Zanzibar isikubali maadili yake kuchezewa

Muktasari:

Kwa kuheshimu hekima ya msemo huu na uzoefu uliopatikana zamani huenda ndiyo sababu watu wa visiwani Zanzibar wakawa na ukarimu kwa wageni kutoka kila pembe ya dunia bila ya kujali imani zao za dini, mila au utamaduni.

Waswahili wanao msemo maarufu usemao “Mgeni njoo mwenyeji apone”. Kwa lahaja asilia ya Wazanzibari maneno sahihi ya msemo huu ni mgeni aje mwenyeji apone.

Kwa kuheshimu hekima ya msemo huu na uzoefu uliopatikana zamani huenda ndiyo sababu watu wa visiwani Zanzibar wakawa na ukarimu kwa wageni kutoka kila pembe ya dunia bila ya kujali imani zao za dini, mila au utamaduni.

Hali hii ilisababisha Zanzibar kuwa kituo cha utalii maarufu zamani na kupokea mamia ya wageni kwa meli kubwa kama Europa na New Castle ambazo zilikuwa zikileta watalii mara tatu hadi nne kwa mwaka.

Karibu watalii wote wa zamani zile, wakiwa Wazugu na wageni kutoka nchi jirani waliheshimu mila, utamaduni na desturi za watu wa visiwani.

Kwa mfano, wanawake waliofika na nguo fupi walijifunika kanga na hata kujitanda nyingine kichwani ili waende sambamba na mwenendo wa maisha ya Wazanzibari.

Hata hivyo, hali imebadilika siku hizi na kila unapokwenda unasikia watu wanalamika kwamba utalii unachangia kuporomoka kwa maadili visiwani.

Baadhi ya wageni siku hizi wamekuwa wakishiriki kuuza miili yao kama vile ni bidhaa. Mara nyingi jambo hili linapolalamikiwa utasikia viongozi wa Serikali wakisema sheria namba moja ya mwaka 1973 inatoa fursa kwa

wananchi kusimamia utekelezaji wake kwa kuwafikisha vituo vya Polisi watu wanaovaa nguo zinazokwenda kinyume na sheria hiyo.

Sheria hiyo pia inawaruhusu wananchi kuwakamata wanaume wanaovaa mapambo ya kike, ikiwamo hereni, kidani na kusuka nywele na kuwafikisha vituo vya Polisi.

Hata hivyo, kuwa na sheria ni jambo moja na sharia hiyo kutekelezeka au kuwekewa mazingira ya kuitekeleza ni jambo jingine.

Uzoefu umeonyesha Serikali imeshindwa kusimamia sheria hii na baadhi ya watu siku hizi wanaonekana kutojali siyo kwenda nusu uchi tu, bali uchi zaidi ya robo tatu.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) sasa inaonekana kuchoshwa na kuporomoka kwa misingi ya dini ya Kiislamu, mila, maadili na desturi za watu wake za mavazi.

Hii inatokana na baadhi ya watu siku hizi kuonekana wanavaa nguo ambazo hazikubaliani na utamaduni wa watu wa Visiwani, jambo ambalo limekuwa likiwakasirisha watu wengi kwa muda mrefu sasa.

Baadhi ya watu hawa wamekuwa wakishiriki kuuza miili yao kama vile ni bidhaa. Taarifa ya Serikali ya hivi karibuni iliotolewa ndani ya Baraza la Wawakilishi imewataka wananchi kuwafikisha katika vituo vya Polisi watu wanaovaa mavazi ya nguo za nusu uchi na zinazobana.

Akijibu swali katika kikao cha Baraza, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema kuwa Sheria Namba Moja ya mwaka 1973 inatoa fursa kwa wananchi kusimamia utekelezaji wake kwa kuwafikisha vituo vya Polisi watu wanaovaa nguo zinazokwenda kinyume na sheria hiyo.

Waziri pia, alieleza kuwa sheria hiyo inawaruhusu wananchi kuwakamata wanaume wanaovaa mapambo ya kike, ikiwamo herini, kidani na kusuka nywele na kuwafikisha vituo vya Polisi.

Katika miaka ya nyuma, pale sheria hii iliposimamiwa vilivyo kila mtu Zanzibar, mwenyeji na mgeni, aliiheshimu na walioivunja walikiona cha mtema kuni.

Watalii waliofika Zanzibar wakiwa nusu uchi walilazimishwa kununua kanga au kitenge na kujifunga juu na chini na kuelezwa kuwa wapo huru kuonyesha sehemu zao za siri huko kwao walikotoka na siyo Visiwani.

Watalii waliokataa kutii amri hiyo walitakiwa kumalizia safari zao uwanja wa ndege au bandarini na kulazimishwa kurudi walikotoka ambako wapo huru kutembea uchi.

 

Hali ilivyo sasa

Siku hizi mambo ni tofauti. Ukitembelea Kijiji cha Nungwi, Kaskazini Unguja watu wanalalamika na ukienda Kambani, Kusini Unguja, kilio ni hicho hicho.

Kwa kweli sheria ya mavazi ipo Zanzibar na inafumbiwa macho na hicho huenda kikawa ndicho kinachotoa mchango mkubwa wa kuporomoka maadili Visiwani.

Kama Serikali inakusudia kuona sheria hii inafanya kazi basi ingetakiwa ionekane inaisimamia kwa vitendo na siyo kila siku kutoa onyo. Zanzibar inazo sheria nyingi zinazolinda utamaduni na heshima ya watu wake, lakini hazisimamiwi na watu wamekuwa huru kuzivunja, kama vile hazipo.

Watu wengi wanaokiuka sharia hiyo ni watalii na hufanya hivyo hata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hawaguswi. Wanawake huweka mambo hadharani hata kwenye masoko.

Ukiuliza kwa nini hali hii inafumbiwa macho unaambiwa ni suala la mgeni njoo mwenyeji apone, yaani kuja kwao kunasaidia kuiingizia Zanzibar fedha za kigeni.

Hii ni sawa na kusema fedha za kigeni zina umuhimu mkubwa kuliko kulinda utamaduni wa Zanzibar ambao umejengwa chini ya misingi ya dini ya Kiislamu kwa vile zaidi ya asilimia 95 ya watu wake ni Waislamu.

Wanaume kuvaa mavazi ya wanawake Sheria ya mavazi na kutoruhusu wanaume kuvaa kama wanawake au wanawake kuvaa kama wanaume zipo kwa miaka mingi na zinakubaliwa na watu wa

Unguja na Pemba ambao husema asiyetaka kuziheshimu arudi huko alikotoka.

Wapo watakaosema sheria hii ni kandamizi, lakini hawana ubavu wa kulazimisha wanawake wa Kiislamu wasivae hijabu kunakofanywa katika nchi za Ulaya siyo kuwaingilia Uislamu katika sheria zao za maisha na utamaduni wao.

SMZ inafaa kupongezwa kwa kutoa onyo la mara kwa mara kwa wageni juu ya hali hii, lakini lilio muhimu ni kuhakikisha sheria inafanya kazi na siyo kwa maneno matupu.

Hapo zamani sheria ilitoa mamlaka kwa wananchi kuwakamata watu wanaokwenda nusu uchi na wanaume wanojigeuza wanawake.

Vizuri kutilia maanani kuwa zama zimebadilika na sasa upo uwezekano kwa watu wachache kuitumia fursa hii kuleta maovu na hata kufanya utapeli.

Ni hatari katika dunia ya leo kumpa kila mtu nguvu za kisheria za kumkamata mtu na kumfungulia mashtaka.

Kazi hii ni ya Jeshi la Polisi ambalo ndilo kisheria lililopewa dhamana ya usalama wa raia na mali zao. Kutafuta wakala kwa kazi hii kunaweza kuleta vurugu na hata baadhi ya watu kuonewa.

Tayari hili linalalamikiwa kwa baadhi ya vikosi vya ulinzi kuchukua mamlaka haya hata kwa mambo ambayo hawana madaraka ya kisheria kuyafanya.

Vilevile, siyo ajabu wakatokea wahuni kwa lengo la kutaka kutapeli wakamkamata mtu na kumvisha nguo zinazoonyesha anakwenda nusu uchi au wakampaka mwanamume rangi ya mdomo wapate kisingizio cha kumkamata na hatimaye kumtoza fedha ili asibanwe na rungu la sheria.

Jingine ni kuhakikisha watalii wanaotembea nusu uchi hasa mbele ya misikiti na kwenye masoko wanalazimishwa kuheshimu sheria hii ili isonekane haiwagusi watalii.

Kwa hakika taswira ya Zanzibar kitabia na mavazi imebadilika na kwa waliotembelea visiwani miaka iliyopita watashangaa wakifika tena na kuiona hali ilivyo siku hizi.

Watu wa Zanzibar wanao wajibu wa kulinda utamaduni wao na kufumbia macho na masikio visingizio vya kuwapo uhuru usio na mipaka kwa wageni kufanya watakavyo ii hatimaye mwenyeji apone hautaisaidia Zanzibar ya leo wala ya kesho.

Wazanzibari wanao msemo unaonena: Zanzibar ni njema atakaye aje. Lakini msemo huu ulikusudia wanaokaribishwa ni wale wenye mambo ya kheri na siyo balaa na laana. Serikali ya Zanzibar ilipongezwa na watu wake ilipokataa miaka michache iliyopita kufanyika Visiwani mkutano wa kimataifa wa mashoga.

Kinachotakiwa sasa ni kuendelea kukaza kamba ili maadili ya watu wa Visiwani yasiendelee kupotoka.

Watatokea watu watakaolalama kuwa Zanzibar ina sheria kali, lakini hatimaye watasema mchana na usiku watalala.

Ni bora kuwaudhi wachache na kuwafurahisha wengi na hasa wakiwa ndiyo wananchi na wazalendo wa Visiwani.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]