|
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema bado inatafakari hatua za kuchukua baada ya Mahakama Kuu kutowatia hatiani washtakiwa tisa katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Morogoro na dereva mmoja wa taksi.
Jaji Salum Masatu alisema katika hukumu yake kuwa waliohusika na mauaji hayo hawako mahakamani na hivyo kuifanya kesi hiyo kuwa nguvu kwake kuwatia hatiani washtakiwa hao tisa, akiwemo mkuu wa zamani wa upelelezi mkoani Dar es salaam, Abdallah Zombe ambaye alikuwa mshtakiwa namba moja.
Kwa maana hiyo, Jaji Masati aliwaachia huru washtakiwa wote tisa waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la kuua kwa makusudi wafanyabiashara hao watatu, Sabinus Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathis Lunkombe pamoja na dereva wa taksi wa Sinza jijini Dar es salaam, Juma Ndugu.
“Siwezi kusema lolote kwa sasa kama tutakata rufaa au la," alisema mwanasheria mwandamizi wa serikali, Jackson Kashozi.
“Msimamo tutautoa mara baada ya jopo la wanasheria wa serikali kukutana ndani ya siku kumi na nne ambazo ndizo zinazoruhusiwa kisheria kukataa rufaa kama upande mmoja haujaridhika.”
Zombe na wenzake walishtakiwa kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia, kesi ambayo upande wa mashtaka unatakiwa uthibitishe bila ya kuacha shaka kuwa wahusika ndio waliotekeleza mauaji hayo.
Lakini Jaji Masati alisema hakuona sehemu ambayo washtakiwa hao walihusika katika mauaji hayo, jambo ambalo litawalazimisha wanasheria wa serikali kuandaa mashtaka mapya iwapo watataka Zombe na wenzake waadhibiwe kwa kushiriki kosa baada ya kosa kutendeka kama upande huo ulivyoomba wakati ukifanya majumuisho yake.
Wakati upande wa mashtaka ukifanya majumuisho, uliomba mahakama imuone Zombe na baadhi ya watuhumiwa kuwa ana hatia ya kuua kwa makusudi na kama haitamtia hatiani kwa kosa hilo, basi imuhukumu kwa kufanya kosa baada ya kosa, jambo ambalo Jaji Masati alilikataa kwa maelezo kuwa atawahukumu kwa kosa waliloshtakiwa. |