‘Bravo’ JK kukemea uonevu wa polisi

Muktasari:

Kukerwa kwa Rais Kikwete kuliongezeka pale alipoona juhudi zake za kuwataka polisi kuacha kuwabugudhi wananchi kushindikana, hadi alipofikia kutamka “Jamani waacheni waje kwa nini mnawapiga? Mbona hamsikii? Kova hebu waambie askari wako wawaache kuwasumbua.” Kwanza tuwashangae polisi kwa kitendo chao cha kuwapiga wananchi, kwa kuwa Rais Kikwete ndiye aliamua kuwafuata kwenye maeneo yao baada ya kusikia wameathirika na mvua.

Jana gazeti hili lilikuwa na habari iliyosema ‘JK akerwa polisi kubughudhi wananchi’. Habari hiyo ilikuwa ikielezea namna Rais Jakaya Kikwete alivyokerwa waziwazi na kitendo cha polisi kuwazonga na kuwasukuma wananchi waliokusanyika eneo la Jangwani, Dar es Salaam kumsikiliza.

Kukerwa kwa Rais Kikwete kuliongezeka pale alipoona juhudi zake za kuwataka polisi kuacha kuwabugudhi wananchi kushindikana, hadi alipofikia kutamka “Jamani waacheni waje kwa nini mnawapiga? Mbona hamsikii? Kova hebu waambie askari wako wawaache kuwasumbua.” Kwanza tuwashangae polisi kwa kitendo chao cha kuwapiga wananchi, kwa kuwa Rais Kikwete ndiye aliamua kuwafuata kwenye maeneo yao baada ya kusikia wameathirika na mvua.

Tunawashangaa polisi kwa sababu Rais ni mwanasiasa na mtaji wa wanasiasa ni wananchi, kitendo chao cha kuthubutu kunyanyua rungu kuwapiga wananchi mbele ya kiongozi wao waliyemchagua kidemokrasia na hadi kufikia hatua mwenyewe kukasirika, kunaonyesha jinsi polisi walivyopitiliza kwa uonevu.

Kwa muda mrefu ripoti nyingi za haki za binadamu zimekuwa zikilalamikia Jeshi la Polisi kwa uonevu, rushwa, mauaji ya raia na unyanyasaji. Mfano, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika taarifa yake kuhusu tukio la Januari 27 la polisi kuwapiga wafuasi wa CUF, huko Mbagala Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, ilisema ni kitendo kilichoashiria uvunjifu wa haki za binadamu.

Mfano mwingine ni ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi. LHRC ilisema tukio hilo ni uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Uonevu dhidi ya raia na wanasiasa unaofanywa na polisi ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948, Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa wa 1966 na Mkataba wa Mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu wa 1981.

Tunamshukuru Rais Kikwete kwa kutofumbia macho uonevu huo, tena uliokuwa ukifanywa bila soni na mbele ya macho yake. Pia, turudishe kumbukumbu nyuma kwa Rais kwamba uonevu huu umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu bila hatua stahiki kuchukuliwa kwa wahusika. Kuna baadhi ya makamanda wa polisi ambao wamehusishwa na uonevu huo lakini badala ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu wameishia kupandishwa vyeo, kuhamishwa maeneo ya kazi na hata kupongezwa kwa kazi nzuri.

Sisi tunasema kwa kuwa Rais ameshuhudia kwa macho yake, ni wakati sasa wa kuchukulia hatua stahiki, tunaamini bado hajachelewa kukomesha vitendo hivi kwa kuwa nchi inakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, polisi watatumika kuonea watu. Hivyo, tunaamini kama hatua zitachukuliwa sasa inaweza kuwa kinga na kuufanya uchaguzi kuwa wa amani na utulivu.

Tunasema hivyo kwa sababu siku za karibuni tumeshuhudia malumbano kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu wimbi la uanzishaji wa vikundi vya ukakamvu vya vijana vyenye mwelekeo wa kijeshi. Tunaamini iwapo Rais Kikwete atachukua hatua stahiki huenda akarejesha imani ya wananchi kwa polisi.