MwanzoContactsEmail
Home Habari Habari za Kitaifa Jaji Mkuu awaonya wanasiasa nchini
BOOKMARK THIS PAGE
Jaji Mkuu awaonya wanasiasa nchini  Send to a friend
Tuesday, 31 August 2010 22:09

Fredy Azzah na James Magai
JAJI Mkuu wa Tanzania, Augustine Ramadhani amewaonya wanasiasa wanaozungumzia kesi mbalimbali zilizopo mahakamani, katika majukwaa ya siasa. Jaji Ramadhani alisema kuzungumzia kesi ambazo bado zinasikilizwa na mahakama mbalimbali, ni kinyume na sheria za nchi.

Katika uzinduzi wa kampeni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zilizozinduliwa Agosti 29, mwaka huu, kada wa chama hicho na mwanasheria mkongwe nchini, Mabere Marando aligusia kesi za wizi wa fedha za Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) zinazoendelea.

Mbali na kesi hiyo ya EPA, katika hotuba yake pia alisema kumfunga Amatus Liyumba pekee yake siyo dawa ya kumaliza ufisadi nchini, bali viongozi hao ndiyo wanaotakiwa kufungwa.  Alisema wamemfunga Liyumba ili waonekane kwa wananchi kwamba wanapiga vita ufisadi.  "Jamani hivi fedha zote zilizoliwa pale Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni Liyumba pekee yake aliyeziiba?, Tunajua ametolewa kama mbuzi wa kafara," alisema Marando.

Jaji Ramadhani  alitoa onyo juu ya kauli hizo  jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kwa semina ya siku tatu ya majaji  wa mahakama za nchi 12 za Afrika. Semina Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

“Kesi zote zilizopo mahakamani hazitakiwi kuzungumziwa nje ya mahakama, mimi mwenyewe wakati kesi ya mgombea binafsi ilipokuwa mahakamani nilikuwa sitaki kuizungumzia nje ya mahakama,” alisema Jaji Ramadhani.  

Kuhusu hatua watakazochukuliwa watu wanaozungumzia kesi zinazoendelea mahamani, jaji huyo alisema hawawezi kutoka mahakamani na kwenda  kuwashika watu na kuwafungulia kesi na kwamba mtu atakapeleka  malalamiko juu ya vitendo hivyo, watayafanyia kazi.

Awali akifungua semina hiyo, rais Karume alisema  bila kuwa na ushirikiano wa kutosha vitendo vya ugaidi na uhalifu wa kimataifa hautawezwa kukomeshwa.
 
Aliwataka majaji waliohudhuria semina hiyo, kubadilishana uzoefu ili kupata njia sahihi ya kukabiliana na matatizo hayo.

“Kutokana na kukua kwa na teknolojia uhalifu wa kimataifa na ugaidi unaendelea, kwetu ni  matatizo makubwa, inatakiwa tukae pamoja na kujadili njia za kumaliza hili tatizo, tunatarajia mkutano huu utatoa  majibu ya matatizo haya,” alisema Rais Karume.

Pia aliwataka majaji hao, kujadili na kuelewa ipasavyo juu ya mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC.

Naye Jaji Ramadhani akizungumzia mahakama hiyo alisema wanachukua tahadhari na kupata uzoefu wa kushughulikia kesi za ugaidi na uharamia kutokana na matukio yanayotokea katika nchi za jirani.

"Hivi karibunu watu wameuliwa na magaidi nchini Uganda, sasa kwanini na sisi tusijiadhari,” alihoji Jaji Ramadhani.

Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa  katika semina hiyo ni pamoja na Ugaidi Mashariki na Kusini mwa Afrika, jukumu la mfumo wa kisheria wa thalifu katika kukabiliana na ugaidi na mapitio ya sheria ya kuzuia ugaidi ya Tanzania ya mwaka 2002.

Nyingine ni Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) na uwezo wake wa kisheria,  hifadhi ya mashahidi, kinga na misamaha kwa wahalifu wa kimataifa na nguvu ya amani na haki katika mkitadha wa uhalifu wa kimataifa.

Pia washiriki wa semina hiyo watajadili mada kuhusu  matatizo na ushirikiano wa mashirika yanayopambana na uhalifu katika kupambana na ugaidi.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?