
| Bwagamoyo:Nahofia wananchi wataposhindwa kuleta mabadiliko kidemokrasia | Send to a friend |
| Sunday, 29 January 2012 08:36 |
|
KUNA watu wanaamini kuwa demokrasia italetwa kwa hisani au kwa huruma ya watawala. Kwamba demokrasia yaweza kuletwa kwa kuwapigia watu magoti na kuwabembeleza. Kweli kabisa wapo watu wanaofikiri katika mioyo yao kuwa, demokrasia inaweza kujengwa bila msuguano kati ya watawala na watawaliwa, walionacho na wasionacho, wenye nguvu na wasio na nguvu. Hakuna nchi iliyowahi kujenga demokrasia kwa kurembuliana, kukonyezana na kukumbatiana. Demokrasia hujengwa kwa migongano. Demokrasia yaani utawala ambao wananchi wana nguvu ya mwisho ya kutawala, kwanza kabisa hujengwa kwa migongano. Migongano ipo ya aina tatu kubwa. Mgongano wa kimaslahi, wa kifikra na wa damu. Harakati za kupigania demokrasia zinapofikia mgongano wa damu maana yake ni kuwa njia nyingine zote za kupata demokrasia zinakuwa zimefikia isipokuwa mapambano na mgongano wa kulazimisha mabadiliko. Mgongano wa Kimaslahi Mahali popote panapotokea tofauti kubwa ya kimaisha kati ya wale walio nacho na ambao wanatamani kuwa nacho, au pale ambapo kuna matabaka ya wenye nguvu na madaraka (mabwana) na wale wasio nacho (watwana au watumwa), hutokea mgongano wa kimaslahi. Wale walio kwenye madaraka na wenye kunufaika na madaraka hayo hutaka kuendelea hali yao hiyo ya kuwa juu ya wengine na hivyo maslahi yao ni kuhakikisha kuwa wao wanadumu katika kufanikiwa kwa milele. Sasa mgongano wa kimaslahi mara nyingi huweza kutulizwa kwa kutoa maslahi fulani kwa walio chini. Yaani, wenye maslahi ya juu zaidi huamua kutoa maslahi kidogo ya waliochini ili kuwaridhisha. Ni kanuni ileile ambayo baba au mama aliyechoshwa na kelele za mtoto kulia, huamua kumpa doli achezee au peremende alambe. Wote wawili maslahi yao yanaridhishwa - baba ya kelele kuisha na mtoto ya kuoneshwa kupendwa na kujaliwa. Katika taifa hata hivyo maslahi yako ya madaraka na kutawala na maslahi ya huduma na mahitaji mbalimbali kutimizwa. Walio na madaraka wana lengo la kuendelea kuwa na madaraka hiyo ili kutimiza mahitaji yao mbalimbali hasa ya mali na hali ya juu ya maisha. Wale watu wa chini maslahi yao ni huduma mbalimbali na nafasi mbalimbali za kuweza kuishi katika hali ya unafuu. Hata hivyo hawa wa chini hawana madaraka au nguvu (wanajiona hawana) ya kujitimizia mahitaji yao. Hawa wa chini wanategemea uamuzi na utendaji wa wale wenye madaraka. Kwa maneno mengine wananchi hutegemea maamuzi na utendaji wa wale walio kwenye serikali ili mahitaji yao ya maji, barabara, afya bora, nafasi za ajira na mengineyo yatimizwe. Hata hivyo kwa vile mahali popote penye utawala wenye kutawaliwa ni wengi kuliko wale wenye kutawala basi ni vigumu sana kwa watawala kutimiza mahitaji yote ya watawaliwa kwa kiwango cha juu cha kuridhisha. Matokeo yake watawala hujaribu kuwaridhisha walio chini kwa kiwango cha chini ya kuwanyamazisha. Kwa mfano, wanaweza kujenga mashule yenye viwango cha chini sana au barabara ambazo zikimalizika zinaonekana nzuri, lakini miezi michache baadaye zinahitaji matengenezo makubwa. Mgongano huu wa maslahi una matokeo ya wazi kabisa katika maisha ya wananchi. Inafika wakati wananchi wanatambua kuwa matatizo yao mbalimbali (maslahi) yanahusiana moja kwa moja na watawala walioko madarakani na hivyo wananchi wanawaasi viongozi wao. Mgongano wa kifikra Jamii ambayo ina migongano ya kimaslahi ambayo inagusa maisha ya watu mbalimbali au makundi mbalimbali na maslahi yao husababisha watu waanze kufikiria. Watu huanza kuuliza maswali na kuhoji, kwa nini hali fulani ipo na kwa nini inaendelea kuwepo. Kwa kutumia njia mbalimbali, mijadala hufanyika katika ulimwengu wetu huu wa teknolojia ya kisasa mawazo na fikra za watu mbalimbali hupitishwa toka upande mmoja wa nchi au dunia kwenda upande mwingine. Mawazo na fikra hizi huchochea majibu kutoka kwa watawala. Sasa majibu ya watawala huweza kwa kiasi fulani kuwatuliza baadhi ya watu. Yaweza kuwa majibu ya kejeli, dharau au kupuuzia lakini kwa vile yanatolewa na wenye madaraka na nguvu basi baadhi ya watu huyapokea, huyakumbatia na kuyabusu kama zawadi ya mkungu wa ndizi toka Luanda. Pamoja na hayo wachache wataendelea kuuliza na kuhoji. Watahoji juu ya uwezo wa watawala, watahoji juu ya nia na mipango ya watawala na watahoji dhamira na maamuzi ya watendaji mbalimbali. Kwa kadiri watakavyoendelea kuhoji ndivyo majibu mepesi yatakavyozidi kukataliwa. Hapa ndipo pande mbili zenye fikra tofauti juu ya jambo lilelile huibuka na huanza kugongana. Mgongano huu wa kifikra huonekana zaidi katika siasa na akademia. Kuhusu akademia niliache kwa wakati huu kwa sababu sijashawishiwa kuwa mgongano huo upo kwenye akademia yetu Tanzania. Mgongano uliopo ni katika siasa ambapo maslahi ya kisiasa ya watu mbalimbali yanagongana. Kwa nchi yetu, sasa hivi bado ni mgongano wa nafasi za maslahi ya kisiasa. Wapo wenye kufurahia nafasi hizo sasa hivi na wale wenye kutamani kushikilia nafasi hizo au zaidi ya hizo. Kwa watu wasio na madaraka wanajikuta wamewekwa pande mbili za kisiasa nchini (yawezekana zipo na pande nyingine ndogondogo). Pande hizi za kisiasa hugawa wananchi katika misingi ya nani anamuunga nani mkono na nani atanufaika na nini nani akiingia madarakani. Katika nchi ambazo zimepiga hatua za kidemokrasia mgongano huu hugeuka na kuwa mgongano wa kiitikadi (ideological conflict). Mara nyingi mgongano wa kiitikadi ukiiva sana huweza kusababisha ule mgongano wa mwisho. Mgongano wa damu/Mgongano wa kimapinduzi. Sasa mgongano wa kimaslahi na mgongano wa kifikra au itikadi unaposhindwa kutatuliwa husababisha mgongano wa damu. Yaani, watu katika jamii fulani wanafikia mahali wanashindwa kutatua tofauti zao au kuridhishana katika matamanio yao na hivyo hulazimika kutotumia nguvu za “hoja” bali hoja za “nguvu”. Hapa ndipo watawala katika kujaribu kuzima kuenea kwa fikra wasizozitaka huanza kutumia nguvu, mauaji, watu kupotezwa, vifungo hutumika. Sasa tatizo mbinu hizo ni kuwa zaweza kufanikiwa kwa muda fulani na kwa baadhi ya watu. Lakini roho ya mwanadamu imeumbwa kuwa huru na haiko tayari kukubali kukandamizwa milele, kunyanyaswa daima au kupuuzwa bila kukoma. Roho ya mwanadamu ikishafikishwa mahali kwenye kona simba anapowindwa na kujikuta kwenye kona ya mlima akiwa amezungukwa na wawindaji mwanadamu hujitetea. Mwanadamu atajitoa mhanga kupigania nafasi ya kuwa haki, kupigania haki yake na thamani yake, mwanadamu atakuwa tayari kupoteza vyote ili kupigania utu wake. Matukio yote ya mabadiliko na hasa tuliyoyaona mwaka huu huko Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati yana ujumbe mmoja tu. Wananchi lazima wasikilizwe na mabadiliko yafanyike kwa njia ya amani, chaguzi lazima ziwe wazi, huru na za haki. Watawala ni lazima wawe tayari kushughulikia kero - siyo kwa ahadi bali kwa matendo na maamuzi thabiti. Pasipo kufanya hivyo wananchi watakata tamaa. Kama wananchi wanafika mahali na kuona mabadiliko wanayoyataka hayawezi kuja kwa sanduku la kura au kwamba, kwenye sanduku la kura sauti yao inapuuzwa na kukejeliwa, watajaribu tena na tena kuleta mabadiliko wa njia hiyo na kwa mazungumzo. Lakini ole wetu kama wananchi watafikia mahali waone kuwa njia za kidemokrasia za kuleta mabadiliko zimeshindikana. Ole wetu kama wananchi wataamua mgongano wao usiwe tena wa maslahi na fikra bali mgongano utakaolazimisha maslahi yao yasikilizwe kwa damu yao. Niandikie: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














