|
Hussein Kauli TUME ya Vyuo Vikuu (TCU) imesema kuanzia wiki ijayo itaanza kupokea awamu ya pili ya maombi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na taasisi za elimu ya juu kwa kutumia mfumo mpya wa udahili wa wanafunzi. Afisa uhusiano wa tume hiyo, Edward Mkaku aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kulikuwa na kasoro nyingi kwenye awamu ya kwanza ya udahili na kusababisha waombaji wengi kukosa nafasi.
Alisema baada ya kukamilisha kutoa ya matokeo wanafunzi waliochaguliwa kesho, watafungua tena mitambo ya kudahili wanafunzi kuanzia wiki ijayo ili wanafunzi wenye matatizo waombe upya. “Siwezi kusema utaanza siku gani na kutakuwa na awamu nyingine zaidi kumaliza matatizo yaliyopo,” alisema Mkaku. Alisema baada ya kumaliza kutoa matokeo yote watatoa majina ya wanafunzi walikosea kwenye maombi yao ili waweze kuomba upya kwa kutumia mfumo huo mpya wa udahili.
Alibainisha kuwa matatizo mengi yaliyotokea yalimesababishwa na wanafunzi kutoelewe vyema mfumo huo, hivyo kufanya maombi yasiyo sahihi kutokana na sababu mbalimbali. “Tatizo la wanafunzi kudahiliwa kwenye kozi ambazo hawakuzichagua limesababishwa na wao wenyewe kutokuwa makini wakati wa kuomba nafasi hizo,” alisema Mkaku. Alifafanua kwa kuwa kozi ziliwakilishwa na namba za mpangilio (code number), hivyo wako wanafunzi waliochagua namba bila kuangalia inawakilisha kozi gani, matokeo yake wakachagua kozi wasizozitaka.
“Yupo mwanafunzi alikuja hapa; yeye amefaulu kwa daraja la kwanza nukta nne kwenye mchepuo wa (historia, kiswali na lugha) HKL, lakini aliomba BS in Engineering, na amedahiliwa kwenye kozi hiyo. Sasa huyu hakuwa makini wakati wa kuchagua kozi,” aliongeza Mkaku. Aliongeza kuwa wapo wanafunzi walioomba vyuo kwa kutumia mitandao mingine ya simu za mkononi badala ya Vodacom, hivyo maombi yao hayakufika TCU na hivyo kutochaguliwa.
Kutokana na matatizo hayo na mengine, Mkaku alisema bado udahili haujakwisha na aliwataka wanafunzi kusubiri kwani watatoa majina ya wanafunzi waliokosea. “Baada ya kukamilisha kutoa matokeo ya awamu ya kwanza tutafanya uteuzi kwa awamu ya pili na huenda tukafanya uteuzi wa awamu nyingine ili kuhakikisha tunamaliza matatizo yote,” alisema Mkaku.
Kwenye ofisi za TCU juzi, wanafunzi wengi walikuwa wakilalamika kutochaguliwa na wengine kuchaguliwa kwenye kozi ambazo hawakuziomba. “Mimi nimetoka Arusha nimekuja hapa kujua hatma yangu, kwa sababu matokeo yangu ya kidato cha sita yalikuwa mazuri tu lakini sikuchaguliwa na rafiki yangu niliyempita, amechaguliwa kwenye kozi kubwa bila kuliko ufaulu wake,” alisema mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Rahim Bendera. Mmoja alidai amekuta jina lake lakini namba siyo yake na mwingine alikuta namba yake, lakini jina la mtu mwingine.
|
Comments
UNAJUA LAZIMA TUANGALIE NI WATANZANIA WANGAPI WANA UWEZO WA KUPATA TAARIFA KUPITIA MITANDAO KWANI KUNA SEHEMU HATA SIMU HAZIKAMATI NETWORK
KWA HIYO NINAIOMBA SERIKALI IUPITIE HUU MFUMO KWA UPYA.TUSIWE WEPESI WA KUWALAUMU WAHITIMU BILA KUANGALIA NINI KIMEMSIBU.