Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::11/19/2008
Bandari mpya iwe fursa ya kukuza uchumi wa Zbar
Bandari mpya iwe fursa ya kukuza uchumi wa Zbar

Na Ally Saleh

HABARI njema zilivuma wiki hii zikisema kuwa baada ya subira ya muda mrefu hatimaye bandari ya Zanzibar imekamilika na kuwa iko njiani kuanza kazi kwa kiwango chake kikamilifu.

Kila Mzanzibari atafurahia habari hii maana kila mtu anajua kuwa kitovu cha uchumi wa Zanzibar ni bandari na mchango wake tunaweza kusema haumithiliki kuanzia zama hizo hadi leo.

Kwa wengi wasiojua bandari ya Zanzibar ilikuwa na umuhimu mkubwa katika eneo hili la Bahari ya Hindi kwa kuwa ilikuwa ni kituo kikubwa cha kutia nanga meli zilizokuwa zikitoka chini ya Afrika kutokea Marekani na juu ya Afrika kutoka Asia na hata Ulaya.

Zanzibar ilikuwa ikitawala ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki kutoka chini ya Somalia mpaka Sofala, Mozambique, ilihitaji

bandari yenye uwezo na haiba.

Mwaka 1892 ilitangazwa nia ya kuifanya Zanzibar

Bandari Huru wazo ambalo halikuwahi kutimizwa kikamilifu na hata baada ya nia hiyo kusisitizwa upya katika miaka ya hivi karibuni basi bado imekuwa ni ndoto.

Kwa maumbile yake ya visiwa bandari ina nafasi maalum katika uchumi, hilo halina shaka yoyote ile. Na kwa hivyo uhai na uzima wa bandari unamgusa kila mtu hapa kwetu.

Ndio maana bandari ilipokuwa inaugua uchumi wa Zanzibar na watu wake walikuwa wanaugua. Ndio maana wakati mivutano ya kisiasa ilipokuwa ikirindima na kukawiza ufadhili wa mradi huo uchumi wa Zanzibar uliumwa nawatu wake waliumwa.

Na pia wakati mvutano uliotokea kuhusu aina ya ujenzi wa bandari hiyo, uchumi wa Zanzibar uliumwa na watu wake waliugua.

Lakini wengi tumekuwa tunajiuliza katika mazingira tuliyonayo au ambayo tunalazimishwa kuishi nayo ni rahisi kiasi gani ujenzi mpya wa bandari hiyo kuwa na faida kwa uchumi wa Zanzibar?

Hapa ni maana mbili. Moja ni ile ya mfumo mzima unaozunguka suala la faida ya ushuru unaoweza kutokana na harakati za bandari hiyo kuingiza na kutoa bidhaa, ambalo hili liko nje ya uwezo au utawala wa Serikali ya Zanzibar kwa upande fulani.

Na maana ya pili ni uwezo ulio ndani wa menejimenti ya bandari hiyo kusimamia na kuwa tayari kivifaa na kitaalamu ili kazi za bandari hiyo ziwe na natija ambayo umma wa Kizanzibari unatarajia kimapato na kiajira?

Kwa sasa bandari ya Zanzibar inafanya kazi katika hali ya ushindani mkubwa. Ushindani nje ya Tanzania dhidi ya bandari ya Mombasa na upinzani ndani ya Tanzania dhidi ya bandari ya Tanga lakini hasa Dar es Salaam na hatua zikianza kuchukuliwa kuiwezesha zaidi ile ya Mtwara.

Hata dhana ya kuwa na bandari huru inapanuliwa pia. Taarifa zinasema Kigoma inasukumwa iwe na hadhi hiyo na hivi karibuni tumeambiwa pia Dodoma pia inaweza kufanywa kuwa na hadhi hiyo ili kushika biashara inayokwenda katika nchi jirani ambazo kwa jumla ni tisa na vunge kubwa la kibiashara kwa Tanzania, lakini fursa hiyo ikiwa bado haijarutumiwa vyema au kikamilifu.

Mbali ya Zanzibar kutengezewa zengwe la ushindani lakini pia kuna suala zima la mfumo wa kodi. Hapa kuna "Ziraili" wa uchumi wa Zanzibar, yaani Mamlaka ya Kodi ya Tanzania (TRA). Kwa hali ilivyo sasa na mipango tunayosikia inazidi kutayarishwa, mikono ya taasisi hiyo itazidi kutopea katika roho ya uchumi wa Zanzibar.

Wengi tunajua jinsi wafanyabiashara kadhaa walivyoamua kuisusa bandari ya Zanzibar na kuhamishia uingizaji wa biashara zao moja kwa moja bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa wanatozwa mara mbili kwa kisingizio cha Zanzibar wanatozwa kiwango kidogo cha kodi.

Sote tunajua athari ya hili. Iwapo wafanyabiashara watapeleka bidhaa zao moja kwa moja Dar es salam ni wazi kuwa TRA itapata kodi yake, lakini itakuwa ni hasara ya Zanzibar maana Bodi ya Mapato ya Zanzibar itakosa kukusanya kodi za ndani na hivyo kutia pengo katika makusanyo ya Zanzibar na kuathiri bajeti na uchumi.

Kwa juhudi zozote zitazofanywa kuimarisha bandari ya Zanzibar kwa maana ya kuongeza uwezo wake wa kupokea na kutoa bidhaa, lakini hilo halitokuwa na baada iwapo Serikali ya Zanzibar haitochukua hatua madhubuti kabisa itayohakikisha kuwa mfumo mzima wa kodi unapitiwa upya kwa kudai kutizamwa upya sheria iliyounda Mamlaka ya Mapato ya Tanzania TRA.

Kwa upande wa pili, kama nilivyotangulia kusema ni uwezo na ubunifu wa menejimenti ya ndani kusimamia operesheni za bandari hiyo ambayo bado hadi leo inavutia kiasi kikubwa cha mizigo kinachoingia hapa, lakini kwa baadhi yetu inatia shaka iwapo tunatumia uwezo wa bandari hiyo kikamilifu.

Lazima tukubali ukweli kuwa hizi ni zama mpya. Ni mpya kisayansi na kiteknolojia na ni mpya kifikra na kibunifu.

Na kwa hivyo ni lazima bodi yenye kusimamia taasisi kama ya bandari ambayo inameza yote mawili ya sayansi na teknolojia na fikra upya na ubunifu ionyeshe sura kama hiyo.

Leo tena si wakati wa kuwachagua "Pandu na Jecha," kuingia katika bodi kama hizo kwa kulipa hisani za kisiasa au kutafutiana nafasi za ulaji.

Pili ni muhimu kuwa na menejimenti ambayo inajua nini inakifanya. Menejimenti ambayo inaweza kumudu kila hatua ya operesheni zinazohusika katika bandari hiyo.

Kuweza kuwa na mipango na taratibu za kitaalamu na sio kazi kufanywa kwa njia ya kukikisa na kubahatisha. Kazi zisitolewe kwa hisia za kisiasa na vyeo vitolewe kwa uwezo.

Bandari kwa sasa, ni jambo ambalo sio siri, ina uhaba mkubwa wa vifaa vya kupakulia mizigo. Hii ni dhambi kubwa katika bandari yoyote ile duniani.

Siri ya bandari nzuri ni vifaa vya kupakulia ambavyo sio tu vinahakikisha usalama lakini pia vinahakikisha uharaka wa mizigo kushushwa na ndio siri ya mafanikio ya bandari yoyote ile iwe ni Singapore, Mombasa au Zanzibar.

Kila mwenye meli na mzigo anataka shehena yake ishuke haraka, kwa salama na ihifadhiwe pahala pema. Mzigo ukishuka kwa haraka unaokoa muda wa meli kukaabandarini au nangani kwa muda mrefu, lakini hali hiyo siyo ilivyo bandari ya hapa Zanzibar.

Mzigo ukishuka haraka pia ni nafuu kwa mwenye shehena maana mzunguko wake wa fedha unazidishwa kasi yake na mzigo ukihifadhiwa palipo pazuri ndipo sifa ya bandari inapokuja juu na watu wengi zaidi kutaka kuitumia.

Sasa hivi kazi zinazopatikana bandarini kwetu hazitoshi umma unaosubiri kibarua ambao hufika kila siku maeneo ya bandarini. Juhudi lazima ichukuliwe kuwezesha ajira zaidi kutengenezwa kuweza kuwasaidia watu zaidi na njia

pekee ya kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi ili mizigo mingi zaidi iweze kushushwa kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi.

Ingawa kuimarika kwa vifaa kutamaanisha watu wachache wataopata kazi ya kibega, lakini pia itamaanisha fursa nyingi zaidi za watu wengine kupata kazi kwa maana ya kuongezeka kiwango cha mizigo itakayokuwa inapakuliwa kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi.

Tusisahau pia kumalizika kwa ukarabati wa bandari hiyo kutaongeza pia idadi ya wasafiri wanaopita katika bandari hiyo na hivyo kuchangia katika sekta ya utalii wa nje na wa ndani mbali ya kuwa abiria nao pia hufanya biashara na sekta hiyo pia kuweza kuimarika.

Makala hii madhumuni yake ni kukumbusha kuwa tusifurahi kwa kuwa ukarabati wa bandari hiyo umeweza kukamilika. Lakini tufurahi zaidi kuwa bandari hiyo itakuwa na fursa bora zaidi ya kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuongeza mapato

serikalini na kupatia ajira zaidi wananchi.

Lakini kwa hali ilivyo sasa haitii moyo sana. Lazima Zanzibar ipiganie kuleta mabadiliko katika sheria ya TRA kuvua minyororo ya "utumwa mpya wa kiuchumi".

Ila zaidi yake bandari ya Zanzibar inahitaji msukumo mpya, fikra

mpya na hasa vifaa vipya bila ya vitu hivyo tutakuwa tumekarabatiwa bandari lakini tutabakia pale pale pa kijungumeko.

+255 777 4300 22

www.eternaltourszanzibar.net

jumbamaro.blogspot.com

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-