Mafaniko ya biashara yako hutegemea jina lake

Muktasari:

  • Katika kufanya utafiti ndani na nje ya nchi, biashara nyingi zinapata changamoto sokoni kutokana na majina zinayotumia. Jina linalokuwa na maana mbili kwa mteja linapotosha na kupoteza uhalisia wa mtoa huduma.

Jina la biashara ni utambulisho wa msingi sana na kila mwenye wazo kinachofuata ni kupata jina sahihi lenye kukidhi hadhi na kuakisi kile anachouza kwa wateja wake.

Katika kufanya utafiti ndani na nje ya nchi, biashara nyingi zinapata changamoto sokoni kutokana na majina zinayotumia. Jina linalokuwa na maana mbili kwa mteja linapotosha na kupoteza uhalisia wa mtoa huduma.

Licha ya mgogoro unaoweza kujitokeza kutokana na maana ya jina la biashara kufanana na jina la biashara nyingine huwachanganya wateja.

Mfanyabiashara anatakiwa kuepuka jina gumu au lenye lugha tatanishi kuutambulisha mradi wake.

Ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa mkanganyiko wa aina yoyote jina la biashara lilenge mteja na soko husika.Hakuna ulazima wa kutumia lugha ya kigeni kwani huweza kumchanganya mteja.

Mteja anatakiwa kuwa sehemu ya jina la bidhaa, sasa asipoelewa ama vinginevyo inakuwa ngumu kwake kufanikisha kutengeneza uhusiano wa kihisia na bidhaa zako.

Kwa mfanyabiashara yeyote lazima azingatie lugha anayoitumia kwa wateja wake kwa kutumia lugha anayoielewa vizuri na kwa ufasaha. Jina la biashara yako halipaswi kufafanuliwa.

Jina la biashara lazima liwe na maana moja kwa mteja ili asitafute muda wa kuwaza unachomaanisha. Mfanyabiashara unaweza kutumia jina kwenye bidhaa au huduma, lakini likawa na maana tofauti kwa kabila au jamii fulani na mwisho wake wateja kutopenda kuzinunua.

Kabla ya kuchagua jina lazima ulifanyie utafiti kujua kama soko litalielewa kama ilivyokusudiwa.

Jina la biashara linatakiwa kuwa fupi ili mteja au aweze kulishika na kulikumbuka haraka. Mwisho wa siku mtu huyu ni balozi wako wa hiari kwani anakumbuka na kuweza kulitaja mbele ya wenzake pale anapotokea mwingine anayehitaji bidhaa au huduma kama yako. Jina limfanye mteja alikumbuke kwa urahisi lililo rahisi.

Mfanyabiashara anatakiwa kutambua kuwa jina la biashara lazima liakisi kile anachofanya. Kuna baadhi ya watu wanafanya biashara ya chakula lakini kwa majina yanayoendana na spea za magari.

Kuna umuhimu wa kuwa na jina linaloakisi biashara, kama unafanya biashara ya chakula basi liwe la mrengo huo ili mteja akilisikia kwa mara ya kwanza ajue ni biashara ya chakula na si vinginevyo.

Hata kama mmiliki ni mwanasisasa, jina la biashara lisiwe na mrengo wowote wa kisiasa au kidini kwani madhara yake ni kuwakosa wateja wenye imani au itikadi tofauti.

Kundi jingine la wateja unaoweza kuwakosa ni wale wasio mashabiki wa itikadi au imani. Ni muhimu kuzingatia hili kwa kuweka jina lenye kuwafaa watu wote bila kujali imani au itikadi za kisiasa na kukubalika kwa makabila yote.

Jina lisilo na mrengo wala mtazamo wa aina yoyote hukusaidia kuwashinda wateja kihisia na kujiona ni sehemu ya biashara au huduma yako.

Msingi mkuu wa jina la biashara au bidhaa yako ni kuleta usawa wa kihisia kati ya mteja na bidhaa yenyewe. Mteja lazima ahisi bidhaa au huduma husika ni kwa ajili yake.

Kwa kuwa na jina linalokidhi mahitaji ya mteja lisilompa karaha za kihisia na kuona huduma ni kwa ajili yake, mteja hukosa namna ya kuiepuka biashara yako.

Wito wangu kwa wajasiriamali, ajenda ya uchumi wa viwanda unatupeleka kwenye ushindani mkubwa unaohitaji bidhaa zenye thamani sokoni siyo zinazosambazwa.

Lazima tujiandae na mabadiliko ya ulimwengu wa ushindani. Ukiwa na jina linalokidhi haja na matakwa ya mlaji litakubalika kirahisi na kupunguza ushindani sokoni.