UCHAMBUZI: Bado tunaiona Dira ya Maendeleo Taifa 2025?

Muktasari:

Tuwe na viwanda vya kubangua korosho nchini ili wakulima wapate masoko ya uhakika badala ya kunufaisha madalali. 

Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea, ambayo yamekuwa na dira na mipango ya maendeleo ili kuhakikisha maisha ya wananchi wake yanakuwa bora.

Kwa utaratibu huo, Tanzania imeweka mipango yake ambayo inataka hadi mwaka 2025 iwe imetekelezwa kwa vipindi vya miaka mitano mitano.

Mipango hiyo ijulikanayo kama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ina malengo makuu matatu, kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri, kudumisha uongozi bora na utawala wa sheria na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Katika dira hiyo, lengo kuu ni kuielekeza Tanzania kufikia hadhi ya nchi zenye kipato cha kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo 2025.

Katika hili tunapaswa kujiuliza tumepambana kiasi gani kama Taifa, kuondoa umaskini hasa kwa kuhusisha sera na matamko tunayotekeleza sasa.

Tunapiga hatua katika kuhamasisha Tanzania ya viwanda lakini je, hivi viwanda vina mahusiano gani ya kuondoa umaskini wa mamilioni ya wananchi  wanaoishi vijijini?

Tujiulize pia aina ya viwanda tunavyoanzisha, kama  cha kutengeneza tairi, vipuri vya magari, pombe kali vina uhusiano kiasi gani na wananchi maskini vijijini ambao ni walengwa wa dira ya maendeleo?

Ni wazi kwamba viwanda ambavyo Watanzania wengi wanavihitaji ni vile ambavyo vitaongeza masoko na thamani ya mazao ambayo yanalimwa hapa nchini.

Viwanda hivyo vikihusisha mazao ya kilimo, vitaondoa umaskini kwa kasi zaidi kwani mbali na kutumia malighafi za ndani, kama mahindi, pamba, alizeti, karanga, miwa, mchele, mtama na mazao mengine, vitaongeza ajira za Watanzania.

Pia ili kufikia malengo ya dira hiyo, mipango ya maendeleo inatakiwa iwaguse wananchi maskini katika kuhakikisha tunakuwa na viwanda vya kusindika mazao yanayozalishwa ndani kama maziwa na nyama na hivyo kuongeza thamani ya mifugo.

Soko na bei ya mifugo ikiwa juu, itakuwa rahisi kuhamasisha wafugaji kuuza mifugo yao, badala ya kufanya hivyo kwa lengo tu la kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima.

Lakini kama kukiwepo na viwanda vya kutosha vya  nyama, maziwa na ngozi ni wazi biashara ya mifugo itakuwa ni nzuri na mifugo itapungua taratibu huku, maisha ya wafugaji yakiboreka kwani watakuwa na vipato vya uhakika.

Ili kuimarisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025, Serikali ilifikia maamuzi ya kurejea katika uandaaji wa mipango ya miaka mitano kama chachu ya utekelezaji na uharakishaji wa kufikia malengo husika.

Lengo la mipango ya muda mfupi ilikuwa  ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi unaolenga watu maskini zaidi, jambo la kuliuliza ni je, tumetekeleza kwa kiasi gani malengo haya.

Katika mipango hii, Serikali inalenga kuwa na wastani wa kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa wa kwanza ni asilimia 8 na kukua uchumi kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka.

Maeneo ya msingi ya kipaumbele katika uwekezaji Ili kufikia malengo katika miaka mitano ya kwanza, ni miundombinu ya nishati, usafirishaji, Tehama, upatikanaji wa maji safi na huduma za maji taka na kilimo cha umwagiliaji.

Pia Serikali inalenga kuwa na viwanda vikubwa vya mbolea na saruji na vya kielektroniki, maendeleo ya rasilimali watu, kuinua stadi za kazi mkazo ukiwekwa katika masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Hayo yapo kwenye mipango, swali la kujiuliza ni mipango iliyowekwa imewezaje kuwahusisha Watanzania maskini.

Bado miaka minane kufika 2025, tujiulze tumefanikiwa kiasi gani kutekeleza mipango hii au tunarudi kuanza upya?

Mussa Juma ni mwandishi mwandamizi gazeti la Mwananchi mkoa Arusha anapatikana 0754296503