
| Kutoka London:Nidhamu ya David Beckham | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 20:34 |
|
Na Freddy Macha David Beckham anafahamika sana ulimwenguni leo. Sifa yake kuu kisoka ni ustadi wa kulipiga gozi toka mbali likaingia au kupasi mpira upande mmoja wa kiwanja hadi mwingine ukamlenga mshambuliaji sawasawa akafunga bao. Kutokana na ufundi huo mwaka 2002 sinema bab kubwa ya Bend It Like Beckham (ukunje mpira kama Beckham) ilionyesha timu ya wasichana Wahindi na Wazungu wakijitahidi kucheza kazuzu. Beckham atakayetimiza miaka 37 mwezi Mei ameichezea timu ya taifa ya Uingereza toka 1996. Alikuwa kiungo wa Manchester United kati ya 1991 na 2003. Husakata kandanda Marekani na timu ya LA Galaxy ambayo awali haikujulikana na miezi miwili iliyopita ilifika fainali kwa mara ya kwanza kutokana na mchango wake. Keshaichezea vilevile timu maarufu ya Hispania, Real Madrid na AC Milan ya Italia. Mwaka 2005 David alisaidia sana kuipigania nchi yake iwe mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki yatakayodata London, mwezi Agosti. Kuna mengi ya kuzungumza kuhusu mtu huyu aliyezaliwa hapa hapa London mwaka 1975. Nje ya mpira Beckham ni mtukuzaji mkubwa wa mavazi na urembo. Na si ajabu alipomwoa mwanamuziki mrembo wa bendi ya wanawake, Spice Girls (iliyoundwa 1994) ikatoka na kibao maarufu “Wanna Be” kinachosisitiza msimamo wa kina mama kwamba “ukitaka kuwa mpenzi wangu kwanza uwe rafiki yangu”... Mkewe huyo, Victoria Caroline Adam (aliyeitwa Posh Spice kutokana na kufutua futua mdomo) ni matajiri wa 19 nchini Uingereza- wakikadiriwa thamani ya paundi 125 milioni (zaidi ya shilingi bilioni 300)- na watoto wanne. Wavulana, Brooklyn Joseph (1999), Romeo James (2002), Cruz David (2005) na msichana Harper Seven (2011). Mafanikio haya nje na ndani ya maisha yake Beckham ndiyo yaliyochangia kutolewa na jarida la Afya ya wanaume la mwezi Machi, 2011. Jarida hilo la “Men’s Health” lilianzishwa Marekani miaka 25 iliyopita likizingatia dhamira za mazoezi ya viungo , chakula bora na afya. Limeshinda tuzo nyingi. Kumi na tano zilitolewa na chuo maarufu cha uandishi wa habari cha Columbia Marekani, moja kwa mhariri wake Mike Lafavore (1994) aliyesimamia jarida lilipoanzishwa na tuzo la jarida la kimataifa mwaka 1998. Men’s Health linauzwa nchi 20 na katika miaka kumi iliyopita idadi ya wasomaji wake imeongozeka haraka. Mathalan 2001 lilikuwa na wasomaji laki nne na 2006 wakafikia milioni moja na nusu. Jarida lina msimamo wa kutoweka matangazo ya pombe na sigara na kuzingatia afya ya wanaume kupitia makala zilizofanyiwa utafiti wa kisayansi na kitaaluma. Majarida ya aina hii yanazidi kukua nchi zilizoendelea. Huelekeza wananchi wake kuzingatia masuala ya kiafya kuliko nchi maskini zinazolenga zaidi siasa na uchumi. Moja ya jarida ya kale Australia ni “Women’s Weekly” lililoanzishwa mwaka 1933. Lina wasomaji nusu milioni, kurasa 240 na huandika mambo ya kina dada ambapo jarida kuu la Bara Hindi (India Today) lenye wasomaji 1,100,000 kila wiki huchapa habari za michezo, sayansi, matukio na historia. Jarida maarufu kuliko yote duniani “Reader’s Digest” limekuwa mstari wa mbele dunia nzima toka lilipoanzishwa Marekani mwaka 1922. “Reader’s Digest” linalomlenga Mzungu wa kawaida lina wasomaji milioni 40 na hutolewa katika lugha 21 tofauti ndani ya nchi 70. Ndiyo maana basi gazeti la Men’s Health limeamua kuanzia mwezi huu kutoa toleo la wanawake (Women’s Health). Mtindo wa jarida hili ni kumchukua mwanaume wa mfano katika jamii, likamhoji, likamuuliza anajiwekaje katika hali ya afya na kuitandaza picha yake jaladani. Maudhui yake huonyesha namna wanaume wa marika yote wanavyoweza kujitunza kupitia mazoezi, chakula, kujiendeleza kikazi na kushauri namna ya kujenga mahusiano yao na wanawake. Kwa mfano kutokana na mahusiano mabaya yaliyoko Uzunguni kati ya wanaume na wanawake leo ndoa huvunjika sana. Wanaume hupewa ushauri wa namna gani wanaweza kuwa wajuzi zaidi, nini siri ya kuwaelewa wanawake, nk. Kati ya watu maarufu walioshahojiwa ni mabondia Amir Khan na David Haye; mcheza tenisi Andy Murray, familia ya wapiganaji wa Jiu Jitsu ya Kibrazili (Gracie) iliyoanzishwa mwaka 1925 ; vile vile wafanyakazi wa kawaida : waalimu, polisi, wahudumu mahotelini, nk. Watu hawa huulizwa wamefanyaje kuwa na miili isiyokuwa na mafuta au vitambi, wamejengaje misuli na ushupavu, hunywa na kula nini, nk. Toleo la sasa basi limemchagua David Beckham. Je, anajisikiaje? Je umaarufu umemvimbisha kichwani? La hasha, anajibu. “Toka utotoni nilichotaka ni kuwa mcheza mpira wa kulipwa. Sasa mimi mchezaji mpira wa kulipwa. Haja yangu haikuwa kuwania umaarufu.” Anaulizwa je wanawe wako kawaida? Maana watoto wa vigogo na mamilionea huzeeka kutokana na maisha ya kibwanyenye. Beckham anasema babu na baba wote walicheza mpira viwanja vya Hackney Marsh (Mashariki ya London) na yeye akaanza kusakata kazuzu hapohapo viwanja vya Hackney Marsh ambapo si mbali na michezo ya Olimpiki itakapofanyika. Anasisitiza Baba na Mama yake walikuwa (na bado) ni wachapa kazi wakubwa. Anahimiza kuwa tabia na itikadi hii ya kuponda uvivu, kuchapa kazi, imemjenga, anaipenda na anaendelea kuifuata yeye na mkewe na wanawe na anahusudu sana kuwa mshindi, kuwa bora kwa chochote anachokifanya. Mwishoni anaelezea siri ya mazoezi yake. Anasema kujiweka alivyo mbali na mpira, zoezi lake kuu ni la Mbio. Anashauri kuwa na mpangilio wa majuma matano. Juma la kwanza unakimbia kwa dakika 5, unapumzika dakika 4, kisha unarudia tena mara tatu. Juma la pili unakimbia dakika mbili, unapumzika dakika mbili, unarudia yote mara saba. Wiki ya tatu unakimbia haraka sana dakika moja, unapumzika dakika moja, unarudia mara 15. Wiki ya nne unakimbia mbele na kurudi haraka sekunde 20, unapumzika dakika moja; unarudia tena mara 10. Wiki ya tano unakimbia haraka dakika moja, unapumzika dakika moja unarudia mara kumi. Anasema ukifanya hivyo utakuwa safi (fiti) daima. Anashauri kupumzika siku mbili baada ya kila zoezi kali. Kwamba ni kosa kufanya mazoezi kila siku. Kwamba mazoezi ya mwili ndiyo siri ya maendeleo ya akili na kuwa mshindi wa maisha na mazingira. Barua pepe: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it Tovuti: www.freddymacha.com |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














