Monday, July 13, 2015

MAONI: Pongezi CCM kumpata mgombea urais

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa amewanyanyua mikono mgombea urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Hayawi, hayawi yamekuwa. Chama cha Mapinduzi (CCM), jana kilifanikiwa kumpata mgombea wake atakayepeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Mgombea huyo, Dk John Magufuli alichaguliwa na Mkutano Mkuu jana naye alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.

Tunawapongeza viongozi na wanachama wa chama hicho kwa kumaliza ngwe hiyo salama. Kazi iliyokuwa mbele yao hakika siyo tu ilikuwa ngumu, bali pia ilichukua muda mrefu na kutoa changamoto nyingi kwa wagombea, wanachama na viongozi wa wake, kiasi cha kuibua hisia kali miongoni mwa makundi ya baadhi ya wagombea, hasa wale waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda. Yaliyotokea wakati wa mikikimikiki ya wagombea kutafuta wadhamini nchi nzima sasa ni historia. Hata hivyo, ukweli ni kwamba mikikimikiki hiyo kwa kiwango fulani ilikitikisa chama hicho na kuacha nyufa ambazo pengine zitachukua muda mrefu kuziziba.

Mchakato huo haukuanzia tu kwenye vikao vya chama vya Kamati ya Maadili na Usalama, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC), ambavyo vilifuatiwa na Mkutano Mkuu uliomalizika mjini Dodoma jana, bali ulianza zaidi ya mwaka mmoja uliopita kwa chama hicho kufanya maandalizi kwa kuweka taratibu zitakazofuatwa na wagombea wote, ikiwa ni pamoja na kutayarisha ilani ya chama hicho, kupitia upya kanuni za kampeni na uchaguzi ambao kilele chake kilikuwa jana.

Baadhi ya vikao kama vya Kamati ya Maadili na Usalama, CC na NEC vilifanyika kwa faragha pengine kutokana na unyeti wa mijadala iliyotokana na mchujo wa wagombea kutoka 38 hadi watano, kisha watatu waliotakiwa kupelekwa kwa Mkutano Mkuu ili apatikane mmoja wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

Wananchi wengi wameonyesha kutiwa moyo na mchakato huo mzima ambao ulionekana kufanyika kwa amani na katika mazingira yanayokubalika. Wajumbe wengi walisema kuwa, pamoja na kuwapo kasoro ndogondogo, waliridhishwa na matayarisho ya vikao husika, ukiwamo Mkutano Mkuu.

Sekretarieti ya chama hicho imepongezwa na wajumbe hao kwa kuratibu mchakato wote na hatimaye kutoa matokeo tuliyoyashuhudia kwa wiki yote iliyopita. Sote tunakubaliana kwamba iwapo sekretarieti hiyo isingefanya usimamizi madhubuti na kuchukua tahadhari kubwa katika kufanya uamuzi husika, leo tungekuwa tunasema mengine.

Katika kuhitimisha shughuli za uchaguzi za chama hicho jana, zilitolewa hotuba nyingi kutoka uongozi wake wa juu, mgombea urais na wagombea walioingia tatu bora katika mbio hizo za urais. Hotuba hizo zilijikita katika kupongezana kwa kile walichokiita umoja na mshikamano ulioonyeshwa na wagombea, viongozi na wajumbe wote waliokaa na kutoa uamuzi katika ngazi zote husika. Tunasema hilo ni jambo jema. Hata hivyo, pamoja na chama hicho kupita katika mchakato huo kikiwa salama, tunadhani kazi ambayo bado ipo mbele yake ni kubwa mno pengine kuliko ile ambayo imemalizika.

Lazima tukubali kwamba chama hicho hakijaponya majeraha na mipasuko iliyotokana na misuguano miongoni mwa wagombea na makundi yao. Pamoja na hotuba za kujiliwaza jana, mpasuko na majeraha hayo yalikuwa bado yapo wakati hotuba hizo zilipokuwa zikitolewa na baada ya wajumbe kuagana na kurudi makwao.

Kazi kubwa inayokikabili chama hicho sasa ni kuvunja makundi hayo kabla ya kukabiliana na wapinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

-->