Tunataka soka ya amani Simba na Yanga

Simba na Yanga zinakutana leo kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tumeshuhudia sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam mashabiki wa timu hizo wakitaniana na yote ni shamrashamra kuelekea mchezo huo unaosuburiwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka  kote nchini.

Mchezo huo umekuwa ukivuta hisia za mashabiki wengi na ndiyo maana mara nyingine hata husababisha matatizo kwa mashabiki wa klabu hizo kongwe pale yanapotokea matokeo  yoyote yawe ya kufurahisha au kuhuzunisha.

Wakati tukielekea katika mchezo huo tunaamini kwamba Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha ulinzi kuanzia ndani na nje ya uwanja, kwani inafahamika kuwa mchezo  baina ya timu hizo mbili huwa na mihemko ya mashabiki ambao huthubutu kufanya chochote.

Ni rai yetu kwa polisi kuwa makini  na  kutimiza majukumu yao vizuri badala ya muda mwingi kuwa makini kuangalia mchezo.

Lakini suala la ulinzi halipo kwa waliopewa dhamana hiyo pekee, hili linaanzia kwa mashabiki wenyewe, kwa kila mmoja kuona kuwa furaha na amani ya mchezo ni suala la msingi.

Kwa upande wa wachezaji, tunaamini wataonyesha soka ya uhakika, isiyo na uhasama kwa kuwa Simba na Yanga ni timu za mfano.

Kwa kuwa soka ina kauli mbiu ya uungwana, hatutarajii kuona soka la vurugu uwanjani, kukamiana  na kuumizana kwani tunaamini mpira ni ufundi na si kukomoana.

Wachezaji watambue kuwa mpira siyo vita bali ni sehemu ya kuonyesha upendo na kuleta amani na ndiyo maana nchi nyingi zenye vita soka huwa linawafanya watu kusahau mapambano na kuwaweka watu pamoja.

Mchezo uvurugike, mwamuzi anaweza kuwa sehemu ya mchango. Mwamuzi atakayesimama kati, ni vema kuondoa mapenzi na ushabiki na kusimama katikati ya Sheria 17 za soka ili mshindi apatikane kihalali na kuepusha vurugu ambazo si za lazima kutokana na mihemko ya ushabiki.

Tumeshuhudia mechi nyingi ambazo waamuzi huwa ni chanzo cha fujo viwanjani na kusababisha mechi kumalizika kwa  vurugu kuanzia kwa mashabiki ikiwemo kung’oa viti na kuharibu miundombinu ya viwanja, wachezaji kupigana na hata waamuzi pia kupigwa na yote inatokana na uchezeshaji mbaya wa mwamuzi.

Tunajua kuwa lengo la mchezo ni kumpata mshindi kwa njia sahihi, lakini pia kwa mashabiki hawana  sababu ya kufanya uharibifu.

Wakati mwingine mashabiki huja uwanjani wakiwa na matokeo yao mifukoni, jambo ambalo si zuri kwani ndiyo huwa chanzo cha vurugu baada ya mchezo kumalizika kwa upande wanaoshabikia kushindwa.

Mashabiki wanapaswa kuwa watulivu na kukubaliana na matokeo yoyote yatakayotokea kwani mpira ndiyo ulivyo na una matokeo matatu, kufunga, kufungwa na kutoa sare.

Mwisho ni  wito kwa viongozi wa klabu hizi mbili, ambao baada ya mchezo huwashutumu wachezaji, kuwafungia kwa kuamini kuwa ndiyo chanzo cha matokeo mabaya. Huu si uungwana kuwafanyia wachezaji.

Viongozi wanapaswa kuacha dhana hii kwa kuwa siku zote, soka ina matokeo matatu, kushinda, kufungwa na sare.