Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::11/23/2009
Karume: Waamuzi Serikali ya mseto Zanzibar ni nyinyi
Rais wa Zanzibar Dk Aman Abeid Karume akiwahutubia wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwenye uwanja wa demokrasia Kibandamaiti.

ATANGAZA AMANI YA KUDUMU IMEREJEA ZANZIBAR

Salma Said na Leon Bahati, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ametangaza rasmi kuzika uhasama wa kisiasa uliokuwepo kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), akisema suala la serikali ya mseto liko mikononi mwa wananchi.

Tamko hilo la Rais Karume limekuja siku chache baada ya katibu mkuu wa CUF, Seif Hamad Rashid kwenda Ikulu ya Zanzibar kuzungumza naye na baadaye kufanya kitendo cha kijasiri cha kuwatangazia wafuasi wake kuwa chama hicho kimeamua kumtambua Karume kuwa rais wa visiwa hivyo.

Tayari CUF imeshafanya mikutano miwili ya kuwataarifu wafuasi wake kuhusu uamuzi huo wa kumtambua Karume, ukiwemo mkutano wa kwanza ambao Maalim Seif alipingwa hadharani na jana ilikuwa zamu ya rais huyo kuwaeleza wafuasi wake wa CCM mjini hapa.

Akihutubia maelfu ya Wazanzibari waliofurika kwenye viwanja vya Demokrasia vilivyo mkoa wa Mjini Magharibi jana, Rais Karume alitangaza kwamba amani ya kudumu Zanzibar sasa imepatikana.

"Zamani magazeti yalikuwa yakiandika Zanzibar kunawaka moto, hakukaliki… sasa ndugu zangu amani ya kudumu imefika Zanzibar. Na hili tulikuwa tunalitafuta kwa muda mrefu sana," alisema Karume huku akishangiliwa na umati wa watu.

Katika hutuba hiyo ya jana, Rais Karume ambaye alianza kwa kueleza historia ndefu ya kisiasa na chimbuko la vyama vya siasa vya TANU na Afro Shiraz (ASP) ambavyo baadaye viliungana na kuunda CCM, aliwataka Wazanzibari wote kwa pamoja kupokea habari hizo njema kwa kuwa zina mustakabali mzuri wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Kwenye hutuba hiyo ambayo iliwasisimua wafuasi wa CCM na ambayo kila mara ikiwa ikikatizwa kwa kelele za shangwe na vigeregere, Karume hakugusia moja kwa moja kuhusu uundwaji wa serikali ya mseto Zanzibar.

Hata hivyo, alisema yuko tayari kulipokea suala la lolote lenye manufaa kwa Wazanzibari, lakini maamuzi hayo yaamuliwe na Wazanzibari wenyewe.

Alisema suala la serikali ya mseto halikuwa miongoni mwa mazungumzo baina yake na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad yaliofanyika Novemba 5 Ikulu Zanzibar.

Viongozi hao wawili wa vyama vinavyochuana vikali kisiasa visiwani hapa, walikutana Ikulu ya Zanzibar takriban wiki mbili zilizopita na siku chache baadaye Maalim Seif akatangaza kuwa CUF imeamua kumtambua Karume kuwa rais na kueleza mlolongo wa sababu za kufikia uamuzi huo.

Jana Rais Karume alisema Maalim Seif ndiye aliyemuomba wakutane na kwa kuwa CCM tayari walikuwa wameshawahi kutangaza kuwa milango ya Ikulu iko wazi na hivyo hakukuwa na kipingamizi.

Alisema baada ya Seif kufika Ikulu, hakumrubuni kwa namna yoyote ile ili wafikie maamuzi hayo na kwamba walichokubaliana kilitokana na utashi ambao tayari ulishafikiwa na baraza kuu la uongozi wa CUF na kushabihiana na msimamo wa CCM katika kuleta umoja.

"Nataka kufuta tetesi hizo ambazo zinazungumzwa mitaani kwamba Maalim Seif alipokuja nilimkaribisha chai ya maziwa. Ukweli ni kwamba yeye alikunywa glasi moja ya maji na mimi nikanywa pia glasi moja ya maji," alisema huku akishangiliwa na mashabiki wa CCM.

Alieleza kuwa Maalim Seif alimueleza katika mazungumzo yao kuwa baraza kuu la uongozi la CUF limeona hakuna haja ya kuendelea na mvutano kwa kuwa hauna maslahi na Zanzibar na badala yake linataka washirikiane katika maendeleo ya pamoja.

Akinukuu maneno aliyomwambia katibu huyo wa CUF, Rais Karume alisema: "Sasa umefika wakati ambao kama tumewakosea nyie, mtusamehe na kama nyinyi mmetukosea tuwasamehe... yaliopita si ndwele, tugange yajayo.

"Mimi pale pale nilimjibu nipo tayari kupokea kwa mikono miwili. Kwa sababu hata pale watu wanapokoseana husameheana… hii ni kwa sababu hata chama chetu tumekuwa tukihubiri mshikamano na amani."

Rais Karume alianza hutuba yake kwa kukitaka kikundi kimoja cha muziki kurejea wimbo mmoja unaosema: "Kukupenda wewe inawachoma" jambo ambalo lilitafsiriwa na watu kuwa kitendo cha yeye kukutana na Maalim Seif na kukubaliana kufuta tofauti zao hakikufurahisha baadhi ya watu.

Huku akishangiliwa na umati uliofurika uwanjani hapo, Karume alisema: "Huu sio tena wakati wa kununiana bali ni wakati wa kufurahi; sote tufurahi; katika siku ambayo nimerurahi, basi ni leo ."

Alisema CCM ina historia ndefu kwa kuwa ilizaliwa baada ya muungano wa ASP na TANU mwaka 1977 kwa lengo la kuwa na chama imara kitakachoongeza mshikamano, umoja, kasi na ari ya maendeleo kwa Watanzania wote.

Lakini alisisitiza kwamba TANU na ASP viliungana huku kila kimoja kikiwa na historia ya kushika bendera ya kuwakomboa wananchi na vyote vilikuwa na sera na ilani zake.

Alisema ilipofika mwaka 1992 CCM ilipoamua kuwa na mfumo wa vyama vingi ya siasa, ulikuwa ni uamuzi wa kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa.

Alisema kwa bahati mbaya chaguzi za Zanzibar za mwaka 1995, 2000 na 2005 zote zilisababisha misuguano kati ya CUF na CCM na kusababisha uhasama kwa Wazanzibari.

Alisema hali hiyo haikumfurahisha ingawa alisisitiza kwamba CCM ilishinda kwa kishindo katika chaguzi zote, lakini alifurahishwa na kitendo cha Seif kwenda Ikulu kumueleza kuhusu maridhiano.

Alimsifu Maalim Seif pamoja na CUF kwa uamuzi waliouchukua na hata ujasiri ambao aliuonesha katika mkutano wake wa kuwaeleza wana CUF, mkutano ambao katibu huyo wa CUF alipingwa waziwazi na wanachama.

"Halikuwa jambo rahisi hata kidogo kwenda kuwageuza watu ambao tayari walikuwa wanaelekea njia hii na kuwageuza kwenda njia nyingine. Kwa hili namsifu Maalim Seif kwa ujasiri aliouonyesha," alisema huku akishangiliwa kwa kupungiwa mikono juu.

Pamoja na kwamba katika mazungumzo yao hawakugusia suala la serikali ya mseto, Rais Karume alisema amefungua milango ya mazungumzo kwa kuwa kila jambo linazungumzika.

Lakini alisema kuwa suala lolote watakalolizungumza litatekelezwa pale wananchi watakapoliridhia.

"Suala lolote litakalozungumzwa lina waamuzi wake! Na waamuzi wenyewe ni nyinyi wananchi," alisema jambo ambalo lilitafsiriwa kuwa litategemea maamuzi ya wafuasi wa vyama hivyo.

Mkutano wa jana umefanyika wakati tayari CUF imeshafanya mikutano miwili ya hadhara kwa ajili ya kuwajulisha wafuasi wao kuhusu uamuzi wa kumtambua Rais Karume.

Chimbuko la CUF kutotambuliwa Rais Karume ni kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi wa rais wa 2005 ikidai kuwa mgombea wake, Maalim Seif alishinda.

Juhudi za vyama hivyo kutafuta muafaka tangu wakati huo hazijafanikiwa baada ya CUF kutangaza kujitoa katika mazungumzo kwa madai kuwa CCM ilipindisha mambo iliposema kuwa suala hilo lirejeshwe kwa wananchi, wakati CUF ilishawatangazia wafuasi wake kuwa wamekubaliana kuunda serikali ya mseto.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-