|
Na Emmanuel Muga
UAMUZI wa Mahakama Kuu wa kuwaachia huru washtakiwa wote katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva mmoja wa teksi iliyomuhusisha mkuu wa zamani wa upelelezi mkoani Dar es salaam, Abdallah Zombe na wenzake, jana ulipokewa kwa maoni tofauti huku baadhi ya watu wakionyesha mshangao.
Mtu mmoja aliuliza: "Kwa hiyo ina maana wale waliouawa walikuwa majambazi? Kweli sheria ina vituko vyake."
Mwingine akasema: "Kila kitu kilikuwa wazi, mahakama imewaachia vipi wakati baadhi ya askari walikiri, hivi hii ndio sheria?"
Kweli kabisa sheria ndivyo ilivyo na inakuwa vigumu kwa baadhi ya watu kuelewa mwenendo wa mahakama na jinsi inavyofanya kazi.
Kwa maoni ya baadhi ya watu, Zombe na wenzake walikuwa na hatia na walikuwa wakisubiri tu Jaji Salum Masatti athibitishe hilo.
Binafsi nilijua kuwa Zombe angeachiwa huru.
Katika kesi hiyo, Zombe na wenzake walishtakiwa kwa kuua wafanyabiashara hao watatu, yaani Sabnus Chigumbi, Ephrahim Chigumbi na Mathias Lunkombe pamoja na dereva wa teksi, Juma Ndugu.
Polisi ilieleza kuwa watu hao ni majambazi ambao walihusika na wizi wa fedha kwenye benki jijini Dar es salaam na waliuawa wakati waliporushiana risasi na askari maeneo ya Sinza.
Lakini baada ya pande zote mbili kuwasilisha ushahidi, kwanza tukumbuke kuwa wakati Jaji Masatti alikiri kuwa ushahidi ulikuwa unajichanganya wakati alipokuwa anafunga kesi.
Ushahidi kujichanganya ni mojawapo ya sababu kubwa za kumwachia huru mtuhumiwa.
Sheria ya makosa ya jinai inataka anayeshtaki, yaani mwendesha mashtaka, atoe ushahidi usioacha shaka kabla ya mshtakiwa hajatiwa hatiani.
Yaani waendesha mashtaka walitakiwa wathibitishe bila ya kuacha shaka kwamba, Zombe na wenzake waliua watu hao kwa kukusudia na endapo inaonekana kuwa kuna shaka kama waliua, basi huwezi kumtia hatiani mtuhumiwa kwenye kosa kama hilo, ambalo adhabu yake ni kuchukua maisha ya mtuhumiwa.
Na Wazee wa Baraza, wakati wakitoa maoni yao, walieleza hivyo kuwa hakuna aliyemtaja Zombe na baadhi ya watuhumiwa kuwa waliua na hivyo kumshauri Jaji amwachie huru afisa huyo mwandamizi wa polisi, na ndivyo alivyofanya Jaji Masatti.
Hata upande wa mashtaka ulipoomba kuwa Zombe atiwe hatiani kwa kushiriki kosa baada ya kosa, au kwa maneno mengine kujua kuwa kulikuwepo na kosa na kutoshtaki au kushiriki kwa njia nyingine yoyote ile, bado Jaji Masatti alisema hangeweza kumtia hatiani kwa kosa ambalo hakushtakiwa.
Yaani Zombe na wenzake walishtakiwa kwa kuua na si kwa kushiriki mauaji.
Mtu aliyetekeleza mauaji hayo, Saad Alawi, yaani anayetuhumiwa kuwaua watu hao, hajapatikana hadi sasa.
Ushahidi wa mwendesha mashtaka ukiacha shaka, basi faida inakuwa kwa mshtakiwa. Siku zote kuna msigano kati ya haki kwa kufuata sheria na haki kwa maoni ya watu wengi, ambao katika kesi hii walitarajiwa kuona Zombe akitiwa hatiani.
Haki kwa kufuata sheria siku zote inawalinda watuhumiwa, kwa sababu mwenendo na kanuni zote zinawapendelea watuhumiwa, ili upande unaoshtaki uweze kuthibitisha tuhuma zake dhidi ya washtakiwa.
Siku zote wanafunzi wanaosoma somo la Sheria za Jinai, wanakumbushwa kuwa ni bora kuwaachia wahalifu 99 kuliko kumfunga mtu mmoja ambaye hana hatia.
Hii ni dhana inayofuata mfumo wa sheria ya Uingereza na ambayo pia inatumiwa na mahakama za Tanzania. Mfumo huu unafaaa zaidi kutumika kwenye nchi zilizoendelea na si kwenye nchi kama Tanzania ambayo iko nyuma kwa mambo mengi.
Nchi zilizoendelea zina teknolojia, vitendea kazi na ufanisi mkubwa unaowafanya wapelelezi na waendesha mashtaka kufanya kazi kwa uhakika na hivyo kutengeneza ushahidi ambao hauachi shaka.
Na Uingereza ilipitia kwenye hatua mbalimbali kabla ya mfumo wake wa kutoa haki haujaimarika. Huko nyuma Mfalme alilazimika kuunda mahakama ya kutoa haki ya ukweli, yaani 'equity' baada ya kuona mahakama za kawaida hazitoi haki ya ukweli.
Watu waliodhani mfumo wa mahakama za kawaida haukuwa unatenda haki, walienda moja kwa moja kwa mfalme ambaye ndio alikuwa kisima cha haki kupitia mahakama yake maalumu.
Baadaye mfumo wa mahakama ya mfalme na ule wa mahakama za kawaida iliunganishwa na kuwa na mfumo mmoja.
Tukirudi kwenye kesi ya Zombe, huenda wapelelezi wa kesi na waendesha mashtaka wangefanya kazi yao vizuri matokeo ya kesi yangekuwa tofauti. Lakini hii ndio sheria na lazima tukubali.
Maoni haya yameandikwa na Emmanuel Muga ambaye ni msanifu habari wa gazeti la The Citizen.
|