Tumuunge mkono Rais ulinzi wa rasilimali za Taifa

Muktasari:

Haikuwa hivyo wamedhihirisha ukweli mchungu ambao baadhi ya Watanzania wenzetu wasingependa uwekwe hadharani.

Jana  Rais John Magufuli alipokea ripoti kuhusu madini ya almasi na Tanzanite, iliyoonyesha kuwapo kwa dosari zinazosababisha nchi kupoteza mapato mengi.

Ripoti hiyo inatokana na kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuangalia mfumo wa uchimbaji, udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini hayo.

Kama tulivyoripoti katika taarifa tuliyochapisha jana gazetini, hii ni ripoti  inayoonyesha hali ya kusikitisha kuhusu wizi unaofanywa nchini katika sekta ya madini na kibaya zaidi wizi huo ukiwa na baraka kutoka kwa Watanzania wenzetu waliopewa jukumu la kusimamia maliasili za Taifa.

Kilichoibuliwa na kamati za Bunge kinaandika historia mpya katika Taifa letu. Kwa namna ufisadi ulivyokubuhu katika sekta ya madini, ingewezekana wajumbe wa kamati wangepindisha ukweli wa waliyoyabaini. Haikuwa hivyo wamedhihirisha ukweli mchungu ambao baadhi ya Watanzania wenzetu wasingependa uwekwe hadharani.

Tunapowapongeza wanakamati kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa, tunalazimika pia kumpongeza Rais kwa hatua ambazo amekuwa akichukua katika siku za karibuni za kupambana na watu wanaohujumu sekta ya madini.

Kama ambavyo amekuwa akisema mara kwa mara nchi yetu sasa  iko katika vita vikali vya kupambana na ‘mabaradhuli’ wa ndani na wa nje  ambao kwa muda mrefu waliigeuza nchi yetu kama mahala rahisi pa kuchuma.

Tukubali tumefanya makosa, lakini kwa kupitia Serikali ya Awamu ya Tano, Watanzania katika kila ngazi tunapaswa kuamka na kuzilinda rasilimali zetu ili zitunufaishe sisi na vizazi vijavyo.

 Tusirudie makosa yaliyokwishafanywa na baadhi yetu waliokosa uzalendo kwa nchi yao na hata kukosa huruma kwa wananchi ambao kama Rais anavyosema wamekuwa wakikosa huduma nyingi kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Ili tusirudi tulipotoka, tumewasikia viongozi wakiagiza kupitiwa kwa sheria zetu kama moja ya mikakati ya kupambana na vita hii. Lakini tunapopotia upya sheria zetu na hata kuzibadili, mchakato huu uende sambamba na upitiaji upya wa mikataba yote  katika sekta ya madini, ili kubaini ile isiyokuwa na tija kwa Taifa na hatimaye kutafutwa njia sahihi ya kuachana nayo.

Kwa muda mrefu, kilio cha Watanzania wengi  kimekuwa ni usiri wa mikataba hasa inayohusu maliasili muhimu kama madini. Kama viongozi wakuu wa nchi wanakiri kuwa tumedhulumiwa na kuibiwa kwa muda mrefu, wakubali pamoja na mikakati mingine kuweka utaratibu wa mikataba ya Taifa kuwa mali ya umma  na si mali  ya watu wachache serikalini. Kuanzia sasa tunapendekeza mikataba yote ipelekwe bungeni na kuridhiwa na wawakilishi wa wananchi.

Kamati hizi mbili za Bunge na zile za awali zilizoundwa na Rais kuhusu mchanga wa dhahabu, ni dalili tosha kuwa Serikali imeamua kwa dhati kuikomboa nchi kutoka kwenye mikono ya Watanzania walafi wanaoshirikiana na wageni kuifilisi nchi.

Tunaunga mkono jitihada za Serikali hii ambayo  kwa hakika imeshajipambanua vya kutosha kwa dhamira yake ya kulinda mali za Taifa.

Wakati wa kuzuia wizi wa mali za nchi yetu ni sasa, wakati wa kuona maliasili zikinufaisha nchi ni sasa, Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana kama tutajipanga kuziba mianya yote inayotoa fursa kwa watu wachache kunufaika kwa migongo ya Watanzania wengi.