Saturday, March 18, 2017

TUONGEE UJANA: Kumbuka ujana hudumu kwa miaka 15

Ujana ni maji ya moto. Hiyo ni kauli ya wahenga inayosemwa na kurudiwa kila mara, iwe na vijana wenyewe au na wazee, ikiwa na lengo la kuonya, kukumbusha na kuwajibisha. Mbali na kauli hiyo ipo nyingine isemayo “wakati ni ukuta”, unaweza kuimalizia kwa kusema, “ukishindana nao utaumia mwenyewe”.

Kauli hii hasa ndiyo nataka kuizungumzia hapa, kuwa wakati ukipita umepita hauwezi kurudi nyuma na kama hukujipanga kwa yanayopaswa kufanywa wakati husika hutapata nafasi ya kufanya hivyo tena.

Usijipe mawazo ya kujutia wakati uliopita, kwa sababu ya kutotimiza wajibu wako, ulipokuwa una nafasi ya kufanya hivyo.

Hivyo  ni jambo muhimu kutumia wakati ulionao sasa hususani, vijana kwa sababu bado una nguvu kwa ajili ya kufanya maandalizi ya baadae.

Kumbuka ujana haudumu zaidi ya miaka 15 baada ya kuwa mtu mzima kwa mujibu wa Katiba, yaani unapokuwa umefikisha miaka 18.

Hivyo wakati huo wa miaka 15 tangu utimize umri wa kuwa huru ni vyema ukafanya mambo yanayoangalia mbele zaidi kuliko kuendelea kufanya vitu kwa kuangalia nani kafanya nini na wewe uige.

Kipindi hiki kama unasoma ni vyema ukasoma kwa bidii. Ukazingatia masomo na kuacha vitu vingine vya ujana ikiwamo anasa kwa ajili ya kuziponda raha baadaye utakapohitimu na kufanya vizuri zaidi.

Kama umebahatika kupata kazi ukiwa ndani ya umri huu, ndiyo wakati wa kufanya maajabu ya utendaji huku ukisumbua akili ufanye kitu gani cha ziada kukuongezea kipato cha halali badala ya kuharibu kwa kuiba au kufanya kazi ndivyo sivyo.

Wakati huu ndiyo utakufanya uishi vizuri baadaye, wewe na familia utakayoandaa kwa sababu kama binadamu hilo haliepukiki.

Kuchelewa kuanza kwa ufanisi na kujituma, husababisha kuanza michakato ya maisha na kusumbua akili wakati ambao unahitaji kutulia.

Kadri umri unavyokwenda na majukumu huongezeka. Ukiwa na umri mkubwa unawaza kuitunza familia, kusomesha watoto, kujenga, kununua gari, itakuwia vigumu kufikiria kitu cha kufanya kujiongezea kipato, uzijue changamoto zake na ufahamu namna ya kukabiliana nazo.

Vitu hivyo hapo juu ni vingi kuvifanya kwa wakati mmoja ilhali unaweza kuvifanya kwa ufanisi na taratibu ukiwa na miaka isiyozidi 35.

Ninachotaka kukumbusha hapa ni kuwa ujana hauzidi miaka 35, baada ya hapo unaanza maisha ya familia na majukumu mengi zaidi. Kujipanga ndiyo jambo pekee la msingi badala ya kusubiri maisha yakupange.

Ukipangwa na maisha utalazimishwa kufanya vile ambavyo hukupanga kuvifanya, utaanza kulea kwa bahati mbaya bila kujiandaa, utasomesha bila kujiandaa, utapanga ilihali ulikuwa na uwezo wa kujenga nyumba yako.

Ukiwa kijana ni vizuri kuhakikisha kila jambo unalolifanya lipo sambamba na mafanikio ya ndoto yako.

Weka jitihada kwenye fani uliyopo kufikia malengo yako, badala ya kuyumbishwa na mipango ya watu wengine, ambayo kwa bahati mbaya haiwezi kukusaidia kwa sababu hamtafuti kitu kimoja kwa ajili ya wote.

Usiwe mtekelezaji wa kukurupuka kwa kusikia maneno na maoni ya watu pekee, bali kuyachambua na kuyafanyia kazi kwa kina.

Siku zote kumbuka hakimu wa kesi zako, mahakama ya kifungo au uhuru wako ni kichwa chako kulingana na malengo yako.

-->