Maandalizi ya mapema ndiyo siri ya mafanikio kwa klabu zetu

Wiki iliyopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa ratiba ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 20.

Kutolewa kwa ratiba hiyo bila shaka ni mwanzo wa msimu mpya wa ligi wa mwaka 2016/17, ambao utakuwa wenye ushindani mkubwa zaidi kwa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Tunatumia nafasi hii kuzipa angalizo klabu zetu zinazoshiriki ligi hiyo, zikiwamo zilizopanda daraja, Mbao FC, African Lyon na Ruvu Shooting kwamba zinakabiliwa na kibarua cha kuonyesha uwezo kisoka.

Tunatambua kuwa wachezaji wetu wanafahamu changamoto zote zinazowakabili wanaposhiriki ligi, zikiwamo za usafiri wa umbali mrefu kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, ambako mbali ya kuwachosha, pia hugharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Kwa kutambua hilo, tunadhani wadhamini wa ligi hiyo watakuwa tayari wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha vifaa vinavyohitajika pamoja na fedha za nauli vinapatikana mapema ili kuwezesha timu zetu kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa ushiriki kwenye ligi.

Kwa upande wa makocha na wachezaji, tunawashauri wazingatie mazoezi kupitia maandalizi ambayo hatuna shaka yalianza tangu ulipomalizika msimu uliopita, ingawa tunatambua kuwa wapo wachezaji wapya ambao wamesajiliwa na klabu hizo, wanaohitaji muda ili kuzoeana na wenzao au mifumo ya klabu mpya walizojiunga nazo.

Tunawashauri wachezaji wajitambue wao na wajibu wao kwa klabu zao na mchezo wa soka kwa jumla, watambue hiyo ni ajira kwao inayowawezesha kumudu maisha yao na hivyo hawana sababu ya kufanya mizaha, ikiwamo ya kuzembea mazoezi, uvutaji bangi na matumizi ya dawa za kulevya.

Tunazishauri timu zetu zizingatie kanuni, zikiwamo za kuwa na vikosi vya vijana  kama  zinavyoshauriwa na TFF kwa maelekezo ya mashirikisho ya mchezo huo,  Afrika (CAF) na hata lile la kimataifa, Fifa.

Tunaamini,  wachezaji vijana tunao wengi nao ni hazina kubwa ambayo ikitumika vizuri, itasaidia klabu zetu na hata nchi yetu kwa jumla kushiriki vizuri mashindano ya kimataifa kila mwaka tena kwa mafanikio.

Kwa kufanya hivyo, vijana wetu walioandaliwa vizuri, wenye nidhamu watakuwa mabalozi wazuri, hatimaye watapata nafasi ya kucheza soka nchini kwa mafanikio au wakati mwingine kucheza soka la kulipwa kama ambavyo wamefanya kina Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na hata Mrisho Ngassa.

Ni lazima makocha wa timu zetu hasa za vijana kwa ngazi ya klabu wapewe nafasi ya kuwaandaa kwa ajili ya kuwamo kwenye vikosi vya wakubwa siku za usoni, wala siyo kuwaokota wale wa mitaani ili kuidanganya TFF.

Tabia ya klabu zetu kubwa na ndogo ya kuota wachezaji wa mitaani na kuwavika jezi zao iachwe kwani haina tija kwa maendeleo ya klabu hizo wala Tanzania kwa ujumla.

Hilo limekuwa likitokea na tunasema ni jambo ambalo halikubaliki. Ni aibu kwa nchi kubwa kama Tanzania yenye vipaji vingi ambavyo vikiendelezwa vitaitangaza kimataifa, kutokuwa na mfumo wa kuendeleza soka. Tunazishauri klabu zetu ziamke na kuwekeze nguvu, akili na rasilimali zao zote na zikumbuke kuwekeza kwenye soka la vijana kwani ndilo chimbuko la wachezaji wazuri wa siku za usoni.

Kwa kufanya hivyo, vijana hao wataonekana  na kuuzwa na hata kuzichezea klabu mbalimbali za Ulaya na kwingineko duniani, ambako wao mbali ya kuitangaza nchi watajiingizia pia kiasi kikubwa cha fedha na kuondokana na umaskini.