hili lakini wanaokumbuka wanakumbuka jinsi kilivyotokea na kufanana kwa namna ya ajabu na kifo cha Sokoine miaka mingi iliyopita au cha Wangwe! Naogopa hata kuanza kuulizia  kuwa dereva aliyehusika yuko wapi!
Mifano hiyo michache inatufanya tuamini kabisa kuwa ni kweli kipo kikundi kinachofanya kazi za kutekeleza mauaji ya kisiasa nchini na ni kikundi ambacho kina nguvu za kuweza kumfikia yeyote, mahali popote, na wakati wowote. Kikundi hiki kimepewa mafunzo ya kina (taarifa nyingine za zamani zinadokeza kuwa watu wake wamepata mafunzo Afrika ya Kusini na Israeli). Ni kikundi ambacho bila ya shaka kina uwezo mkubwa wa kifedha, teknolojia na nafasi. Uwepo wa kikundi hiki ni vigumu kukanushwa hasa baada ya tukio la Dk Mwakyembe kuugua.
Tunaweza kuamini mambo machache juu ya kikundi hicho:
•    Kiko karibu sana na wanasiasa. Tunaweza kuona kuwa kikundi hicho kinatumia mwamvuli wa kuwa karibu na wanasiasa na urafiki wa karibu ili kuweza kutekeleza majukumu yake. Vinginevyo, inawezekana vipi kumsogelea Ballali au Mwakyembe bila kushukiwa? Haiwezekani kuwa ni watu wasiojulikana; ni watu wa karibu na yawezekana ni watu wenye nafasi za kisiasa vilevile.
•    Kinapewa amri kutoka juu sana. Mojawapo ya mambo yananitisha kuhusu kundi hili ni uwezekano kuwa kundi hili linaamrishwa na watu wajuu sana kwani kuweza kuwafikia watu ambao wanatakiwa kuwa na ulinzi wa hali ya juu si jambo dogo. Yeyote anayewaamrisha hawa watu ni lazima yeye mwenyewe awe na uhakika wa kuwa watamtii na wao kuwa na uhakika kuwa hawawezi kushtakiwa. Nani anawaamuru au ni mkuu wa genge hili la wahalifu?
•    Mpaka hivi sasa hakuna chombo nchini ambacho kina uwezo wa kuingilia mtandao huu na kuwashughulikia.  Mtandao huu hauwezi kuvunjwa kwani kila dalili zinaonesha kuwa wahusika wake wametanda kwenye vyombo mbalimbali kiasi kwamba ni vigumu polisi kuweza kuchunguza au Usalama wa taifa au chombo kingine chochote.
Ni kutokana na mambo hayo matatu naamini kuwa tusipoangalia tutaendelea kushuhudia vifo vya wanasiasa katika mazingira ya utata huku tukiambiwa tukubali tu kuwa ni “mapenzi ya Mungu” kumbe ni “mapenzi ya mafisadi” yakitimizwa. Kwa vile mauaji ya kutumia risasi yatashtua zaidi nchi yetu naamini  genge  hili linaendelea kutumia mauaji ya kutumia ajali na sumu ili kunyamazisha wanasiasa na watu ambao wanatishia maslahi yao. Nani atachunguza kama wote wako ‘compromised’?
Mwakyembe inawezekana amenusurika lakini sidhani kama yuko salama. Na kwa vile serikali imeamua kukaa kimya na kuonesha kushindwa kufuatilia watu waliojaribu kumdhuru ni wito wangu kwa kila mwanasiasa na mwanaharakati kuwa makini; siyo kuwa makini na watu ambao anaamini ni maadui wake bali zaidi kuwa makini na watu ambao anaamini kuwa ni marafiki zake. Kwani kundi hili la wauaji wa kisiasa haliji kama adui, bali kama rafiki.
Unaposimama dhidi ya ufisadi, mfumo mbovu wa utawala na utetezi wa raslimali zetu ujue kuwa wapo wengine ambao wamekuwekea alama ya kukuondoa au kukunyamazisha milele.
 Fikiria!
Niandikie: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner