Usalama wa nchi ni wa kila Mtanzania

Muktasari:

  • Jambo hilo liliibuka zaidi baada ya sakata la kutekwa kwa msanii wa muziki wa Bongo fleva, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ hivi karibuni na hivyo kuwafanya watu mbalimbali kuhoji alipo Saanane. Baadhi ya wabunge waliomba matukio ya utekaji wasanii na tishio la kutekwa wabunge yajadiliwe kwa kina bungeni.

Tangu ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa Chadema wataarifu kuhusu kupotea kwa kada wa chama hicho, Ben Saanane kulitokea maoni mbalimbali kutoka kwa watu wakitaka Serikali itoe kauli kuhusu hilo.

Awali, kukosekana kwa maelezo hayo kulifanya mjadala kuwa mkubwa katika mitandao ya kijamii na hata kufanya wanasiasa wa vyama vya upinzani kuibua suala hilo mara kwa mara bungeni na kwenye mikutano ya ndani.

Tatizo lilianzia kwa polisi kuonekana kuwa kimya kwani tangu Saanane alipotoweka Novemba 18, mwaka jana ndugu na viongozi wa Chadema walitoa taarifa polisi ili kusaidia kupatikana kwa kada huyo aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Waziri wa Mambo ya Ndani aliwahi kukaririwa akisema amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi awaagize polisi kumtafuta Saanane lakini hakukuwa na taarifa zaidi kutoka polisi, ambalo mara kwa mara walisema wanalifuatilia suala hilo.

Katikati ya Desemba polisi waliwataka ndugu na jamaa kwenda Mto Ruvu eneo la Bagamoyo kukagua miili ya watu waliokufa kwa kutumbukizwa majini ikiwa imefungwa kwenye viroba.

Mazingira haya hasa ya vyombo vya dola kuonekana kushughulikia taratibu suala la kumsaka mwanasiasa huyo na kujua usalama wake, yaliwafanya wabunge wa Chadema kuhoji bungeni ili Serikali itoe majibu ya kuridhisha.

Jambo hilo liliibuka zaidi baada ya sakata la kutekwa kwa msanii wa muziki wa Bongo fleva, Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ hivi karibuni na hivyo kuwafanya watu mbalimbali kuhoji alipo Saanane. Baadhi ya wabunge waliomba matukio ya utekaji wasanii na tishio la kutekwa wabunge yajadiliwe kwa kina bungeni.

Hii ndiyo sababu mbunge mmoja aliamua kuiomba Serikali ikaombe msaada kutoka kwa makachero wa Scotland Yard ya Uingereza ambao mwaka 1990 waliisaidia Kenya kujua alivyotoweka hadi kufa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Robert Ouko.

Katika majibu yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema vyombo vya dola nchini vina uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina, bila msaada wa nje, hadi kujua hatima ya kada huyo.

Waziri Mkuu amewataka wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikitumia kila aina ya nyenzo, rasilimali na uwezo wote kufanya uchunguzi na kutoa majibu.

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Msaju ameeleza kushangazwa na vyombo vya usalama kutochukua hatua sahihi kujua ukweli wa kupotea kwa kada huyo.

Mwanasheria huyo alisema hafahamu sababu za suala hilo kujitokeza mara kwa mara ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Tumefurahishwa na mwelekeo huu ambao tunaamini utaiweka Serikali huru.

Tunaamini majibu hayo siyo tu yatakidhi vigezo bali kukubalika na kufanyiwa kazi na vyombo vya dola ili suala hilo lipate majibu ambayo yataridhisha pande zote.

Pia, tunaungana na Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu kuwataka wananchi wawe watulivu. Lakini kutokana na unyeti wa suala hii tunaisihi Serikali isichukue muda mrefu na ijitahidi kuwaaminisha na kuwahakikishia raia wake kuhusu jukumu ililonalo la kulinda haki ya kuishi na kuwaletea maendeleo na siyo vinginevyo.

Tunawasihi wananchi nao kuwa bega kwa bega kuisaidia Serikali katika masuala mbalimbali na hasa yanayohusu usalama wa nchi.