Haki za raia ni muhimu, wanastahili kuishi

Muktasari:

  • Inasikitisha kuona licha ya tukio lile lililolaaniwa na kusababisha mawaziri waandamizi wanne kujiuzulu, askari wengine, safari hii wa Suma JKT wamewaua watu wanne na kujeruhi wengine watano.

Miaka minne iliyopita Serikali ilianzisha Operesheni Tokomeza iliyolenga kuwasaka kwenye maeneo tengefu na hifadhi za taifa watu wanaofikiriwa kujihusisha na ujangili wa tembo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Operesheni hiyo ilifanywa na maofisa kadhaa wa polisi, Jeshi la Wananchi na kikosi maalumu cha wanyamapori waliopewa maelekezo ya kazi hiyo. Kwa bahati mbaya sana, mafunzo na maelekezo hayo hayakuwasaidia; askari wale walishindwa kutofautisha raia wema na wahalifu – wote waliwekwa kapu moja la majangili.

Kutokana na baadhi ya askari hao kutotofautisha wahalifu na wasio wahalifu, kutozingatia haki wala kutumia sheria wakati wa operesheni ile, watu waliokutwa na mifugo na waliokuwa wakiendesha shughuli za kilimo kwenye hifadhi walikamatwa; wakadhalilishwa, wakateswa na baadhi waliuawa. Si hivyo tu, mifugo iliyokamatwa ilifungiwa kwa siku kadhaa bila kupewa majani wala maji.

Inasikitisha kuona licha ya tukio lile lililolaaniwa na kusababisha mawaziri waandamizi wanne kujiuzulu, askari wengine, safari hii wa Suma JKT wamewaua watu wanne na kujeruhi wengine watano.

Askari hao waliokuwa wanalinda msitu wa serikali wa Meru wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha wamesababisha vifo vya watu hao baada ya kuwapiga kwa risasi za moto katika tukio la kukamata mifugo yao na kuipeleka kwenye zizi la serikali.

Mbali ya wafugaji hao wanne kuuawa, wenzao watano akiwamo mtoto wa umri wa miaka 13 anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Oldonyosambu walijeruhiwa kwa risasi za moto.

Mtoto huyo Isaya Thomas (13) aliyepaswa kuwa darasani akiendelea na masomo na wenzake sasa anapigania uhai wake hospitalini baada ya kupigwa risasi mgongoni katika kile kilichodaiwa ni vurugu kati ya wafugaji na askari wa Suma JKT waliokuwa wanalinda msitu wa serikali wa Meru.

Thomasa aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru amehamishiwa Hospitali ya Rufani ya KCMC baada ya hali yake kuwa mbaya. Daktari aliyekuwa akimtibu anasema mtoto huyo alianza kuonyesha dalili za kupooza, kuanzia kiunoni hadi miguuni kutokana na risasi aliyopigwa kuonekana inakaribia uti wa mgongo, hivyo kuhitaji matibabu zaidi.

Hali hiyo sasa inasababisha hali ya baadaye ya maisha ya mtoto huyo kuwa tete. Vilevile, hali hiyo  inasababisha Serikali igharimie matibabu ya mtoto huyo.

Tunashauri kwamba askari wanapotumwa kukamata mifugo au watu kwa madai ya kuingia kwenye maeneo wasiyoruhusiwa wanapaswa kuzingatia sheria, kujali haki na kulinda uhai ili watuhumiwa wakabiliwe na mkono wa sheria. Askari wanapaswa kufuata sheria na kuwakamata wahalifu kwa kuwapeleka mahakamani badala ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha vifo vya raia.

Tunajua kwamba kazi hiyo ina changamoto zake; baadhi ya wahalifu hujifanya raia wema au wengine hata kujifanya wanataka kusaidia askari lakini hugeuka na kusababisha madhara kwao. Kama hayo yanafahamika basi askari ni lazima wajiongeze kiweledi kukabiliana na wahalifu wa kila aina ili wanapolazimika kutumia risasi uwepo uhalali wa kufanya hivyo.

Tunashauri risasi za moto zitumike tu baada ya kwanza kutumia risasi za mpira, kupiga risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi. Hata hivyo tunawashauri raia kuacha kujichukulia sheria mkononi kutaka kupambana na askari kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujikuta wakijiletea madhara ikiwamo kifo.