Mashabiki wasiamue malengo ya timu zao

Muktasari:

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kesho watakuwa Ghana kucheza mechi yao ya marudiano dhidi ya Medeama ukiwa ni mchezo wa nne wa Kundi A wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kesho watakuwa Ghana kucheza mechi yao ya marudiano dhidi ya Medeama ukiwa ni mchezo wa nne wa Kundi A wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Katika mchezo huo, Yanga inahitaji kushinda ili kujiweka katika matumaini ya kusonga mbele na endapo itafungwa, basi ndoto yao ya kucheza nusu fainali itakuwa imefikia mwisho.

Mashabiki wengi wa Yanga wamekuwa wanyonge kutokana na mwenendo wa timu yao katika hatua ya makundi baada ya kupoteza michezo miwili na kutoka sare moja tena dhidi ya Medeama, timu waliyoamini ni dhaifu zaidi katika kundi hilo lenye timu za TP Mazembe ya DR Congo na MO Bejaia ya Algeria.

Hapo ndipo ninapojiuliza, hivi malengo ya Yanga yalikuwa ni yapi katika mashindano ya kimataifa na wote walijua nia yao au vipaumbele vilikuwa ni tofauti?

Nakumbuka kocha wa Yanga, Hans Pluijm mwanzo wa msimu alisema wazi kuwa lengo lake ni kuhakikisha Yanga inacheza kwanza hatua ya makundi na chochote kitakachotokea baada ya hapo ni ziada.

Simba kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa ikisajili wachezaji vijana kwa lengo la kujenga timu, lakini wanapofika katikati ya msimu wanabadili malengo na kuwaza ubingwa na wanaposhindwa wanatimua wachezaji na makocha.

Ndiyo maana, kila msimu wamekuwa wakitimua makocha na kusajili rundo la wachezaji wa kigeni wasiokuwa na viwango kwa sababu ya kukosa malengo.

Azam ikiwa ndiyo kwanza imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kocha wake, Joseph Omog (kwa sasa yuko Simba) alipewa jukumu la kuhakikisha timu inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, kitu ambacho ni kigumu kufikiwa na timu inayoshiriki kwa mara kwanza mashindano hayo.

Mbeya City baada ya kufanya vizuri katika msimu wake wa kwanza mashabiki na viongozi wake walijiaminisha kwamba timu yao inastahili kuingia katika kundi la timu zinazowania ubingwa. Kilichofuata, baada ya hapo ni kulaumiana na kocha, huku wachezaji wakionekana hawafai jambo lililosababisha msimu uliopita kupigana kuepuka janga la kushuka daraja.

Timu kama Mbao FC, Ruvu Shooting na African Lyon zilizopanda daraja msimu huu zinapaswa kujiwekea lengo moja la kuhakikisha hazishuki daraja, jambo jingine lolote litakalotokea baada ya hapo ni ziada na halipaswi kuwaondoa katika lengo kuu.

Viongozi wa klabu wanapaswa kuwapa malengo makocha wao tangu mwanzo wa msimu. Wajue nini wanachokitegemea kupata kwa timu zao mwisho wa msimu bila ya kukubali kuingiliwa na nguvu ya mashabiki. Kitendo cha kuruhusu mashabiki kuamua malengo ya timu siku zote kumekuwa na mwisho mbaya kwa timu pamoja na makocha na viongozi kuonekana hakuna walichokifanya.

Viongozi wanapaswa kuwa na umoja kuunga mkono kocha hasa pale anapokuwa katika mstari ule wa malengo waliyokubaliana. Msimamo huo umemfanya Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kudumu katika timu hiyo kwa miaka inayokaribia 20 sasa.

Wenger lengo lake kubwa alilopewa ni kuhakikisha Arsenal inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikimaanisha ahakikishe timu inamaliza katika nafasi nne za juu za Ligi Kuu England wakati wote, jambo ambalo amelitimiza hivyo hata mashabiki wakipiga kelele vipi uongozi unamlinda.

Viongozi wa klabu ni lazima wajiamini katika uamuzi wao wa nini timu inatakiwa kufanya katika kila msimu na kuwaambia mashabiki bila ya kuwaonea aibu kwamba malengo yetu msimu huu ni kuchukua ubingwa wa Kombe la FA au kumaliza katika tatu bora.

Mwisho viongozi wa klabu wanatakiwa kujifunza kwa Kocha wa Leicester City, Claudio Ranieri pamoja na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini msimu huu ameweka malengo ya kumaliza katika 10 bora.

Andrew Kingamkono ni mhariri wa michezo gazeti la Mwananchi