Ifike hatua sasa polisi waheshimu kazi za waandishi wa habari

Kila Mtanzania anafahamu siku zote kuwa kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, unapozungumzia usalama unamaanisha maisha ya raia yasiwe katika mazingira ya hatari.

Ukiingalia na kuisoma kwa umakini dhima ya Jeshi la Polisi inasema, askari wanatakiwa kuhakikisha usalama wa raia, ulinzi na kinga ya maisha na mali ya wakazi wote wa jamii yetu.

Ukijiuliza kwa nini tuna Jeshi la  Polisi, jibu unalopata kwa haraka haraka ni kwamba wapo kwa ajili ya  kuwahakikishia  wananchi  usalama  wao  na  mali zao, kudumisha amani na utulivu katika jamii, pia kuzuia, kubaini na kupambana na uhalifu.

Sheria iliyounda Jeshi la Polisi inaelekeza watu kufuata sheria wakiwamo askari polisi katika kila hatua ya utendaji wao wa kazi. Hakuna kipengele cha sheria kinachowapa mamlaka ya kupiga watu hovyo, tena ambao hawakufanya vurugu yoyote.

Nasema hivyo kutokana na mazingira yanayoendelea kujitokeza kwenye viwanja vingi vikubwa vya michezo na hasa mchezo wa soka ambao una mashabiki lukuki wanaojitokeza kuungalia.

Lakini, licha ya sheria kuitambua kazi hiyo kubwa ya Polisi ya kulinda usalama wa raia na mali zake, bado kuna baadhi ya askari wasiotambua wajibu wao wawapo kazini, wameendelea kukiuka wajibu huo kwa makusudi.

Wameamua kuweka pamba masikioni kisa  amebeba mtutu wa bunduki, amevaa mkanda wenye rangi ya Bendera ya Taifa na amevaa kofia yenye nembo ya ngao ya Taifa ya ‘Bibi na Bwana’ , basi wanajiona kuwa wako juu ya sheria.

Ikumbukwe kuwa ni wajibu wa kiraia wa Tanzania wakiwamo polisi kuilinda misingi inayodumisha amani na utulivu katika kuhakikisha ustawi wa jamii ya Watanzania.

Alhamisi ya wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa maarufu ‘Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, ilipigwa mechi ya kihistoria ya kirafiki kati ya Timu ya Everton kutoka Uingereza na Gor Mahia ya Kenya.

Kutokana na umaarufu wa mchezo huo, maelfu ya mashabiki kutoka ndani na nje ya Tanzania walimiminika kushuhudia mtanange huo ambao ulimalizika kwa timu ya Everton kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Pamoja na mechi kumalizika salama, lakini nje ya uwanja mapema kabla ya mechi kuanza, kuna mambo mengi ya kusikitisha na kutia aibu yaliyofanywa na baadhi ya walinzi wetu wa amani ambayo hayana afya kwenye ulimwengu wa michezo.

 Hakuna mtu asiyetambua kuwa kila jambo huwa linafanywa kwa maandalizi na utaratibu wake. Ndivyo ilivyofanywa na waandaaji wa mchezo huo, SportsPesa. Lakini cha ajabu Katika mchezo huo, asilimia kubwa ya waandishi wa habari ambao walipangiwa kwenda kuripoti, licha ya kupatiwa vitambulisho kwa ajili ya kuingia uwanjani, walikumbana na kadhia ya baadhi ya askari ambao waliamua kuwazuia kuingia uwanjani na pale walipohoji kwa nini wanazuiwa, walijikuta wakikumbana na vipigo.

Hali kama hii, niliichukulia kama ni matokeo ya askari kukosa mbinu za kuimarisha hali ya amani na usalama uwanjani, kiasi cha kujikuta wakipiga na kuwabugudhi raia na watu wengine waliofika viwanjani kufurahia michezo.

Kitendo cha Polisi kuwashambulia kwa kipigo waandishi wa habari bila huruma wala kujali kujitambulisha kwao wakiwa kazini kukusanya taarifa za kuripoti kwa umma si cha kukivumilia na kukiacha kipite hivihivi hata kidogo.

Waandishi wengi waliokumbana na vipigo hivyo ni wale waliokuwa wakipita kwenye lango kuu waliloelekezwa kupita wakiwa wamevaa vitambulisho vyao, lakini baadhi ya askari hao, walijifanya vipofu hata wasione vitambulisho hivyo na kuwaona kama ni wahuni tu waliofika kuvamia uwanjani hapo, jambo ambalo si sawa hata kidogo.

Kama ambavyo ninataka kazi za polisi ziheshimiwe, pia, ifike mahali na kazi ya waandishi wa habari iheshimiwe, kwani nao wanao wajibu na dhima kubwa inayoinufaisha jamii, askari hao wakiwa sehemu yake.

Nawaomba viongozi wa Jeshi la Polisi, wawaelekeze vijana wao namna ya kufanya kazi kwa kufuata maadili badala ya kukurupuka. Kwa thathmini yangu, asilimia kubwa ya askari wakorofi ni wale wenye umri mdogo jambo linaloonyesha kwamba bado wanahitaji kuelimishwa kuhusu majukumu yao wanapokuwa kwenye maeneo kama hayo ya viwanja vya michezo.

Sikatai kuwa wapo baadhi ya raia watukutu na wavunjaji wakubwa wa sheria, lakini polisi wanazo mbinu mbadala za kuwawajibisha watu kama hao badala ya kutembeza vipigo kwa kutumia virungu na mikanda bila mpangilio.

Nawaomba viongozi wa Jeshi la polisi, waendelee kuwasisitizia vijana wao kufanya kazi kwa ushirikiano. 

Lilian Timbuka ni Mhariri Msanifu wa gazeti la Mwananchi. Anapatikana kwa email: [email protected]