Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::8/29/2009
Waraka wa Waislamu waionya serikali 2010
Waumini wa dini ya Kiislamu wakigombea kununua waraka wa waislamu kuhusu uchaguzi mkuu ujao baada ya kuzinduliwa rasmi jana jijini Dar es Salaam

Salim Said na Ummy Muya

SHURA ya Maimamu Tanzania imezindua rasmi mwongozo wa pamoja kwa Waislaam kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Waraka huo, ambao umetumia maneno "sidanganyiki kwa wanasiasa wasio waaminifu na kupiga kura ya kundi" unawaelezea waumini wa dini ya Kiislamu sifa za kiongozi anayefaa kuchaguliwa katika chaguzi zijazo.

Mwongozo huo una kurasa 45 na sehemu 19 zinazoeleza taswira ya uchaguzi wa mwaka 2005, dhana ya uchaguzi, uhuru wa kutoa maoni, tumefikaje hapa tulipo, maadili, elimu, afya, kilimo, fedha na uwezeshaji, maisha bora, sheria, umoja na amani, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uwakilishi wa umma, hadaa za uchaguzi na dira katika uchaguzi na hitimisho.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo uliohudhuriwa na mamia ya waislamu kutoka mikoa 22 ya Tanzania na kufunguliwa na amiri wa shura ya maimamu, Sheikh Mussa Kundecha, mhadhiri wa msikiti wa Idrisa, Sheikh Ally Basaleh aliwataka Waislamu kushikamana na kupiga kura kama kundi maslahi na kuwaambia wanasiasa wasio waaminifu kuwa hawadanganywi tena kwenye chaguzi.

Katibu wa kamati kuu ya siasa ya Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda ndiye aliyezindua mwongozo huo.

"Waislaam nchini tumedanganywa sana na wanasiasa wasio waaminifu chini ya serikali ya Chama cha Mapinduzi, lakini kuanzia sasa tunaingia katika uchaguzi na kupiga kura ya maslahi kama kundi maslahi, na hili si jambo baya," alisema Sheikh Basaleh.

"Tumedanganywa, hatukudanganywa? Tumedanganywa, hatukudanganywa," alihoji Basaleh na kujibiwa na umati wa waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kiislaamu kwa sauti ya pamoja wakisema: "Tumedanganywaa."

Alisema: "Katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na ule wa urais, wabunge na madiwani mwakani, waislamu tuseme hatudanganyiki."

Aliwaeleza kuwa kura itakayomkomboa kila mwananchi ni kura ya maslahi pekee.

Awali akifungua mkutano huo, Sheikh Mussa Kundecha aliiomba serikali kuufuata mwongozo huo ili kuweza kuzitawala nyoyo za wananchi na kwamba iwapo itaupuuza itawaongoza wananchi katika maafa makubwa ambayo hayajawahi kutokea nchini.

"Mwongozo huu ni wa watu wote na Waislaam. Serikali ... ikiupuuza itawaongoza wananchi katika maafa makubwa ambayo hayajawahi kutokea nchini hata mara moja," alisema Sheikh Kundecha.

Kwa mujibu wa Kundecha, mwongozo huo umetolewa baada ya serikali kushindwa kudhibiti makundi ya dini kutoa maoni yao binafsi, kitu ambacho alisema kinalenga kuvuruga amani, usalama na umoja wa kitaifa.

Aliilaumu serikali kwa kushindwa kuwashirikisha Watanzania katika mambo yanayowahusu na Waislaamu katika mambo yanayowahusu.

"Kwanza, tunakutana hapa kama Waislaam; pili kama Watanzania ili kuieleza serikali kwamba inapaswa kuwashirikisha Waislaam mapema katika mambo yanayowahusu bila ya kushinikizwa," alisema.

Mjumbe wa kamati kuu ya siasa ya shura ya maimamu, Sheikh Mohammed Issa alisema Tanzania ina makabila 120 na watu zaidi ya milioni 40 hivyo serikali inapaswa kujenga umoja katika makabila hayo badala ya kuendeleza ubaguzi mtu, dini na ukabila.

"Ukifanya ubaguzi wa aina yoyote unatengeneza bomu na dhambi kubwa isiyofutika. Kwa Tanzania, Waislaam ndio waliobeba uhuru na ukombozi wa nchi hii," alisema Issa.

"Waislaam hawapaswi kukubali kudhulumiwa hata kidogo na serikali haipaswi kufanya ubaguzi wa aina yoyote kwa sababu sote tunaipenda nchi yetu, sote tuna haki ya nchi yetu na sote ni muhimu na hakuna aliye muhimu zaidi kuliko mwingine."

Alisema wazee wa kiislaam walisimama katika viwanja vya Mnazi Mmoja miaka 50 iliyopita kupambana na dhulma, uonevu na kudai ukombozi wa Tanzania na kwamba na wao wamekutana hapo kufanya kama kile kilichofanywa na wazee hao.

"Tutachagua kiongozi mwenye imani ambaye atakuwa muadilifu na hatutakubali kubabaishwa na suti ya mtu yeyote. Sisi kuingia katika uchaguzi kama kundi maslahi si dhambi," alisema Issa.

Pia alimshukia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Philip Marmo kwa kuwaonya Waislaam kutoa mwongozo huo wakati alishindwa kufanya hivyo kwa waraka wa Kanisa Katoliki uliotolewa miezi kadhaa iliyopita.

"Hii yote ni kwa sababu serikali haina mdomo mbele ya kanisa na hata Kingunge ambaye alionya waraka huo amezidiwa nguvu na kufunga mdomo kwa kusema 'No Comments' alipoulizwa na vyombo vya habari juzi,"alisema.

Baada ya hotuba hizo, mwongozo huo ulianza kuuzwa kwa Sh2,000 kwa nakala na watu walijipanga kwenye misululu wakisubiri kununua waraka huo.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-