Simba, Yanga mnazalisha matatizo yenyewe

Muktasari:

Wakati mwingine, mtu anafikiria kufanya a, b, c kwa ajili ya ama Simba au Yanga, sasa watakachofanya wanachama, wanakuangalia tu unachofanya, baada ya muda utasikia tayari zengwe limeanza, hatutaki, hatutaki bila hata lengo kufikiwa.

Ukizigusa Simba au Yanga kwa chochote kile, wanachama wanakuja juu. Ukitaka kufanya mabadiliko kidogo, wanakuja juu.

Wakati mwingine, mtu anafikiria kufanya a, b, c kwa ajili ya ama Simba au Yanga, sasa watakachofanya wanachama, wanakuangalia tu unachofanya, baada ya muda utasikia tayari zengwe limeanza, hatutaki, hatutaki bila hata lengo kufikiwa.

Sasa unajiuliza, ninachofanya si kwa ajili yangu, ni maendeleo ya klabu, ni kwa ajili ya mafanikio ya klabu, lakini bado mizengwe iko hapa na pale.

Sitaki kuingia kwenye mzozo wa Yanga kwa kuwa tayari suala liko katika vyombo vya sheria, lakini ninachotaka kusema hapa ni kwa wanachama wa Simba na Yanga kwa jumla.

Dunia inavyokwenda sasa, teknolojia iko juu mno, kwamba kila kitu kinafanywa kwa njia rahisi mno. Mataifa yaliyoendelea kila kukicha hawataki kusumbua mwili, hutengeneza vitu rahisi kwa ajili ya kurahisisha maisha kwa jumla.

Mabadiliko ya teknolojia ndiyo maendeleo. Huwezi kuwa na maendeleo bila kuwa na mabadiliko, sasa kwa wanachama wa Simba na Yanga msamiati wa mabadiliko ndani ya klabu zao bado hawajaufahamu.

Wanachama wengi wa Simba na Yanga, hawataki mabadiliko, wanataka kubakia kwenye zama za ujima ambao kila mmoja anafikra za umiliki wa mali kwa pamoja.

Kukubali mabadiliko ya mifumo ya maisha, ndiko kunafanya kuwapo na mabadiliko ya utendaji na uendeshaji wa raslimali kwa ajili ya kuleta matokeo mapya katika jamii inayotuzunguka na jamii za mbele kwa kuwa maisha yanaendelea.

Tatizo lililopo hasa kwa wanachama wa Simba na Yanga ni kutotaka kuzisaidia klabu, lakini wanakuwa wakali kwelikweli inapotokea viongozi wameamua sasa ni wakati wa klabu kufanya mabadiliko hata kama unafuata utaratibu wa Katiba.

Ikiwa wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga, kama kweli wanataka kuona klabu zao zikipiga hatua, ziwafanyie tathmini wawekezaji katika klabu hizo na kisha wanachama kumaliza wenyewe kuliko kuanza mizengwe kukataa au kuwachambua wawekezaji. Kupitia matawi ya Tanzania nzima kwa wanachama wa Simba na Yanga, kupitia wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga wangebuni utaratibu wa kuzichangia klabu zao kwa maendeleo yao.

Bila kuingiza mafisadi kwenye ukusanyaji mapato, wanachama na mashabiki watakuwa na uwanja wao ama chochote kile wanachotaka kwa kuwa fedha ipo.

Mfano, tuchukue wanachama na mashabiki wa Simba au Yanga wapo 1,000,000 Tanzania nzima baada ya sensa yao kufanyika, ukaandaliwa utaratibu kila mmoja akachanga Sh50,000 kama kweli wanaumwa na Simba au Yanga na ninajua wengine watatoa zaidi, zitapatikana Sh50 bilioni.

Hivi Sh50 bilioni timu zitashindwa kujiendesha? Mfano, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji inaelezwa anaidai Yanga Sh11 bilioni hapo hazijalipwa? MO alisema anataka kuipa Simba Sh20 bilioni kwa hicho anachotaka kukifanya, sasa wenye kuipenda Simba wakichanga Sh50,000 kwa idadi yao 1,000,000 hazifikii malengo?

Watu wanalialia tu mimi Simba, mimi Yanga lakini hakuna wanachokifanya, mabadiliko yakija hata kwa kufuata katiba, wanaweka zengwe, hivi tuwaweke kundi gani?

Viongozi Simba na Yanga watumieni wanachama na mashabiki wenye moyo, kuendesha klabu kuliko kuwatumia kupokea majungu na mizengwe.

Baadhi ya wanachama kazi yao ni kubeba majungu huku kupeleka kule, tunataka wachangie kuonyesha kweli wanaipenda timu.

+255 655 264 003