
| Bwagamoyo:Tusipohitimisha madaktari 2,000 kwa | Send to a friend |
| Saturday, 21 January 2012 18:27 |
|
mwaka tutakuwa na matatizo makubwa L. W. Nzela MOJAWAPO ya magazeti ya serikali limeripoti kuwa Serikali ya Tanzania imeingia mkataba na Serikali ya Misri ambapo taifa hilo la Kiarabu litatoa msaada wa madaktari kwa Tanzania. Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuingia mikataba ya aina hiyo na Wamisri hawatokuwa madaktari wa kwanza kuja kufanya kazi Tanzania. Tulikuwa na madaktari kutoka Cuba, China na nchi nyingine na wengi wao wakiwa ni watalaamu ambao walikuja kufanya kazi nchini chini ya mashirika na makampuni mbalimbali. Sasa, kuna watu katika serikali yetu ambao uwezo wao wa kufikiria unaanzia na kuishia kwenye misaada. Ndugu zetu hawa wakiambiwa wajenge shule swali la kwanza ni “msaada utatoka wapi” na wakiambiwa tuongeze walimu swali linaloanzia ni “msaada wa kuwasomesha utatoka wapi”. Watawala hawa walioshindwa wakiambiwa jinsi gani tuongeze madaktari swali linalofuatia ni “nchi gani gani itatusaidia madaktari”. Ndugu zangu, ninachoandika hapa ni jaribio la kuonesha kuwa tuna uwezo wa ndani ya kupata madaktari wetu tena wataalamu wa hali ya juu bila kuomba msaada kutoka nchi nyingine. Tunapofikia kama taifa kuachilia afya zetu mikononi mwa mikataba na nchi za nje tunahatarisha afya zetu na za watoto wetu na kukihukumu kizazi kijacho katika hali ya mashaka ya kudumu. Ndugu zangu, hakuna nchi ambayo inaweza kutupa misaada ya kila kitu. Ndio maana Uingereza hivi karibuni imeonekana kushangazwa na jinsi gani Tanzania taifa ambalo liko katika hali ya utulivu mkubwa na amani (kulinganisha na mataifa mengi ya Kiafrika) linaongoza kwa kuombaomba bara la Afrika kupita hata nchi kama Congo, Somalia, Angola, n.k. Kwamba Tanzania iko nyuma ya Iraq na Afghanistan kwa kupata misaada ni jambo la kutisha. Lakini kwamba tunatafuta hata misaada ya madaktari tena tukitia misaada kwa furaha linatisha zaidi. Nina mapendekezo kadhaa ya jinsi ya kubadilisha kwa haraka hali hii ya upungufu mkubwa wa madaktari. • Madaktari waondolewe kwenye kazi za utendaji serikalini Hili ni pendekezo rahisi kulifanyia kazi. Sijafanikiwa kupata idadi kamili ya madaktari wanaofanya kazi wizarani kama watendaji katika ajira ambazo zingeweza kufanywa na watu wasio madaktari. Hata hivyo, ninajua kwa uhakika kuwa wizarani na mikoani wapo madaktari ambao wanafanya kazi za kazi za utawala. Ninafahamu pia madaktari ambao wanafanya kazi za utafiti katika idara na taasisi mbalimbali. Hawa wote kwa namna moja wanaondoa nguvu kazi hii ya madaktari katika kuhudumia wagonjwa. Naamini kuwa ipo haja ya kuweza kutumia madaktari hawa katika kutibu wagonjwa na huduma nyingine za afya na hivyo kukabiliana na upungufu huu wa madaktari. Je, inawezekana kwa mfano katika kazi ambazo hazihusiani na utafiti wa kisayansi au tiba ajira hizo ziachiliwe kwa watu wengine wenye utaalamu wa mambo hayo au ambao wanaweza kufanya bila kulazimika kuwatumia madaktari? Je, inawezekana kuweka utaratibu ambapo daktari yoyote wa Kitanzania kutakiwa kutoa huduma fulani za afya kila mwaka ili kuendelea kuwa na leseni yake ya udaktari? Kwa mfano, daktari anapokuwa Mbunge je anatakiwa kutoa huduma bado au atakuwa anafanya kwa kujitolea tu? Hili linaweza kufikiriwa na tukaja na utaratibu mzuri wa kutumia madaktari hawa wa maofisini na kuwarudisha madaktari mahospitalini! • Madaktari wachukuliwe na kuhudumiwa kama wataalamu wa kigeni Ipo haja ya kubadilisha jinsi tunavyowaangalia madaktari kama mojawapo ya fani za kisomi tu na kuziweka kundi moja na mawakili na walimu. Ninaamini madaktari ni fani ya kipekee kwa kila kipimo; ni fani ambayo mtu anaamua kuhatarisha maisha yake kila siku kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine. Ni kwa sabab hiyo naamini tuangalie jinsi tutakavyoweza kubadilisha mfumo wa mishahara ya madaktari uwe kama wataalamu wa kigeni. Hili linaweza kufanywa kwa mfano kwa madaktari waliosomea nchini na kuamua kufanya kazi nchini na wamekuwa katika huduma kwa miaka kumi hivi. Huku madaktari wapya wakiingizwa katika mfumo mpya. Kwa mfano, daktari aliyesomea nchini na amekaa nchini kwa miaka kumi hivi mshahara wake usipungue • Serikali iwahamasishe madaktari Watanzania walio nje Hili linaweza kufanywa katika kuvutia madaktari warudi nchini katika kugeuza kile kinachoitwa “brain drain” ambapo madaktari waliosomeshwa kwa fedha za nchi maskini kama za kwetu wanaenda kusoma na kufanya kazi katika nchi zilizoendelea kama Uingereza, Australia, Canada na Marekani. Je, tunaweza kuwapa ofa gani hawa ili warudi kufanya kazi nchini? Naamini mojawapo ya ofa nzuri inahusiana na mishahara na mafao pamoja na nafuu katika kodi. Kwa mfano, tukisema madaktari hao wakiamua kuja kuanzisha kliniki au hospitali nchini watapata unafuu fulani wa kodi katika vifaa, mishahara n.k nina uhakika itawachochea baadhi yao kuja nchini. • Mikataba na mataifa yanayochukua madaktari wetu Mojawapo ya mambo ambayo yanawezekana kabisa kufanyika ni kuingia mikataba na mataifa ambayo yanachukua madaktari wetu hasa ambayo ratio yao ya madaktari kwa wagonjwa ni ndogo. Kwa mfano, kwanini Marekani, Ujerumani, Japan, Australia, Uingereza na Canada zikubali kuchukua daktari kutoka Tanzania? Lengo la mikataba hii siyo kuwakatalia Watanzania wasiende kufanya kazi huko, lakini kuweka utaratibu ambao utawafanya Watanzania hao kuweza kurudi nyumbani na kutoa huduma fulani. Kama tunaweza kudai “wachezaji wetu” wa mpira kwenye mataifa yenye soka la kulipwa kuja nyumbani kuchezea “timu ya taifa” nina uhakika ipo haja ya kufikiria jinsi gani madaktari wa Tanzania wanaweza kuitwa nyumbani kuchezea “timu ya taifa”. Pamoja na hilo inawezekana kuweka mikataba ambayo mataifa hayo yanapokubali kumsajili daktari aliyesomeshwa na Watanzania basi yaturudishie fedha zetu tulizotumia kumsomesha daktari huyo pamoja na adhabu ya wao kumchukua. Haiwezekani nchi maskini kama ya kwetu isomeshe wataalamu wa nchi za kigeni halafu turudi baadaye na kuomba misaada kutoka huko! Daktari aliyesomeshwa na Watanzania anapoamua kufanya kazi huko ughaibuni lazima hao wakubwa watulipe vinginevyo tuweke vikwazo ambavyo havitawawezesha madaktari hao kupata usajili huko au hata kutambuliwa! • Kuunda mtandao wa madaktari Ipo haja ya kuunda chombo ambacho kitakachowaunganisha madaktari wa Kitanzania duniani. Mtandao huu utasaidia katika kuwezesha mafunzo ya pamoja na kupeana utaalamu mbalimbali. Hili ni muhimu kwa kuwezesha wataalamu walioko katika nchi zilizoendelea sana kushirikishana ujuzi na watalaamu walioko nyumbani na hivyo kuwezesha kufanya kile kinachoitwa “kuhamisha ujuzi” (skill transfer) kutoka nchi zilioendelea na kuleta nchini. Je, hili linawezekana? Je madaktari walioko nyumbani wanaweza kujihisi wivu au kuonekana duni badala ya kuichangamkia nafasi kama hiyo? Ninachosema ndugu znagu ni kuwa tuna uwezo na sisi kufikiri nje ya misaada na tunaweza kabisa kuboresha sekta ya afya na kuongeza idadi ya madaktari nchini. Mimi naomba wakuu wetu hawa wakae siku moja na waulizane swali moja tu “tufanye nini kuboresha maisha ya madaktari wetu na vilevile kuongeza idadi ya madaktari nchini kwa muda mfupi bila misaada?” Waangalie watapata majibu gani. Wakiweza kuja na mambo kama kumi tu yanayowezekana basi tutakuwa kwenye mstari sahihi. Nani atatusaidia kuitisha mkutano wa aina hiyo na tutapata wapi wafadhili wa kugharimia semina au mkutano huo? Mweh! Niandikie:
This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
|

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














