MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Uchambuzi & Maoni Kutoka London:Mtutusiko wa 2012 una kiini katika umasikini
BOOKMARK THIS PAGE
Kutoka London:Mtutusiko wa 2012 una kiini katika umasikini  Send to a friend
Saturday, 14 January 2012 19:48

Na Freddy Macha

NILIKUWA nikiongea na rafiki yangu wa Nigeria akasema kila kukicha Wazungu wanashuka Afrika. “Uchumi wa Ulaya mbaya sana sasa hivi,” ali jamaa huyo huku akicheka; ”si ajabu wanakimbilia Afrika.”

 Si Wazungu tu, nikamwambia. Wachina wanalikamua bara kama maziwa ng’ombe. Afrika ni tajiri wa madini, mimea, mafuta na wanyama pori. Tovuti maarufu la habari Wikipedia linasema Afrika ina neema kubwa kiasi ambacho pamoja na kuibiwa na wageni  na mafisadi wachache, bado hata nusu ya mali asili yake haijagunduliwa au kufaidika sawasawa.

 Karibuni mafuta yanaendelea kuvumbuliwa na tayari Wachina wanamiliki asilimia 40 ya mali hiyo ya WaSudan mathalan. Wakati huo huo Sudan ni maskini sana. Vita vya wenyewe kwa wenyewe  vilipokua vimechachamaa miaka kumi iliyopita ripoti ya Umoja wa Mataifa (HDR) ilieleza  asilimia 25 ya Wasudan  hawafikishi miaka 40.

Sasa hivi tunapoambiwa hali ni mbaya kiuchumi duniani Jumatatu kampuni maarufu ya magari, Rolls Royce, ilitangaza ongezeko la faida kwa asilimia 14 mwaka jana. Wanunuzi  wengi wanatoka Marekani na China na wanamudu kununua gari moja kuanzia  shilingi 480,000,000 kuendelea.

 Rolls Royce imeeleza haijawahi kupata faida kiasi hiki tangu ilipoanzishwa miaka 107 iliyopita. Eti kwa vile linazuka tabaka jipya la wenye pesa hasa China.

Takwimu za Benki kuu ya Dunia ( mtoa mikopo mkubwa nchi zinazoendelea) zinakiri wanadamu bilioni moja na robo ni maskini wanaoishi kwa mlo mmoja tu kwa siku. Ingawa ulimwengu wetu una wakazi milioni saba, asilimia 80 hutumia pesa wanayoipata kwa chakula, bas. Hii ina maana masuala muhimu kama elimu, afya na makazi hayapatikani. Wengi wanasukuma tu siku. Inanikumbusha msemo wa Kiswahili  Bora Twende.

Ukitathmini saikolojia yetu Watanzania utagundua baadhi yetu tumo tumo  tu. Hatujali kuvaa mikanda katika magari na mabasi (jambo lililodhihirishwa na uchunguzi wa kitaalam duniani kwamba hukinga na kupunguza madhara ya ajali); hatujisomei vitabu au kujiendeleza, hatuangalii afya zetu na unene unazidi kutuletea maradhi kama kisukari na presha ya moyo(hata vijana chini ya miaka 30 wanakumbwa leo).
Wiki iliyopita tulitazama neno “tutusa” lenye maana ya kudunda moyo  au kutafuta kitu gizani. Tukaona namna mtitiso ulivyoenea duniani kuwa mwaka 2012 ni wa mwisho. Kwamba watabiri wa woga (kama Nancy Lieder, 1995) aliyeanzisha tovuti iitwayo Zeta Talk iliyosema Mei 2003 ungekuwa mwisho  na  21 Desemba 2012  ulimwengu wetu utaangamizwa na sayari ya Nibiru Planet X.
Ukweli vilio kwamba uhai utakwisha vimetoka mbali sana. Kati ya mwaka 1348 hadi 1350 asilimia 60 ya Wazungu wa bara Ulaya walitokomezwa na tauni.

Chimbuko la “kifo cheusi” (Black death) lilianzia miaka 30 awali.
 Mwaka 1315 dunia ilikumbwa na hali mbaya kimazingira ambapo mavuno na uhaba wa vyakula  vilizua njaa, ujambazi, watu “kula watu” wenzao na maradhi. Hatimaye ndipo mapanya yakaenea na  msemo wa mwisho wa dunia ukakita; wanajimu wakasema Mungu kakasirika na kadhalika.

Wanadamu wanapokosa mambo ya msingi (chakula, malazi na afya) hutafuta majawabu katika kiza na tutusa. Ila unapochunguza, umaskini ndiyo chanzo cha matatizo makubwa ya vita na hasira za wanadamu.

Mifano iko mingi
Tatizo la vita vya wenyewe kwa wenyewe linaloendelea sasa hivi Somalia na kuwaathiri majirani zetu Kenya limeanzia wapi? Asili mia 95 ya Wasomali wanaishi vijijini. Kati ya wanakijiji hawa walezi wa watoto na familia ni wanawake wasiosoma na ambao hawana haki yeyote katika jamii. Takwimu za Umoja wa Mataifa zimeeleza kiasi cha wanawake 45 wa Kisomali hufa kila siku kutokana na athari za ukeketaji au tohara za akina mama. Vifo hivyo huja nyakati za uzazi unaombatana na damu na maumivu makali.
 
Mbali na mila na desturi kama hizi  hali ya hewa imeisambaratisha Somalia. Mwaka 2006 mafuriko makali yalipokumba uwanda wa kati  wa nchi yaliendeleza vurugu zilizoanza toka kuangushwa kwa Rais Mohammed Siad Barre, 1991.
Labda Somalia ingekuwa na utajiri wa madini mambo yangekuwa afadhali lakini asilimia 60 hutegemea ufugaji.  Tatizo hili limezidishwa na ulaji mirungi unaowafanya wanaume kuranda randa ovyo, kutojali mifugo, kazi au  familia. Matokeo wananchi 12.4 wameathirika na njaa; milioni 1.5 wako  ukimbizini ughaibuni.

Nigeria hivyohivyo.
Kinyume cha Somalia, Nigeria ni moja wa matajiri  Afrika kutokana na mafuta. Mafuta hayo toka majimbo ya kusini (Niger Delta) yamewafanya wananchi wengi  walalamike kwamba  kipato cha mali hii asilia hakiwafaidi. Mwaka 1995 mwandishi na mtangazaji maarufu wa TV, Ken Saro Wiwa, alinyongwa na serikali  kutokana na jitihada zake kupinga uporaji na uharibifu wa mazingira ya watu wa kabila la Ogoni.  Ingawa Nigeria ilifukuzwa ndani ya Jumuiya ya Madola kwa miaka mitatu, hali iko vile vile. Asilimia 65 ya Wanigeria ni maskini sana.
Tatizo hili limechipusha vyama vyenye itikadi za Kiislamu hasa  majimbo ya kaskazini . Kabila la Wahausa  na Wafulani  (asilimia 30 ya Wanigeria) lina Waislamu zaidi ya Wakristo ambapo kusini wapo Waislamu wachache. Ingawa Uislamu umekuwepo Nigeria toka karne ya 11, miaka 30 iliyopita umechipusha viongozi waliotumia dini hiyo kuleta uhasama kupitia makundi matatu.

 Boko Haram (“Elimu ya Kizungu ni Dhambi” kwa Kihausa) ilisababisha mauaji ya wananchi 450 mwaka jana. Boko Haram inadaiwa kuwasiliana na magaidi wa Kisomalia. Maitatsine (Kihausa “Yule anayelaani”)  iliasisiwa na  Mohammed Marwa (aliyefariki 1980) ikipinga baadhi ya nguzo za Kiislamu kama Sunnah na Hadith. Marwa alishutumu “mambo ya Wazungu” mfano redio, baiskeli, magari na pesa. Mwaka 2004 “Maitatsine” ilisababisha vifo 1,000  mjini Yola.
 
 Mwaka juzi Darul Islam (“Nchi ya Kiislamu) inayolilia Nigeria iwe ya Waislamu watupu ilisababisha ghasia zilizoua 700. Makundi haya matatu yanalilia Sharia iwe kanuni ya taifa hilo.

 Ugaidi husababishwa na umaskini; ambao hutokana na siasa na uongozi mbaya. Si ajabu karibuni baadhi ya watabiri wa woga kudai  mwisho wa dunia ungekuwa 1994, 1999, 2000, Septemba 2001, Mei 2003, 11 Novemba 2011 na  sasa 21 Desemba 2012.  Msingi hapa si kuogopa kwisha dunia bali kusuluhisha matatizo ya wale wanaokula mlo mmoja tu kwa siku.

Barua pepe: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
Tovuti: www.freddymacha.com

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner