Athari za Trump kwa uchumi wa Marekani na dunia

Muktasari:

  • Ikiwa Trump atatimiza ahadi yake ya kuweka vikwazo vya biashara ya kimataifa dhidi ya China na nchi nyingine, bila shaka vita vitaanza. 

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ameshinda kiti hicho kwa sababu Wamarekani wengi hawakufaidi matunda ya utandawazi.

Sera za soko huria na kupunguza kodi za matajiri zimewanufaisha mabilionea, huku wafanyakazi wa kawaida na tabaka la kati likishindwa kunufaika.

Kwa muda wa miaka zaidi ya 20 wastani wa kipato cha Wamarekani wa tabaka la kati hakikuongezeka kabisa. Ukilin-ganisha na miaka baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ukuaji wa uchumi wa Marekani uliwanufaisha wafanyakazi wa kawai-da.

Vijana waliomaliza elimu ya sekondari walipata kazi zinazolipa vizuri viwandani. Sera za soko huria na kupunguza kodi za matajiri zilizoanza wakati wa Rais Ronald Reagan mwaka 1980, hazikuwasaidia wafanyakazi wa kawaida.

Mfumo wa uchumi wa Marekani wa miaka 30 iliyopita, umewabana asilimia 80 ya Wamarekani wa kipato cha chini na cha kati na kuwanufaisha zaidi asilimia moja ya wananchi wenye kipato cha juu.

Chama cha Republican ndicho kilichoongoza mabadiliko ya mfumo wa uchumi na kuelekea kwenye soko huria na utandawazi unaowanufaisha zaidi mabilionea wachache.

Mwaka 2008, Rais Barack Obama alirithi uchumi wa Marekani uliokuwa hatiani kuporomoka kabisa. Mafanikio ya Rais Obama kuepusha kusambaratika na kuporomoka kabisa kwa uchumi hayathaminiwi inavyostahili.

Baada ya kuingia madarakani Rais Obama alifanikiwa kupitisha mpango wa kuongeza matumizi ya Serikali na kupunguza kodi wa dola 800 bilioni, uliosaidia kufufua uchumi wa Marekani.

Benki kubwa zilizokuwa hatarini kufilisika zilisaidiwa na Serikali. Rais Obama alipitisha sera hizi kwa kutegemea wabunge wa chama chake cha Democratic. Wabunge wote wa Chama cha Republican walipinga sera hizo.

Baada ya uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2010, Chama cha Democratic kilipoteza wingi wa viti katika Bunge la Ma-rekani. Sera za Rais Obama kuongeza matumizi ya Serikali, kujenga miundombinu na kuwekeza kwenye elimu zili-pingwa na kukataliwa na Bunge la Marekani lenye wabunge wengi kutoka Republican.

Trump ameahidi atarejesha ajira za viwandani Marekani ambazo zimeondoka na kwenda Mexico, China na nchi nyingine kwa sababu ya soko huria ya biashara ya kimataifa.

Tija ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani inaongezeka kwa kasi kubwa kuliko mahitaji ya bidhaa hizo. Idadi ya ajira za viwandani katika dunia kwa ujumla inapungua wakati uzalishaji wa bidhaa hizo unaongezeka.

Viwanda vingi vikiwamo vya magari, kemikali, nguo na viatu vinatumia roboti na kuajira wafanyakazi wachache. Trump hawezi kuongeza idadi ya ajira za viwandani zinazolipa mishahara mikubwa nchini Marekani.

Ikiwa Trump ana nia ya kukuza kipato cha wafanyakazi na kupunguza tofauti za vipato vya wasionacho na walionacho, kwanza inabidi aongeze uwekezaji wa vitega uchumi ili kuchochea kasi ya kukuza uchumi.

Serikali iwekeze kwenye maeneo mawili: Mosi, miundombinu kama vile barabara, reli na viwanja vya ndege. Pili, utafiti wa msingi. Hivi sasa Marekani inatumia sehemu ndogo ya pato lake la taifa katika utafiti kuliko ilivyokuwa ikifanya mi-aka 50 iliyopita.

Tatu, upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wakati, itachochea uwekezaji wa sekta binafsi.

Miundombinu ya Marekani imeharibika. Madaraja zaidi ya 60,000 yanahitaji ukarabati. Barabara kuu zinahitaji ku-karabatiwa. Viwanja vya ndege vingi vya Marekani ikiwamo vya miji mikubwa kama vile New York ni vya zamani. Hav-ina huduma nzuri na ni kama vya nchi za dunia ya tatu. Havifanani na viwanja vya ndege vya Dubai, Singapore au Bei-jing.

Baadhi ya miji ya Marekani hasa maeneo ya watu maskini hawana maji safi na salama. Miundombinu ya maji taka ni mibovu.

Miundombinu bora itaongeza tija na faida ya wawekezaji wa sekta binafsi. Hivi sasa Marekani inaweza kukopa kwenye soko la mitaji kwa gharama ndogo. Riba ya mikopo ya Serikali inakaribia asilimia sifuri.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Marekani Chama cha Republican kimeshinda kiti cha urais na kina wabunge wengi kwenye Baraza la Wawakilishi na Seneti ya Marekani.

Katika kampeni zake Rais mteule Trump aliahidi kuwa na programu ya kujenga miundombinu ya walau dola 1000 bilioni.

Mpango wa Trump wa kujenga miundombinu umejikita zaidi katika kutumia kampuni za sekta binafsi na kuzipa misamaha ya kodi ili ziwekeze kwenye kujenga miundombinu.
Profesa Ibrahimu Lipumba ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]