Kweli, Tazara inahitaji kuzaliwa upya

Muktasari:

  • Kama Rais Magufuli alivyoeleza, Tazara ilipoanzishwa ilikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni tano, lakini mwaka 2005 uwezo huo ukashuka hadi kufikia tani 500,000 na sasa umeporomoka zaidi kwani inaweza kubeba tani 128,000 tu kwa mwaka.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu juzi, Rais John Magufuli na mwenzake wa Zambia, Edgar Lungu walikubaliana kubadilisha Sheria ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili kuliwezesha shirika hilo kupata watendaji wanaoweza kuliendesha kibiashara.

Uamuzi huo umetokana na ukweli kwamba uendeshaji wa shirika hilo lililozinduliwa mwaka 1976, umekuwa ukiporomoka siku hadi siku na kugeuka kuwa mzigo kwa mataifa haya mawili.

Kama Rais Magufuli alivyoeleza, Tazara ilipoanzishwa ilikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni tano, lakini mwaka 2005 uwezo huo ukashuka hadi kufikia tani 500,000 na sasa umeporomoka zaidi kwani inaweza kubeba tani 128,000 tu kwa mwaka.

Reli ya Tazara ilijengwa na Serikali ya China kwa lengo la kuziwezesha nchi hizo mbili kusafirisha mizigo hasa ikizingatiwa kwamba Zambia ambayo haina bahari ilihitaji kusafirisha mizigo yake ikiwamo shaba kwenda nje kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mataifa ya Kusini, hatua iliyotokana na kushindwa kutumia Bandari ya Durban, Afrika Kusini iliyokuwa imefungiwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na siasa za kibaguzi wakati huo.

Hata hivyo, baada ya Afrika Kusini kujitoa kwenye makucha ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994, nchi nyingi zilianza kuitumia Bandari ya Durban lakini pia kadri siku zilivyosonga, Bandari ya Beira, Msumbiji nayo ilijiimarisha hatua ambayo iliongeza wigo wa uchaguzi wa njia za usafirishaji baina ya mataifa ya Kusini. Kimsingi Tazara ilishindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya kibiashara kutokana na kuendeshwa katika misingi ya kisiasa kwani kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha, mkurugenzi mkuu anatakiwa kutoka Zambia na naibu wake Tanzania hiyo ni bila kujali weledi au kuzingatia vigezo vingine. Tunasema hiyo ni moja ya kasoro ambazo zimelifikisha shirika hilo hapo lilipo.

Ni kwa sababu hiyo, tunapenda kupongeza hatua ya marais hao ya kutangaza azma yao ya kufumua sheria hiyo na kutunga nyingine ambayo itakuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi hivyo kulifufua shirika hilo ambalo bado tunaamini kwamba lina umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa mataifa haya.

Kama Rais Lungu alivyonukuliwa akisema: “Tunatarajia kupata viongozi wengine wa Tazara kutoka popote pale. Iwe China, Canada, Marekani, tutafanya hivyo. Tutatangaza kazi za mameneja, kwa hiyo watakaokuwa na sifa waje ili kuifanya Tazara kuwa ya kibiashara.”

Nasi tunajazia, hata watumishi wengine wa kada za chini nao wanapaswa kuwa na mtazamo na mwelekeo wa kibiashara zaidi na siyo kuligeuza shirika hilo kama kijiwe cha kuchuma na majungu

Tazara ni shirika lenye mtaji mkubwa wa kibiashara ambao unahitaji usimamizi makini ili kuleta tija iliyokusudiwa na kama Rais Lungu alivyobainisha kwamba, yeye na mwenzake, Dk Magufuli wanajua gharama kubwa iliyotumika kujenga reli hiyo na kazi kubwa iliyofanywa na Watanzania, Wazambia na watu wa China waliojenga, njia bora ya kuwaenzi ni kulifanya kuwa tegemeo kubwa na la uhakika katika usafirishaji wa mizigo na abiria hivyo kuwa kiunganishi kikuu baina ya Tanzania, Zambia na mataifa mengine ya Kusini.