Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::11/7/2009
Serikali yachochea hasira za wabunge kuhusu Richmond
Fredy Azzah na Habel Chidawali,Dodoma

SIKU moja baada ya mjadala wa Richmond kuahirishwa bungeni, baadhi ya wabunge wamesema serikali imechangia kuchelewesha suala hilo ili kukwepa fedheha na kuonya kwamba ujanja huo hautaisaidia.

Wakati wabunge wakitoa kauli hiyo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa wanajiandaa kuishtaki serikali kwa wananchi ili waihukumu kwa kuikumbatia Richmond.

Wabunge waliozungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili jana, walisema licha ya kuendelea kuupiga kalenda mjadala, bado wanaisubiri ripoti ya Richmond kwa hamu na kwamba hawatalala mpaka kieleweke.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, William Shellukindo alisema hajui kilichotokea hata ripoti hiyo ikaahirishwa tena.

"Siku mbili za mwisho sikuwa bungeni, niko nyumbani nimefiwa na mtoto wangu…, sijui kilichotokea mpaka waahirishe ripoti hiyo katika Bunge hili,” alisema Shellukindo.

Alipoulizwa kuwa kamati yake itafanya nini baada ya serikali kupiga chenga kuiwasilisha ripoti hiyo, Shellukindo alisema: "Bado niko kwenye msiba, sijafikiria cha kufanya".

Mmoja wa wajumbe wa kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza suala la Richmond, Lucas Selelii ambaye ni Mbunge wa Nzega alisema: "Hii ni chenga ya mwili ya serikali dhidi ya wabunge".

Hata hivyo, akatahadharisha kuwa kama serikali inaona kuna sababu za msingi kutoijadili ripoti hiyo bungeni ni bora wakawasiliana na kamati hiyo kuliko kuendelea kuwapiga chenga.

“Ni ajabu kuona ripoti hii inachukua muda mrefu bila kuwasilishwa bungeni ijadiliwe..., kama kuna sababu za kikatiba ama za kisera zinafanya kuwe na ugumu wa kuiwasilisha, ni bora serikali ikutane na kamati husika ieleze mambo hayo,” alisema Selelii.

Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM) alisema: “Tuko stranded (tumepigwa bumbuwazi)... wananchi hawatatuelewa kuhusu kuahirishwa kwa suala la Richmond na kwa kweli linazidi kutuchanganya”.

Jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema baada ya serikali kushindwa kuwasilisha taarifa ya Richmond bungeni sasa anakuja na mbinu mpya ya kuanzisha hoja nzito ndani ya Bunge.

 Dk Slaa alisema ana mbinu nyingi za kuanzisha vita ya ukombozi kwa wananchi wa Tanzania na kwamba amekuwa akiungwa mkono hata na wabunge wa CCM. Hata hivyo, alisema serikali imeamua kwa makusudi kuzima moto wa Richmond na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha kihuni.

 Mbunge huyo alionyesha wasiwasi wake kufuatia taarifa hiyo kutowasilishwa katika mkutano wa 17 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma na kusema kuwa hiyo ni chenga ya mwili kwa Watanzania.

Alisema haki ya Watanzania haitapatikana kupitia Bunge tu, kwani wabunge wameonekana kuwa si chochote mbele ya serikali.

“Jambo pekee litakalofanywa na Chadema ni kwenda kwa wananchi kwa sababu ndio mahakama kubwa kuliko zote,” alisema katibu huyo wa Chadema.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti alisema alitegemea serikali ingetoa taarifa kuhusu kilichotokea kwa sababu hata mpangilio wa ratiba ulikuwa ni wa kubalikabadilika.

Serikali ilishindwa mara mbili kuwasilisha ripoti hiyo kwa Kamati ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam kwa kutoa sababu mbalimbali; ikiwa ni pamoja na kutokuwepo nchini kwa Waziri William Ngeleja na aliporejea nchini waziri huyo aliwaambia waandishi kuwa wamekubaliana suala hilo lipelekwe moja kwa moja Dodoma.

Hata hivyo, suala la kuwasilishwa kwa hoja hiyo likawa kitendawili baada ya mkutano huo wa 17 kuanza baada ya kutojumuishwa kwenye shughuli za Bunge na iliripotiwa baadaye kuwa suala hilo lingerejeshwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini.

Miongoni mwa maazimio hayo 23 ni kuwajibishwa kwa Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah.

Akiahirisha shughuli za Bunge juzi, Spika Sitta alisema ripoti ya Richmond ilikuwa ijadiliwe pamoja na mambo mengine kwenye mkutano huo wa 17 wa Bunge, lakini haikuwezekana kwa sababu mbalimbali.

“Nasikitika kwamba, tumefikia muda wa kuahirisha mkutano huu wakati bado kuna viporo. Liko suala la ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Richmond, suala la mgodi wa Kiwira, suala la (Kampuni ya Reli) TRL na Ticts (kampuni inayoendesha kitengo cha makontena Bandari ya Dar es salaam),” Spika Sitta alilitaarifu Bunge jana.

Sitta alisema nia yake ilikuwa kuhakikisha suala la utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kuhusu Richmond lifikie mwisho katika mkutano huo, lakini jambo hilo limeshindikana.

Katika mkutano wa 16 baada ya hoja hiyo kupigwa chenga Spika alitaka serikali kujiandaa kikamilifu na kwamba, lazima ripoti hiyo ya utekelezaji iwasilishwe katika mkutano uliomalizika juzi.

Hata hivyo dalili zilionekana tangu awali kuwa suala hilo lisingemalizika katika mkutano huo, baada ya serikali kushindwa kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ndiyo inatakiwa iipitie kabla ya kupelekwa bungeni.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-