Monday, July 17, 2017

Tumejipa kazi ya bure kwa Rwanda

By Julius kihampa

Matokeo ya sare ya bao 1-1 yanaifanya Taifa Stars kujiweka katika wakati mgumu wa mchezo wa marudiano mwishoni mwa wiki dhidi ya Rwanda.

Katika mchezo wa juzi wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) tulihitaji ushindi wa aina yoyote ili kujiweka katika mazingira mazuri.

Lakini kwa mshangao, Taifa Stars ilijikuta ikiduwazwa kwa bao la ugenini la Rwanda lililofungwa na Dominique Nshuti dakika ya 18, kabla ya Stars kusawazisha kwa mkwaju wa penalti wa nahodha Himid Mao.

Haikuwa kazi rahisi, lakini nadhani kocha Salum Mayanga alipoteza maajabu aliyofanya Afrika Kusini katika mashindano ya Kombe la Cosafa.

Si mimi peke yangu niliyeshindwa kuamini, lakini matokeo ya juzi ni wengi yamewahuzunisha kutokana na imani kubwa iliyokuwa kwa Stars hasa baada ya kucheza vizuri katika mashindano ya Cosafa.

Sitaki kuamini kwamba kukosekana kwa Elias Maguli na Thomas Ulimwengu kumeiathiri timu ya Mayanga kiasi cha kushindwa kuonyesha soka tuliloliona Afrika Kusini.

Ni wachezaji hao wawili ambao walikosekana katika kikosi kilichopita ukiacha Mbaraka Yusuf aliyeumia, lakini ugumu ambao tumejiwekea ni kama tumeamua tu iwe hivyo.

Tukianza na kocha mwenyewe, sidhani kama aliyategemea matokeo haya kutokana na aina ya timu waliyoidhania na kuishi na kumbukumbu za Afrika Kusini.

Ni ukweli usiopingika kwamba Taifa Stars ilikuwa katika kiwango kizuri ilipokuwa Afrika Kusini, lakini kilichoshindikana juzi ni kushindwa kuutambua mchezo husika kwa kina.

Tulikuwa na umakini mzuri katika mashindano ya Cosafa tukiwa waalikwa tu, lakini kilichoonekana ni kwamba akili ya wachezaji ilikuwa makini kana kwamba ilikuwa ni mashindano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Kuanzia pale, kila Mtanzania alikuwa na uhakika kuwa mchezo dhidi ya Rwanda unaweza kuwa na matokeo mazuri kutiokana na aina ya kikosi kinachounda Taifa Stars kwa sasa.

Ukiangalia kwa timu iliyocheza juzi ni dhahiri utajua kuna sura mpya ya John Bocco pejkee aliyechukua nafasi ya Maguli, ambaye hatakiwi kucheza mashindano hayo kutokana na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi (Oman).

Lakini akili za wachezaji ama mbinu ya kocha Mayanga katika kuelekea mchezo huo haikuwa rafiki kama ilivyokuwa katika mashindano ya Cosafa wiki mbili zilizopita.

Matokeo ya sare ya bao 1-1 tena tukianza kufungwa tukiwa nyumbani kumezua hofu ya kufuzu kwa mashindano haya, ambayo yangeweza kututoa kimasomaso angalau nasi tukashiriki kimataifa badala ya kuendelea na mechi za kirafiki kila kukicha na kusubiri kuitwa na wenzetu wa Afrika Kusini kwenda kunogesha mashindano yao.

Kuna kila sababu ya kocha Mayanga kuwashityua wachezaji wake, kuwaaminisha kuwa mashindano haya ni muhimu kuliko ilivyokuwa kwa Cosafa.

Kushinda mchezo ujao kutatufanya kukutana na mshindi kati ya Sudan Kusini na UGanda, bado unaona jinsi hali ilivyokuwa ngumu kwa Tanzania na hili linatakiwa kuwa chachu ya kubadilika.

Vijana wetu wanatakiwa kubadilika kuanzia sasa, kwanza kutambua umuhimu wa mashindano yenyewe na pili kutoka usingizini na kupambana kama walivyofanya Afrika Kusini.

Sitaki kuamini kama vijana wamechoshwa na kazi ngumu waliyofanya Afrika Kusini, walikuwa na mapumziko ya kawaida, ambayo yalikuwa endelevu kimazoezini na kuwa na muda mwingi wa kuweka miili sawa.

Kiujumla tunahitaji kurudisha akili mchezoni kama tunahitaji kwenda Kenya kwa ajili ya kushiriki mashjindano ya CHAN msimu huu.

-->