Saturday, March 18, 2017

Mawaziri wapunguze kauli za kukurupuka

 

Kuna migongano isiyo ya lazima tuliyoishuhudia kati ya mawaziri na Rais ambayo kimsingi inatokana na baadhi ya mawaziri kutoa maagizo, la hivi karibuni likiwa hitaji la vyeti vya kuzaliwa katika ndoa.

Tutaorodhesha. Mwaka jana, kuna waziri alimteua mkuu mpya wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lakini saa tano baadaye, tena usiku ikulu ilitoa taarifa ya kutengua uteuzi huo.

Pia, tulishuhudia wakuu wa mikoa ikiwamo Mkoa wa Mwanza wakishirikiana na makamanda wa polisi kuwaswaga na kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo kutoka kwenye maeneo wanayofanyia biashara zao na kuzua taharuki lakini siku iliyofuta mkuu wa nchi alikemea akisema hakuahidi hivyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba 2015.

Halafu tulishuhudia matangazo ya kuwataka wananchi wajiandae kwa bei mpya ya umeme lakini mkuu wa nchi, tena akiwa kanisani alisema upandishaji umeme ulikuwa ukiukwaji wa sera ya kuandaa mazingira mazuri ya kukaribisha uwekezaji wa viwanda.

Tulijiuliza sana. Je, kabla waziri hajatoa agizo huwa hakuna mawasiliano na mkuu wa nchi ili ajiridhishe kwamba haliwaumizi wananchi? Je, waziri hutangaza hadharani mambo yake au yanayokuwa yamejadiliwa na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri?

Kabla hatujapata majibu ya maswali hayo, juzi Alhamisi, akiwa Morogoro Waziri wa Sheria na Katiba alitoa agizo tenge akiwataka viongozi wa Serikali, kimila na dini wanaofungisha ndoa kuhakikisha kuwa kabla ya kufanya hivyo wahusika yaani wanaooana wana vyeti vya kuzaliwa.  Agizo hilo lilimaanisha kwamba sifa mojawapo muhimu ya kuoa au kuolewa ni cheti cha kuzaliwa.

Kama tulivyotarajia, jana asubuhi Rais John Magufuli alitoa tangazo la kufuta agizo la waziri akieleza kasoro kadhaa mojawapo ikiwa changamoto ya kupata vyeti hivyo kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelifuta agizo lililotolewa jana tarehe 16 Machi, 2017 na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti la kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa watu wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe 01 Mei, 2017,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.

Je, kwa nini waziri hakujiuliza changamoto hiyo itatatuliwa vipi? Hivi anajua mpaka leo kati ya Watanzania wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 45 ni asilimia ngapi wana vyeti vya kuzaliwa? Kwa nini waziri anataka jamii itekeleze agizo lake wakati hakuna kifungu cha sheria kinacholazimisha?

Tunampongeza Rais Magufuli hasa aliposema “ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida” maana kwa wakati huu hakuna kifungu chochote cha sheria ya ndoa kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe.

Mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo. Tunaomba mawaziri wasiwe chukizo, karaha na kero; wapime kauli zao kabla ya kuzitoa katika jamii.

-->