Suluhu ya Serikali, Dangote izingatie maslahi

Aliko Dangote

Muktasari:

Kilichoelezwa katika taarifa ya kampuni hiyo wiki hii ni kwamba kimesitisha uzalishaji, kwa zaidi ya wiki kutokana na hitilafu katika mitambo yake ambayo mafundi wanashughulikia.

Tumefuatilia kwa umakini mkubwa hoja za Kampuni ya Dangote Tanzania kuamua kusitisha uzalishaji wa saruji katika kiwanda chake cha mkoani Mtwara.

Kilichoelezwa katika taarifa ya kampuni hiyo wiki hii ni kwamba kimesitisha uzalishaji, kwa zaidi ya wiki kutokana na hitilafu katika mitambo yake ambayo mafundi wanashughulikia.

Katika ufuatiliaji huo tumezingatia maslahi ya pande zote yaani Serikali na Dangote hasa madai ya ukubwa wa gharamza uzalishaji hapa nchini ikilinganishwa na nchi nyingine 15 barani Afrika ambako kampuni hiyo iliwekeza.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na mwenzake wa Nishati na Madini waliibuka kutoa msimamo wa Serikali kuhusu uwekezaji wa kiwanda hicho kilichopanga kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na kamishna wa madini pia walitoa ufafanuzi kuhusu kinachochangia kampuni hiyo kutumia gharama kubwa.

Vilevile, tumesoma kwa umakini maelezo yaliyotolewa na aliyekuwa kamishna wa madini katika kipindi ambacho Serikali ilifanya ushawishi na kukaribisha uwekezaji wa Dangote. Tumegundua kuwa kwa makusudi ya kuongeza uwekezaji nchini Serikali iliingia mkataba ya Dangote Tanzania kwa ahadi ya kupewa nafuu kubwa katika uwekezaji wake.

Kamishna huyo wa zamani anasema, “Nikiwa Kamishna wa Madini wakati ule, tulishirikiana na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuipa Dangote leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini ya chokaa zilizokuwa zinamilikiwa na Stamico... Ahadi pia ilitolewa kukipa kiwanda cha Dangote nishati ya umeme wa bei nafuu kwa kuiuzia gesi na makaa ya mawe kwa bei nafuu na pia uwezekano wa kutoa umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa kwa gharama nafuu. Kwa mazingira hayo kiwanda kilijengwa.”

Waswahili wanasema ahadi ni deni. Japokuwa makubaliano hayo yanatonesha vidonda vya miaka mingi kuhusu kutokuwepo kwa uwiano wa vivutio kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje, ukweli utabaki kama hayo ndiyo yalikuwa makubaliano kati ya Serikali (bila kujali awamu) na kampuni mama ya Dangote Group ambayo iliridhia kujenga kiwanda hicho, ahadi hiyo itekelezwe.

Serikali ndiyo ilifunga safari kuishawishi kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini kwa ahadi ya vivutio kadhaa hivyo si sahihi kwa Serikali kubadili msimamo bila kukaa meza moja na mwekezaji huyo au wawekezaji wengine kwa majadiliano.

Serikali inaweza kusema itabaki na msimamo wake, lakini tunadhani ikiwa itafikia mahali mwafaka usipatikane kutakuwa na madhara makubwa.

Madhara ya kwanza ni kwamba kiwanda kikifungwa maelfu ya watu waliopata ajira rasmi na zisizo rasmi wataathirika. Lakini pia itatoa picha mbaya kwa wawekezaji wengine wa nje kusita kuja nchini kwa hofu kwamba nao wanaweza kubadilishiwa gia angani.

Sakata la Dangote liwafumbue macho watunga sera kwamba waweke wazi fursa zilizopo kwa wawekezaji ya nje bila kuwaumiza wa ndani, bila kuipendelea moja wala kuikandamiza nyingine.

Sera hiyo iwe mwongozo kwa wataalamu wetu wanapoingia makubaliano wasibabaike au kuridhia maombi ambayo wawekezaji wa nje wakija nchini hawawezi kutekelezewa kama inavyotokea sasa kwa Dangote.

Mwisho tunawashauri viongozi wetu wasisubiri mambo yaanikwe kwenye vyombo vya habari ndipo waanze kushughulikia matatizo kama Jeshi la Zimamoto; Wawe wasikivu, wajadili kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.