|
| Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi ambaye inadaiwa kuwa amejiuzulu wadhifa wake na nafasi yake kuchukuliwa na David Kitundu Jairo aliyekuwa katibu wa rais Jakaya Kikwete |
 |
Na Boniface Meena
MMOJA wa watuhumiwa wa kashfa ya mitambo ya kufua umeme ya Richmond Development (LLC), ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi amestaafu wadhifa wake huo na nafasi yake imechukuliwa na David Kitundu Jairo, aliyekuwa Katibu wa Rais Jakaya Kikwete.
Mwakapugi amestaafu wakati serikali ikisubiriwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Kampuni ya Richmond kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mkutano wa 17 wa Bunge unatarajiwa kutawaliwa na mzimu wa Richmond, ambayo ilipewa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura mwaka 2006 kwa njia ambazo zilionekana kukiuka taratibu na kusababisha Bunge liunde kamati teule iliyotoa taarifa ambayo iliwahusisha baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu ya nne.
Kufuatia kuibuka kwa kashfa hiyo, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu wadhifa wake huo baada ya kuhusishwa katika sakata hilo.
Katika mkutano wa 16 wa Bunge uliomalizika mwishoni mwa Agosti mwaka huu mjini Dodoma, serikali ilijaribu kuwasafisha maafisa wake waandamizi; mpango ambao ungewasafisha pia mawaziri waliojiuzulu, lakini Bunge likagoma na kuiagiza serikali kutekeleza maazimio yake kwa kuwawajibisha maafisa hao.
Mwakapugi ni mmoja wa watuhumiwa waliokuwa wakichunguzwa kuhusu kashfa ya Richmond na wengine ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(Takukuru), Dk Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.
Tayari Mwanyika amechukua likizo na anatarajiwa kustaafu mwezi ujao. Kwa upande wa Dk Hoseah na maafisa wengine wa serikali bado haijulikani ni hatua gani za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao kama Bunge lilivyoagiza katika maazimio yake.
Kustaafu kwa Mwakapugi kumetokea mapema, kwani awali Ofisa Uhusiano wa Wizara ya Nishati na Madini, Aloyce Tesha aliliambia gazeti hili kuwa, Mwakapugi yuko likizo na anatarajiwa kustaafu mwezi Januari mwakani atakapotimiza rasmi miaka 60.
"Yuko likizo, kwa kuwa alikuwa akihitajika sana ofisini, hivyo likizo zake alikuwa nazo na ndiyo amezichukua sasa hivi, anatarajiwa kustaafu mwezi Januari mwakani kisheria," alisema Tesha.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo imeeleza kuwa Rais Kikwete amefanya mabadiliko katika safu ya maofisa waandamizi wa serikali kwa kuteua makatibu wakuu wa wizara wanne wapya, kuhamisha wengine wawili na kuteua katibu mpya wa rais.
Katika taarifa hiyo, Luhanjo, alieleza kuwa Rais Kikwete amefanya mabadiliko hayo kufuatia kustaafu kwa baadhi ya makatibu wakuu wa wizara akiwemo Mwakapugi.
Tayri Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, ambao walijiuzulu uwaziri kutokana na taarifa ya kashfa hiyo, walishatoa maelezo yao bungeni na nje ya Bunge huku Karamagi akisema kama kuna ushahidi apelekwe mahakamani.
Tangu kusainiwa kwa mkataba wa Richmond Juni 23, 2006 na Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, wabunge wamegawanyika kutokana na baadhi kuunga mkono maazimio na wengine kupinga.
Mgawanyiko huo umesababisha kundi moja kujiita kuwa ni vinara wa mapambano dhidi ya ufisadi na jingine likipinga vita hiyo kwa madai kuwa inaichafua serikali ya CCM na chama chake.
Mbali na Ikulu kuridhia Mwakapugi kustaafu, taarifa yake iliyotolewa na Luhanjo imeeleza kuwa mabadiliko hayo yameanza jana Oktoba 19, 2009.
Luhanjo alisema kuwa pia, Rais Kikwete amemteua Sazi Salula kuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi wake, Salula alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa Rais Kikwete amemteua Mbarak M. Abdulwakil aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Abdulwakil anachukua nafasi ya Patrick Rutabanzibwa ambaye amehamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama Katibu Mkuu. Rutabanzibwa anachukua nafasi iliyoachwa na Salome Sijaona ambaye amestaafu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete pia amemteua Christopher Sayi kuwa Katibu Mkuu wa Wizata ya Maji na Umwagiliaji.
Kabla ya uteuzi wake, Sayi alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo hiyo, anachukua nafasi ya Wilson Mukama ambaye ameanza likizo ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Luhanjo alisema katika taarifa yake kuwa vile vile Rais Kikwete amemteua Sethi Kamuhanda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. Kabla ya uteuzi wake, Kamuhanda alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Anachukua nafasi Dk Florence Turuka ambaye anahamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kama Katibu Mkuu. Turuka anachukua nafasi ya Dk Naomi Katunzi ambaye anamaliza mkataba wake wa utumishi wa serikali mwezi ujao, Novemba, 2009.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi pia inaeleza kuwa Rais Kikwete amemteua Prosper Mbena kuwa Katibu wa Rais. Kabla ya uteuzi wake, Mbena alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, anachukua nafasi ya Jairo. |