
| Mkapa: Afrika isiyumbishwe na mataifa ya Magharibi | Send to a friend |
| Tuesday, 31 August 2010 22:06 |
|
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amezitaka nchi za Afrika kutoyumbishwa na propaganda za mataifa ya Magharibi kwamba wimbi la Wachina kuwekeza Afrika, linaweza kuwafanya Waafrika kupoteza ardhi yao. Badala yake amezitaka nchi za Afrika kuweka mfumo mzuri wa majadiliano na Wachina, ili kushirikiana nao katika matumizi ya ardhi kwa lengo la kuzalisha kwa wingi na kukuza uchumi. “Msije mkababaishwa kwamba wawekezaji Wachina wana lengo la kuwanyonya na kuwanyang’anya ardhi Waafrika. Kinachotakiwa ni mpango mzuri wa kujadiliana nao na kuweka mfumo mzuri kwa manufaa ya kiuchumi,” alisema Mkapa baada ya marais wastaafu wa nchi za Afrika kumaliza mkutano wao Jijini Dar es Salaam jana. Mkapa alikuwa akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari kuhusu propaganda zinazoenezwa na mataifa ya Magharibi ya kuzihadharisha nchi za Afrika kuwa Wachina wanaweza wakawanyonya na hata kuchukua ardhi yao. Katika mkutano huo wa siku mbili uliojadili na kutoa mapendekezo kuhusu mabadiliko ya usimamizi wa ardhi katika barani Afrika, uliwashirikisha marais sita wastaafu pamoja na wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika. "Jambo la muhimu nchi za Afrika zinapaswa kuchunguza na kujua ni mwekezaji gani ambaye ana uwezo wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi haraka na kuwaletea wananchi maendeleo, na siyo kuangalia ni nani watashirikiana naye" alisema Mkapa. Alisema hayo wakati uchumi wa China umeonekana kukua kwa haraka katika miaka ya karibuni na hata kuyashangaza mataifa ya Magharibi na kutishia kumiliki sehemu kubwa ya uchumi wa dunia. Akielezea mambo waliojadiliana kwenye mkutano huo, Rais Mstaafu wa Mauritus, Karl Offmann alisema suala la ardhi barani Afrika wameliona ni jambo nyeti ambalo linayumbishwa na misimamo mbalimbali ya kisiasa. Offmann alisema hawawezi kusema kwamba suala la ardhi Afrika halijatumika vizuri katika kuwaletea maendeleo Waafrika ila wana wasiwasi kasi ya ongezeko la watu, inaweza kuleta matatizo zaidi katika miaka ijayo. “Tunaposema idadi ya watu Afrika ni kubwa tunalinganisha na mabara mengine. Afrika imeonyesha kasi ya ongezeko la watu. Kwa mazingira hayo ni wazi matatizo yanaongezeka. Hali hiyo inaashiria kwamba sasa ni wakati wa kutatua matatizo yanayotokana na suala la umiliki wa ardhi,” alisema Offmann. Offmann alisema tatizo kubwa kwa nchi za Afrika ni kuweka usimamizi mzuri wa ardhi ni mawasiliano duni kama vile barabara na reli, hivyo masuala hayo, yanayopaswa kuwekewa kipaumbele. |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Links za wateja na washirika wetu
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani












