MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Maoni ya Mhariri Mgogoro wa Serikali, madaktari sasa unahitaji wapatanishi
BOOKMARK THIS PAGE
Mgogoro wa Serikali, madaktari sasa unahitaji wapatanishi  Send to a friend
Monday, 30 January 2012 20:25

YEYOTE aliyemsikiliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akitoa majumuisho ya mgomo wa madaktari katika Ukumbi wa Karimjee juzi, bila shaka aliweza kung’amua kwamba Serikali awali ilifanya makosa kwa kushindwa kutambua ukubwa wa  mgomo huo na athari zake kwa jamii. Tunasema hivyo kwa sababu uongozi wa wizara husika ulionekana kutosikia sauti zilizokuwa zinapazwa na madaktari hao kabla mgomo wao haujashika kasi.
   
Itakumbukwa kwamba wakati mgomo huo ukiwa katika hatua za awali, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya aliombwa kukutana na madaktari hao lakini akawapiga chenga  na baadaye akaibuka ghafla na kusema madai ya madaktari hao hayakuwa na msingi wowote. Mgomo uliposhika kasi ndipo Waziri mwenye dhamana, Dk Hadji Mponda alipoingia ulingoni kwa kukutana na waandishi wa habari na kusoma taarifa kuhusu namna Serikali  ilivyokuwa inashughulikia madai yao.
   
Hata hivyo, badala ya kuleta ahueni, taarifa hiyo iliwasha moto na kuibua hasira za madaktari hao ambao waliituhumu Serikali kwa kuwadanganya, huku mgomo huo ukisambaa katika hospitali kubwa nchi nzima na kuwaacha wagonjwa wakilia na kusaga meno. Madaktari sasa walionyesha kuishiwa uvumilivu na ndipo walipotaka kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Kiongozi huyo alikubali kukutana nao bila kusita na bila masharti yoyote.
   
Lakini jambo la kushangaza madaktari hao walikataa kukutana naye, huku wakimpa masharti mapya ya kukutana nao. Kwa mshangao wa wengi, Waziri Mkuu aliyakubali masharti yao yote  lakini ghafla wakabadilisha msimamo na kuitaka Serikali ikubali kwanza kutekeleza madai yao yote kuanzia mwezi huu.
   
Ndiyo maana tumesema kwamba kila aliyemuona Waziri Mkuu akifanya majumuisho ya mgomo huo juzi atakuwa ameng’amua kwamba Serikali awali ilifanya makosa ya kuudharau mgomo huo kwa kuwatumia waziri na naibu wake ambao hakika hawakuwa na mbinu, uwezo wala karama ya kuwashawishi madaktari kusitisha mgomo na kurudi kazini, huku wawakilishi kutoka pande hizo mbili wakiwa wanaendelea na mazungumzo.
   
Katika majumuisho yake, Waziri Mkuu aliwafanya wananchi waliomsikiliza au kumwona katika televisheni akielezea jinsi alivyojitahidi kuwashawishi madaktari hao wasitishe mgomo wao, waamini kwamba katika wakati mfupi alioingilia mgomo huo alijitahidi sana kuonyesha jinsi Serikali ilivyokuwa na dhamira nzuri ya kuzungumza na madaktari hao kwa lengo la kupata suluhisho la matatizo yao. Kinyume na viongozi wengi serikalini, Waziri Mkuu huyo hakutumia ubabe, bali alionyesha busara, ushawishi, unyenyekevu na umakini mkubwa katika kujaribu kumaliza mgomo huo.  
   
Kuvunjika kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili kunatupa fundisho moja muhimu. Kwamba upatanishi wa migogoro (conflict resolution) katika karne tuliyomo hivi sasa haufanywi tena kwa kutumia mitulinga kama inavyofanyika sasa katika mgogoro huu wa Serikali na madaktari. Dunia ya leo inachukulia upatanishi wa migogoro kama taaluma inayohitaji wapatanishi wenye weledi wa hali ya juu.
   
Kama tulivyosema kupitia safu hii wakati mgogoro huu ulipoanza, kuna umuhimu wa kupata wapatanishi ambao wataaminiwa na pande zote mbili na ambao hawana maslahi yoyote katika mgogoro huo. Tuliishauri Serikali kwamba, kwa kuwa yenyewe ndiyo inatuhumiwa, haiwezi wakati huohuo kuwa mwamuzi wa suala hilo.
   
Ndiyo maana tunadhani kwamba watu wanaokubalika na kuheshimiwa katika jamii yetu, wakiwamo Jaji Joseph Warioba, Jaji Mark Bomani, Dk Salim Salim na Profesa Geoffrey Mmari na wengine wengi wanaweza kabisa kuwa wapatanishi katika mgogoro huo. Waziri Mkuu Pinda anayo haiba ya kuuongoza ujumbe wa Serikali kwenye mazungumzo hayo.
   
Wakati tukizihimiza pande zote mbili kurudi kwenye meza ya mazungumzo, tungependa madaktari waelewe kwamba katika hali kama hiyo, ni ndoto za mchana kufikiri kwamba watapata kila kitu walichokitaka, hasa kwa kutilia maanani kwamba baadhi ya madai yao hayatekelezeki. Tungependa kuwashauri pia kwamba katika mazungumzo yao na Serikali wanahitaji wawakilishi wanaoheshimu hoja za upande wa pili, siyo wababe na waropokaji mithili ya akina Stephen Ulimboka.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
+3 #3 2012-01-31 09:45
KWA HIYO MNATAKA KUTUAMINISHA KUWA LISEMWALO NA MKUBWA NI SAHIHI. JE NI KWELI KUWA HAWA MADAKTARI WALIKATAA KUONANA NA BWANA MKUBWA ? KWA NINI TAARIFA YA KUWAONA ITOLEWE JIONI AMBAPO INAKUWA VIGUMU KUITANA, KWANI MADAI YAO YAMEANZA LEO. HIZO JUUHUDI ZA KUTAKA SULUHISHO ZIMEANZA LEO, MASLAHI DUNI NA UKOSEFU WA VITENDEA KAZI UMEANZA LEO.JAMANI TATIZO NI KUBWA
Quote
 
 
-1 #2 2012-01-31 08:06
madaktari ni wataalam na wasomi wazuri,inakuwaj e msitofautishe waajiriwa serikalini na binafsi,mnaongo zwa kwenye mgomo na daktari asiye mwajiriwa wa serikali ambaye hana cha kupoteza mkifukuzwa.fikirieni mara mbili kabla hamjaendelea na mgomo.kweli mnastahili nyongeza inayoendana na hali halisi ya mapato ya serikali,hasa baada ya wabunge kuongezewa lakini,tumieni ushawishi unaokubalika kistaarabu.
Quote
 
 
+1 #1 2012-01-31 02:06
Ushauri wako ni nzuri na ninakubaliana na wewe. Utatuzi wa migogoro unahitaji busara na hekima ya hali ya juu.

Madai ya madaktari yanatekelezeka ingawa sio kwa haraka kama wanavyotaka kutokana na hali ya nchi. Ila ya awali kama kuwahamisha watekelezaji wa sekta ya afya, posho ya kulala kazini inawezekana kwa wakati huu maana mjengoni tumeshaongezewa . Ila katika makala yako umesahau kwamba mtoto wa mkulima alitoa majibu yake kupitia ofisi yake kabla, majibu ambayo pia yalikuwa na dharau fulani.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner