Ukweli wa Tattoo na Maadili Yetu Nchini

Muktasari:

Tukumbuke kuwa tattoo ni fani inayoingiza mamilioni ya dola katika dunia yetu na imekuwa ikitanuka kwa kasi hasa ukizingatia nyota wa filamu, michezo na sanaa nyinginezo huitangaza fani hii bure kwa michoro inayochorwa katika miili yao.

Wiki iliyopita nilianza mfululizo wa makala haya kuhusu michoro ya mwilini maarufu kwa jina la tattoo. Nilieleza mengi na leo nitaendelea na mada hii.

Tukumbuke kuwa tattoo ni fani inayoingiza mamilioni ya dola katika dunia yetu na imekuwa ikitanuka kwa kasi hasa ukizingatia nyota wa filamu, michezo na sanaa nyinginezo huitangaza fani hii bure kwa michoro inayochorwa katika miili yao.

Hapa Tanzania hatujabaki nyuma kwa kuwa vijana wetu wanajicharaza ‘manembo’ na mapicha katika miili yao.

Jambo hili linagusa maeneo ya maadili, afya na utawala wa sanaa. Swali la kujiuliza ni je, vyombo vya usimamizi wa sheria kama polisi wanaijua vizuri kisheria sanaa ya tattoo?

Ni sehemu ya fani ya sanaa za ufundi inayogeuza mwili wa binadamu kuwa malighafi au kitambaa (turubai) ya kuchorea.

Uchoraji wa tattoo ni utamaduni wa siku nyingi wa Mwafrika na Mtanzania. Makabila mengi kama Wamakomde, Wasukuma, Wamang’ati, Wasonjo, Wambulu, Wangindo, Wandengereko, Wabarbeig na wengine wengi wanatumia tattoo katika tamaduni zao.

Hata katika makabila yasiyo na tattoo za jumla kwa watu wake, wanazo kwa makundi maalumu kama machifu, waganga, majemedari, wanikulu na kadhalika. Tattoo za kisasa ziliongezewa umaarufu na mabaharia enzi za miaka ya 1980 na mwendelezo wake ndio huu wa leo hii.

Upo mpambano kwa maana ya maadili katika nyanja nyingi za sanaa kama muziki, uchoraji, uchongaji na kadhalika katika jamii yetu. Baadhi ya watu (hasa wazee) hawapendi ujumbe unaowekwa na vijana katika miili yao na mara nyingine ujumbe huu hutukuza (glorify) tamaduni za nje au za kisasa.

Vijana kwa upande wao wanaiendeleza sanaa hii ya mababu zao kujichora au kujiandika nembo na michoro mipya waliyotunga au waliyoiga mara nyingine bila hata kujua maana yake. Mjadala huu ni mpana na hautaisha kwenye makala hii. Napiga ‘tatoo’ ya kudumu katika mawazo yangu inikumbushe niutendee haki mjadala huu.

Kadri siku zinavyosogea umuhimu wa kuwa na utaratibu wa uchoraji tattoo ndivyo unavyozidi kuongezeka. Tayari hapa nchini hasa mijini zipo saluni za uchoraji maarufu kwa lugha ya kigeni kama tattoo parlours.

Ipo haja sasa kufanya usajili wa saluni za uchoraji katika Baraza la Sanaa la Taifa (Basata). Baraza linaweza kufanya uhakiki na usajili wa uwezo wa wachora tattoo hasa zile za kudumu.

Vilevile kupitia kitengo cha Osha (Occupational Safety and Health) ambacho kiko Wizara ya Kazi na kitengo cha udhibiti wa magonjwa katika Wizara ya Afya tunaweza kupata miongozo juu ya usalama wa kikazi na kiafya maalumu kwa eneo hili, ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za wateja ili linapotokea tatizo, ufuatiliaji unakuwa rahisi. Sera ya Serikali ya usalama kazini (National Occupational Health and Safety Policy) ya mwaka 2009 iko wazi kuhusu usalama katika maeneo ya kazi.

Wachora tattoo ni vyema wasaini mkataba na wateja wao kwani upo uwezekano mkubwa sanaa iliyochorwa mgongoni mwa mtu mmoja ikawa mali ya mchoraji na si mchorwaji.

Sasa hapa sheria ya hakimiliki na hakishirikishi inahusika, hivyo ni vyema wachoraji na wachorwaji wakaijua sheria hii.

Uchoraji tattoo una mazingira hatarishi kiafya kama utokaji damu na majimaji ya mwili, hivyo lazima ziwepo kanuni na miongozo ya namna gani kazi hii ifanyike na katika mazingira hayo lazima pawepo na huduma ya kwanza.

Magonjwa kama wa hepatitus ‘B’ na C, na Ukimwi yanaweza kuambukizwa wakati wa kuchora tattoo. Vyombo vinavyotumika sharti vipitishwe katika dawa za kuua wadudu ama viwe vya matumizi ya mara moja (disposable) na takataka kama za sindano ziwe zina udhibiti wa utupaji wake kwani zikitupwa hovyo zinaweza kuishia mahali ambapo watoto au wasiojua vitokako wakadhurika.

Ni vyema wachoraji wakawaelimisha wateja wao kuhusu athari zinazoweza kujitokeza katika uchoraji, la sivyo malalamiko na kesi nyingi zinaweza kuibuka. Vilevile msisitizo uwekwe katika kukataza uchorwaji tattoo kwa watu wenye ugonjwa wa ngozi mpaka pawepo na ruksa ya daktari. Hii itaepusha magonjwa ambukizi kutapakaa. Katika muktadha huu pia kuna haja ya wachorwa tattoo kutochora maeneo ya makovu au majeraha kama ya operesheni na kadhalika.

Mojawapo wa matatizo makubwa katika mfumo wa nchi yetu ni uwepo wa vyombo huru vya walaji katika maeneo mengi. Walaji hao (wachorwaji) wakipewa nafasi wanaweza kuchangia mjadala kwa kuujenga.

Muafaka wa jambo hili la tattoo endelevu ni mazungumzo. Mazungumzo kati ya Serikali na wadau, vijana kwa wazee, wanamtandao na wanamitindo, wanasheria na wabunge, wanautamaduni kwa wanasayansi.

Mwandishi ni msanii wa siku nyingi na Mkurugenzi wa Mipango wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini.