...Halafu tunajifanya tunashtuka

Muktasari:

Ni kawaida kifimbo hicho kukimbizwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na hupokewa na wakuu wa mataifa husika.

Aprili 2017, Kifimbo cha Malkia, wa Uingereza, Queen’s Baton kinatarajiwa kuwasili nchini na kupokewa na Rais John Magufuli.

Ni kawaida kifimbo hicho kukimbizwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na hupokewa na wakuu wa mataifa husika.

Ujio wa kifimbo hicho ni kiashiria cha uzinduzi wa Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2018 itakayofanyika kwenye mji wa Gold Coast, Australia.

Michezo hii hushirikisha mataifa mbalimbali duniani yaliyokuwa chini ya utawala wa Waingereza.

Tanzania ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Madola, itakuwa miongoni mwa mataifa ambayo kifimbo hicho kitakimbizwa katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Wanamichezo mashuhuri hapa nchini ni miongoni mwa wanaotarajiwa kukimbiza kifimbo hicho, ambacho msimu uliopitwa kilipokewa na Rais aliyemaliza muda wake, Jakaya Kikwete kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.

Japo msimu uliopita, Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa bega kwa bega na tasnia ya michezo na iliagiza tufanye vizuri kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika New Zealand, ikiwamo Rais wa nchi wa wakati huo kuikabidhi timu bendera kama moja ya kuwapa hamasa, lakini mambo yalikwenda tofauti kabisa.

Ujio wa kifimbo hicho ni kiashiria kuwa Michezo ya Madola inayotarajiwa kuzinduliwa Machi 13, 2017 huko Buckingham Palace inaanza.

Kila baada ya miaka minne, kifimbo huja Tanzania katika moja ya safari zake za kuzunguka mataifa yaliyokuwa makoloni ya Uingereza.

Ujumbe mbalimbali hutolewa, hamasa mbalimbali hutolewa, maonyo na mengine mengi kwa wanamichezo na wadau wa michezo nchini.

Ninachokiangalia hapa, tumeshaambiwa kuwa kifimbo cha Malkia kinakuja na maana yake ni kwamba Michezo ya Jumuiya ya Madola inakuja, sasa tunafanya nini?

Ndiyo maana nikasema halafu tunajifanya tunashtuka, kwa maana ya kwamba hapa tumeisikia hiyo, lakini hakuna anayejali, hakuna anayehangaika na maandalizi na mwishowe tunajikusanyakusanya alimradi tu twende nasi tuweke saini kuwa Michezo ya Australia Tanzania na wanamichezo wake na wao walikuwapo.

Vyama vyenye Michezo ya Madola ambavyo ni sawa na Olimpiki na ile ya Afrika, wakae chini waone ni namna gani ya kupeleka wanamichezo walioiva huko.

Kuna waogeleaji wakiongozwa na Hilal Hilal pamoja na Sonia Tumiotto, Celina Itatiro, Smriti Gorkarn na Vansh Ladwa katika riadha kuna Andrew Simbu aliyeshjika nafasi ya tano kwenye Olimpiki sasa tukiwaandaa hawa kwa umakini, watakuja na medali za dhahabu, ninaamini.

Wapo wanamichezo wengi na wao wakiandaliwa mapema, ninaamini wakienda Gold Coast, Australia 2018, watakuwa na historia nyingine kwa Tanzania.

Ninachokiona ni nafasi ya Waziri wa Habari na mwenye dhamana ya michezo, Nape Nnauye kukaa chini na watu wake kuangalia nini cha kufanya kuwaweka sawa viongozi, uongozi wa vyama vya michezo na wanamichezo.

Ifahamiken nani na nani wanafuzu kwa michezo hiyo, kama viwango vianze kutafutwa sasa mwaka 2018 si mbali.

Kinachoshangaza, Kenya ambao ni jirani pua na mdomo wanafanya vizuri lakini sisi kila siku tunasema tunajiweka sawa, tunajiandaa au utasikia maandalizi hayakuwa mazuri, kinachokera zaidi, kama mlijua maandalizi hayo, mlifuata nini mashindanoni au ndiyo posho?

Ukweli ‘tumemiss’ kujaa uwanja wa ndege na kujipanga barabarani kuwalaki wanamichezo wakirudi kishujaa.

Hebu badilisheni gia, isifanywe kushindwa kama ni mazoea.

Ujio wa Kifimbo cha Malkia uwe chachu ya maandalizi ya Madola, na mjue 2018 si mbali.