Mchango wa vijana unahitajika katika uchambuzi wa bajeti

Muktasari:

Kabla ya kutangaza bajeti mpya, Serikali hupitia utekelezaji wa mpango wa mwaka wa fedha uliomalizika ikiwamo mapato na matumizi yake.

Bajeti ya Serikali ni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha ambao huanza rasmi Julai mosi.

Kabla ya kutangaza bajeti mpya, Serikali hupitia utekelezaji wa mpango wa mwaka wa fedha uliomalizika ikiwamo mapato na matumizi yake.

Baada ya mapitio hayo huwasilisha mpango wa mwaka wa fedha unaofuata na bajeti yake ikiwa ni pamoja na makadirio na mapato.

Pia, huonyesha maeneo ambayo fedha za bajeti mpya zitakakotoka ikiwa ni vyanzo vya ndani na nje ya nchi, vya kodi na visivyokuwa vya kodi.

Si hivyo tu, ni pamoja na mikopo yenye masharti nafuu, na fedha kutoka kwa wafadhili, mikopo ya kibiashara na huonyesha fedha zitakavyotumika katika maeneo gani kugharamia huduma na bidhaa za umma, ikilenga zaidi shughuli za maendeleo.

Haya yote hufanyika kwa uwazi ili kuwapa fursa wananchi ya kutambua wizara gani imepangiwa kiasi gani na kwa sababu gani na zitatumika kufanya nini na kwa wakati gani.

Jukumu la wananchi, hususan ninaozungumza nao hapa, yaani vijana, ni kuhakikisha wanafuatilia kwa kina ili kuhoji wanapoona hapajakaa sawa.

Wiki hii Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh898.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Bajeti hii pekee inaweza kuibua mjadala mkubwa kwa vijana kwa kuchambua vipengele mbalimbali vilivyomo, kama fedha iliyotengwa.

Kwa mujibu wa wadau na wachambuzi wa bajeti inaonyesha sehemu ya fedha zinazotamkwa kwenye bajeti hazipatikani kama ilivyopangwa.

Badala yake hutokea zaidi ya nusu au robo yake kupatikana, jambo linalokwamisha utekelezaji wa baadhi ya shughuli za wizara husika.

Kwa mfano kwa Wizara ya Afya, fedha halisi iliyotolewa kwa ajili ya kununulia dawa hadi kufikia Februari kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni asilimia 23 ya fedha yote iliyopangwa kutolewa.

Uchambuzi unaonyesha kiasi hicho cha fedha ni kidogo ukilinganisha na asilimia 54 ya fedha iliyotolewa kwa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2016/17.

Hapa ndipo panahitaji mjadala mpana. Hii ni wizara moja pekee, zipo nyingi ambazo huenda zikiwasilisha bajeti zake zitakuwa na tatizo katika utekelezaji kwa kutopata bajeti yote. Hivyo, kwa kijana anayefuatilia atalibaini hilo mapema na kuhoji, kuainisha maeneo yatakayoathirika na upungufu wa fedha.

Katika kuchambua bajeti yapo mambo mengi ya kuangalia ikiwamo mikataba ya kimataifa ambayo nchi imetia saini na namna inavyotekelezwa.

Kwa mfano katika Wizara ya Afya utekelezaji wa bajeti yake unatakiwa uzingatie mkataba wa Abuja ambao umetoa maelekezo ya nini kifanyike.

Mkataba huo ambao Serikali iliusaini mwaka 2001 unazitaka serikali za nchi kutenga asilimia 15 ya Pato la Taifa (GDP) kwa ajili ya afya.

Hivyo kwa kufuata vipengele mbalimbali vilivyomo ndani ya mkataba huo kunaweza kuwa mwongozo wa uchambuzi wa bajeti hiyo.

Nasisitiza kila wizara ina mwongozo wa upangaji na utekelezaji wa bajeti yake, hivyo wakati wa kufanya uchambuzi huo utakuwa ni mwongozo wa kuhoji na kukosoa.

Kijana kumbuka Taifa linakutegemea na familia yako inakutegemea. Kuwa makini, chukua hatua, usichoke kuhoji kuhusu maendeleo ya Taifa lako.