Monday, July 17, 2017

ZFA, malizeni changamoto kabla ya Fifa

Katikati ya wiki iliyopita, Mbunge wa Malindi na wakala wa soka anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Ally Saleh alitoa kauli kupinga hatua zinazofanyika kuhakikisha Zanzibar inapata uanachama wa shirikisho hilo.

Saleh alikuwa mjumbe kwenye jopo lililokwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa ajili ya kuiombea Zanzibar uanachama wa shirikisho hilo.

Baada ya baada ya kupewa uanachama wa CAF katika mkutano mkuu uliofanyika Machi huko Addis Ababa nchini Ethiopia, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alithibitisha kuwasilisha ombi la kutaka Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa Fifa.

Katika mahojiano na gazeti hili, Saleh alisema hakuna ulazima wa kukimbilia kuomba uanachama wa Fifa, bali kuweka mikakati ya kushughulikia changamoto zinazoukabili mchezo huo Zanzibar.

Pamoja na nia njema ya kutaka kuwa mwanachama kamili wa Fifa, kuna kila sababu ya kujitafakari kuona jinsi gani ya kujipanga kwa uanachama uliotangulia wa CAF kabla ya kuufikia ule wa Fifa.

Kinachotakiwa ni Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kuhakikisha kinatumia fursa ya CAF kuinua soka la visiwa hivyo.

ZFA na wadau wangejipa kwanza  ajili ya mpango mkakati wa muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu wa jinsi gani ya kuinua soka ya Zanzibar hasa baada ya hatua hii kubwa ya kupata uanachama wa CAF. Tunadhani kwamba ingependeza kuanza kutumia matunda ya uanachama huo kujipanga kabla ya kuanza hatua nyingine kubwa zaidi.

Kimsingi kuna changamoto nyingi katika mchezo wa mpira wa mifii Zanzibat ikiwamo ya uendeshaji wa ligi zake iwamo ile kubwa ya ligi kuu.

Ligi hiyo na hata za chini imekosa msisimko na hamasa kiasi kwamba haitoi timu na wachezaji wenye ushindani ndani na nje ya Tanzania kama ilivyokuwa miaka ya 1980 na 1990.

Timu nyingi za Zanzibar hivi sasa hazina uwezo wa kutoa ushindani wa dhati katika mashindano ya klabu Afrika, zimekuwa zikitolewa mara kwa mara katika hatua za awali na ni nadra kufika hatua ya kwanza au pili na tatu.

Wengi wetu tunakumbuka jinsi timu ya Taifa ya Zanzibar ilivyokuwa ikitamba Afrika Mashariki na Kati enzi zile za Small Simba, Malindi, Mlandege, Black Fighters, KMKM ambazo baadhi zipo lakini hoi, na nyingine zimepotea katika ulimwengu wa soka.

Moja ya sababu za kukosekana msisimko na hamasa ni ufadhili. Baada ya kupata uanachama wa CAF, tunadhani kwamba sasa ni wakati muafaka kwa ZFA na wadau kutafuta njia ya kutengeneza wadhamini na wafadhili na zaidi ili kuleta hamasa na msisimko na kuirejesha Zanzibar katika ubora ule wa zamani.

Ni wakati pia wa kuangalia miundo ya uendeshaji wa soka la vijana, ujenzi wa viwanja vya kisasa vya kati kwa timu pamoja na kuwa na akademi za kukuzia vijana.

Tuonavyo, hakuna haja ya kukimbilia Fifa kutaka uanachama kabla ya kutengeneza msingi wa soka ya Zanzibar.

Pamoja na kwamba Fifa kuna misaada kwa  ajili ya maendeleo ya soka, lakini ingependeza kama ZFA ingepambana kutengeneza mfumo yake na kuwa imara kwanza.

Ijipange na iweke utaratibu wa kuendesha soka ili hata misaada ya Fifa itakapokuja baada ya kupata uanachama, iwe na mwendelezo mzuri.

-->