Ligi Kuu yetu hii haiwezi kutoa timu bora ya Taifa

Muktasari:

Kuna mengi yamesemwa kuhusu maandalizi na mambo mengine. Timu hiyo inatakiwa kujipanga ili iweze kufika mbali. Kila mmoja anaiangalia Cameroon kwa jicho jepesi pamoja na kwamba Tanzania imepangwa na Lesotho, Uganda na Cape Verde, bado kuna kazi ngumu.


Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ina kibarua cha kucheza na Lesotho katika mechi ya kuwania kucheza Fainali za Afrika 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon. Fainali hizo zinafanyika baada ya kumalizika kwa Fainali za Gabon ambazo Cameroon ilitwaa ubingwa.

Kuna mengi yamesemwa kuhusu maandalizi na mambo mengine. Timu hiyo inatakiwa kujipanga ili iweze kufika mbali. Kila mmoja anaiangalia Cameroon kwa jicho jepesi pamoja na kwamba Tanzania imepangwa na Lesotho, Uganda na Cape Verde, bado kuna kazi ngumu.

Ni kama tunadharau, hatuoni mikakati ya maandalizi ya maana na mchezo wa Lesotho japokuwa Juni ni mbali, kuanza na ushindi nyumbani ni muhimu kwani inatakiwa safari kuanza na mguu wa kulia.

Lakini pamoja na hayo, nikiangalia, tuna wachezaji wa Ligi Kuu ambao ndiyo huzalisha timu ya Taifa, lakini kwa ligi hii, haiwezi kuzalisha timu bora ya Taifa.

Wakati Ligi Kuu Bara ikiendelea huku kila timu ikiwa imebakisha mechi nane mpaka saba kabla ya kumalizika, imeonyesha karibu timu 10 zinapambana kujinasua na janga la kushuka daraja.

Timu za JKT Ruvu, Majimaji, Toto Africans, African Lyon, Ndanda, Mbao, Stand United, Ruvu Shooting, Mbeya City na Prisons zote haziko salama na atakayechanga karata zake vizuri atabaki.

Ukiangalia hilo unaona kabisa kuwa hali ni mbaya kwenye ligi yetu na Ligi Kuu ambayo ni ya timu chache kwani robo tatu ya timu zote hivi sasa zinapambana kutoshuka daraja.

Hapo ndipo unajiuliza, kwa hali hii kweli, tutapata timu bora ya Taifa kama nusu ya timu za Ligi Kuu zinawania kujinasua kushuka daraja!

Tunajua kuwa kuna vitu vigi vinavyochangia hilo ikiwamo ratiba mbovu ya ligi, hali mbaya ya kifedha kwa timu husika lakini kingine ni wachezaji kutoonyesha moyo wa kupambana, wanacheza tu ili mradi mechi iishe.

Lazima tujue timu bora ya Taifa inatokana na ligi bora lakini kwa hapa kwetu naona mambo ni tofauti na ndiyo maana tunahangaika kupata matokeo katika mashindano mengi tunayoshiriki.

Tumekuwa tukisikia mallalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa timu ndogo kuwa makocha wengi wa timu za Taifa wamekuwa wakizipendelea klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam wakati katika timu nyingine kuna wachezaji wenye viwango vizuri vinavyoweza kutoa ushindani wa kimataifa.

Hivi katika hali hii ambayo inaonekana karibu robo tatu ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu zinapambana kujiokoa, kocha gani wa timu ya Taifa anaweza kupata wachezaji huko?

Kocha lazima ataangalia timu zinazofanya vizuri tu kwa sababu anaamini angalau ndizo zenye wachezaji wazuri .

Lakini pia hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wakati mwingine ndiyo wanaosababisha tushindwe kupata wachezaji bora wa timu ya Taifa kutokana na ratiba mbovu wanazopanga ambazo zinachangia kuwachosha wachezaji.

Wakati mwingine ratiba mbovu inawafanya wachezaji kuchoka na kushindwa kuonyesha viwango vyao uwanjani na mwisho tunaishia kuwalaumu.

Haiwezekani TFF ikawa inaipangia timu mechi tatu ndani ya wiki moja tena ikitakiwa kusafiri mikoa miwili tofauti, hiyo si haki, viongozi wa shirikisho hilo na Bodi ya Ligi wanatakiwa kubadilika.

Kwa hali halisi ya miundombinu yetu na kipato cha timu hasa ndogo ni kama kuwatesa kuwapangia mechi mbili ndani ya wiki moja tena wakitakiwa kusafiri mkoa mmoja kwenda mwingine. TFF, Bodi ya Ligi badilikeni kwani wakati mwingine ndiyo chanzo cha timu kufanya vibaya kwenye ligi.