Serikali iwasaidie wakulima kuijenga Tanzania ya viwanda

 Waziri Profesa Jumanne Maghembe

Muktasari:

Alitolea mfano wa kilimo cha zao la pamba kwamba kwa kutumia mbegu za kawaida uzalishaji wake ni mdogo na hauna tija kwa mkulima tofauti na mbegu za GMO ambazo zinaonyesha uwezo mkubwa wa uzalishaji.

Katika miaka ya hivi karibuni tumewasikia baadhi ya wanasiasa wakitoa maoni tofauti juu ya matumizi ya mbegu zinazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).

Baadhi yao, ambao sauti zao husikika zaidi kuliko hata watafiti wetu, wamekuwa wakisema kuwa mbegu za GMO ni nzuri kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara lakini wengine wamekuwa wakipinga, siyo uwezo wake, bali athari kwa utafiti wa ndani.

Msimamo wa serikali katika suala hili haukuwa wazi hadi hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane, Waziri Profesa Jumanne Maghembe aliposema Tanzania itapiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara iwapo wakulima na wadau wengine wataondokana na dhana potofu ya kukwepa matumizi ya mbegu zinazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya GMO.

Akitumia kaulimbinu ya mwaka huu, “Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati”, Profesa Maghembe alisema sekta ya kilimo ndiyo itakayowezesha upatikanaji wa mahitaji ya malighafi ya viwanda na matumizi ya mbegu bora zinazotokana na teknolojia ya GMO ndiyo pekee itakayowezesha kufikiwa malengo hayo pamoja na kumwongezeka mkulima tija.

Alitolea mfano wa kilimo cha zao la pamba kwamba kwa kutumia mbegu za kawaida uzalishaji wake ni mdogo na hauna tija kwa mkulima tofauti na mbegu za GMO ambazo zinaonyesha uwezo mkubwa wa uzalishaji.

Wanaotoa angalizo kuhusu mbegu za GMO wanasema nchi zitakazoingia kwenye mtego wa GMO, ikiwemo Tanzania zitakuwa tegemezi na hazitakuwa na mbegu zake tena zaidi ya kulazimika kuziagiza nje ya nchi kwenye makampuni makubwa.

Kwa maoni yao teknolojia hiyo itakuwa inaweka mfumo wa kudhibiti uzalishaji wa chakula kwa mataifa maskini, na kufanya bidhaa hiyo imilikiwe na mataifa machache.

Tunadhani angalizo hili lina mashiko, lakini ikiwa kwa kauli ya Profesa Maghembe Serikali tayari imefanya utafiti na kujiridhisha kuhusu teknolojia hiyo basi kazi kubwa iwe kuwaelimisha wakulima manufaa ya teknolojia hiyo mpya kuelekea mapinduzi ya kilimo.

Mambo mengi mazuri huonekana au kufanyika wakati wa sherehe na sikukuu tu mijini na siyo kwa walengwa vijijini. Wakulima ni asilimia zaidi ya 75 ya Watanzania na wanaishi vijijini ambako hawafikiwi na tafiti hizi kwa sababu ya uhaba wa maofisa ugani.

Maofisa hao muhimu wanapaswa kukaa karibu na wakulima ili kuwafundisha, kuwaelekeza na kubadili fikra zao katika uendeshaji wa kilimo ili kiendane na teknolojia mpya, mabadiliko ya tabia nchi na hali ya mvua.

Wakulima wanahitaji elimu hasa kwa vile mbegu za aina hiyo imeelezwa zinastahimili magonjwa ya aina mbalimbali, ukame na kuongeza uzalishaji.

Kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa mazao, basi waanzishiwe pia masoko ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri badala ya kipindi cha mavuno kuwaachia walanguzi.

Tunatoa rai kwamba katika kipindi hiki ambacho Serikali inahimiza matumizi ya mbegu za GMO basi wakulima wapelekewe pembejeo kwa wakati, maofisa ugani wajenge utaratibu wa kutoa elimu na wakulima watafutiwe soko la mazao yao ili waweze kuchangia ujenzi wa Tanzania ya viwanda.