
| ‘Siasa zimechangia uporaji rasiliamli nchini’ | Send to a friend |
| Wednesday, 22 February 2012 21:02 |
|
BAADHI ya maofisa wa Serikali wamesema viongozi wa siasa nchini huingilia masuala ya utaalamu kwa lengo la kuwapendelea wawekezaji wanaopora rasilimali za taifa. Wakizungumza kwenye kongamano la saba la kitaifa kuhusu masuala ya ardhi, lililoandaliwa na asasi ya HakiArdhi Dar es Salaam jana, maofisa hao kutoka wizara za Nishati na Madini, Kilimo na Chakula, Ardhi na Kituo cha Uwekezaji (TIC), walisema uamuzi mwingi unaotolewa na viongozi wa Serikali hukiuka ushauri wa kitaalamu. “Msiwalaumu maofisa wa Serikali kwa kuchangia uporaji rasilimali. Tatizo ni siasa zinazoingilia ushauri wa kitaalamu. Naweza kusema mwekezaji huyu hafai kupewa ardhi, lakini mwanasiasa analazimisha apewe na ukikataa unaweza kufukuzwa kazi akawekwa mwingine,” alisema Hansi Msemo kutoka TIC na kuongeza: “Kuna mambo mengi yanafanyika humu nchini kwa sababu ya uamuzi wa wanasiasa tu. Mbona hata wanyama wanachukuliwa kwa ndege na kusafirishwa nje ya nchi? Inabidi sasa tuangalie upya Katiba yetu kuhakikisha kuwa haitoi mwanya kwa wanasiasa kuruhusu uporaji huo.” Hata hivyo, Msemo alisema wawekezaji wa kigeni na wenyeji, wote wana haki na wajibu sawa mbele ya sheria na iwapo Serikali ikibaini kasoro huzirekebisha. Naye Mtunzi Suleiman ambaye ni Mwanasheria katika Wizara ya Nishati na Madini, aliunga mkono kauli ya Msemo akisema wanasiasa wamechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo. “Siasa imetuathiri sana. Mimi kama mwanasheria naweza kushauri kitaalamu, lakini siasa zinakuja, mwisho unajiuliza, uache kazi au vipi?” alihoji Suleiman. Aliongeza kuwa sheria za madini hazifafanui suala la ardhi, hivyo kuweka njia panda haki za wananchi kutetea haki zao pale mwekezaji anapohitaji ardhi kwa ajili ya kuchimba madini. “Tunahitaji kuboresha sheria zetu hasa wakati huu tunapozungumzia mabadiliko ya Katiba, ili tuwe na mamlaka ya kudhibiti ardhi,” alisema Suleiman. Naye Mwanasheria kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Flora Tenga, alisema uamuzi wa kisiasa ndiyo unaodhoofisha utendaji wa Serikali. Hata hivyo, Jane Kapongo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema halmashauri za vijiji na wilaya ndizo zinapaswa kulaumiwa kwa kutokuwa makini katika utoaji ardhi kwa wawekezaji. |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani















Comments