|
Leon Bahati na Mussa Mkama
WADAU wa masuala ya elimu nchini wamepinga vikali hatua ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kukifunga chuo hicho wakisema, hatua hiyo haikuzingatia masuala muhimu ya msingi kitaaluma na haitasaidia kupunguza matatizo bali itachochea zaidi tatizo na kusababisha madhara zaidi kwa watoto wa masikini.
Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alisema kuwa, serikali ingepaswa kuwasikiliza na kwamba kuwasimamisha masomo ni kutumia ubabe uliopindukia.
"Hatua iliyochukuliwa ni sawa na kutumia rungu kuua nzi. Kama tuliweza kuwa na uvumilivu na mafisadi wa EPA (Akaunti ya Madeni ya Nje) tangu mwaka 2005, imeshindikana nini kuwa na 'dialogue' (mazungumzo) na wanafunzi hawa?" alihoji Mrema.
Alikosoa vigezo vinavyotumiwa na Bodi ya Mikopo katika utoaji wa mikopo, akitoa mfano wa sula la walemavu kupewa mikopo ya asilimia 100 bila kujali wametoka katika familia zinazojiweza au la.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria, Dk Sengodo Mvungi amesema sera ya uchangiaji elimu ya juu ilitungwa na Benki ya Dunia na sera hiyo ni kwa ajili ya nchi tajiri na si masikini kama Tanzania.
Alisema mgomo wa wanafunzi hao ni wa haki na utaendelea kuwa wa haki. Aidha alisema katika wanafunzi 18,000 walio nao ni wanafunzi 6,000 tu ndio waliosajiliwa kuendelea na masomo, kwa hiyo wanafunzi 12,000 hawajasajiliwa kutokana na kutolipa ada je wataingiaje madarasani.
Waziri anatoa amri ya kuwataka wanafunzi wote kuingia madarasani kuachana na mgomo, wataingiaje wakati hawajasajiliwa.
"Tuna wanafunzi 12,000 ambao hawajasajiliwa kutokana na kutolipa ada, hao wataingiaje madarasani wakati hawatambuliki, ni lazima wagome ili wapewe mikopo waingie madarasani," alisema Mvungi.
Alisema wapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza hadi wa nne ambao hawajaonyeshwa matokeo yao ya mtihani kwa sababu hawajalipa ada sasa wanaambiwa waingie madarasani wakafanye nini ilihali serikali haijawapa mikopo hiyo.
"Tuna wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza hadi wa nne hatujawaonyesha matokeo yao ya mitihani kutokakana na kutolipa ada wapo tu chuoni kama kivuli, bodi bado inawasumbua inawapa mikopo kwa ubaguzi, hakuna mtoto wa tajiri ambaye hajapewa mkopo," alisema Dk Mvungi.
Nacho Chama cha Wananchi (CUF) kililaani hatua iliyochukuliwa dhidi ya wanafunzi hao na kudai kuwa njia ya mazungumzo ilikuwa mwafaka.
"Kwa jinsi nilivyokuwa nawasikiliza wanafunzi hao kupitia kwenye televisheni, walionyesha wazi kuwa serikali ingeweka wazi mfumo wa mazungumzo, wasingeendelea kugoma," alisema Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Alfred Lwakatare.
Chama cha NCCR-Mageuzi kilitoa msimamo kuwa serikali ikiamua inaweza kuwapatia wanafunzi mikopo ya asilimia 100 na kwamba, picha inayoonekana kwa sasa ni suala la elimu ya juu kutotiliwa mkazo kama ilivyo masuala mengine hasa yanayohusu maslahi ya viongozi serikalini.
"Hivi leo serikali ingeamua, badala ya kununua magari ya bei mbaya kwa viongozi kama vile mashangingi na kununua mazuri ya kawaida ya bei ya chini, tungeshindwa kuwakopesha vizuri wanafunzi hawa?" Alihoji Mkuu wa Idara ya Organaizesheni, Kampeni na Uchaguzi ya NCCR, Faustine Sungura.
Alikosoa pendekezo lililotolewa hivi karibuni na CCM la wilaya zote nchini kufanywa majimbo, akidai kuwa mpango huo haufai kwa sababu utaongeza matumizi ya kuendesha serikali pasipo sababu ya msingi.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, Hiza Tambwe alikuwa na maelezo tofauti na vyama hivyo vya upinzani kwa maelezo kuwa walichofanya wanafunzi hao ni kinyume na mikataba waliyoingia na Bodi ya Mikopo.
"Kama mtu alijaza na kusaini fomu ya bodi ya kupatiwa asilimia 60, akapewa na kwenda chuoni, akasoma mwaka wa kwanza, halafu mwaka wa pili akaanza kugoma na kusema fedha hazitoshi, hii naona siyo sahihi," alisema Tambwe.
Alifafanua kuwa kama ni kugoma walitakiwa kuanza kugomea kusaini mikataba ile hivyo walipaswa watambue haki zao kulingana na mkataba.
Tambwe alielezea kusikitishwa na kitendo cha wanafunzi waliokuwa kwenye mgomo kuwalazimisha wenzao ambao hawakuwa wanaunga mkono hoja hiyo. Alielezea kitendo hicho ni kinyume cha haki za binadamu na kinapaswa kukemewa vikali.
Kuhusu suala la mizozo na mivutano mbalimbali ambayo ilitafsiriwa na wapinzani kama alama za nyakati za nchi kuelekea katika wakati wa kutotawalika, Tambwe alisema kuwa ni propaganda za wapinzani.
"Haijawahi kutokea wapinzani kuunga mkono utawala uliopo madarakani. Hivyo katika hili hakuna jipya," alisema Tambwe akiisifu CCM kuwa imetoa uwanja mpana wa demokrasia nchini, jambo ambalo linawapa fursa wapinzani kuropoka lolote wanalofikiria ni la kukiponda chama tawala.
Alielezea mizozo iliyojitokeza kuwa inatokana na serikali ya awamu ya pili kutoa nafasi kwa kila mtu kueleza madukuduku yake na kwamba kila jambo linashughulikiwa kwa kuzingatia taratibu.
Aliponda shutuma hizo kwa maelezo kuwa, wanachotaka wapinzani ni serikali kushughulikia mambo kwa papara jambo ambalo linaweza kuwa hatari kwa taifa.
|