MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Maoni ya Mhariri TFF ifungue akaunti ya Twiga Stars
BOOKMARK THIS PAGE
TFF ifungue akaunti ya Twiga Stars  Send to a friend
Saturday, 28 January 2012 09:33

KESHO timu ya Taifa ya soka ya wanawake (Twiga Stars)  itavaana na Namibia kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kushiriki Fainali za nane za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.Mechi hii ya marudiano inachezwa huku Twiga ikiwa na faida ya hatua moja mbele kufuatia ushindi wa mabao 2-0 waliopata ugenini wiki mbili zilizopita Windhoek, Namibia.

Sare yoyote itashuhudia Twiga ikivuka hatua nyingine mbele na kusubiri mshindi wa mechi kati ya Misri na Ethiopia Mei mwaka huu.Kama itafanikiwa kushinda mechi dhidi ya Ethiopia au Misri, basi itakata tiketi ya kucheza fainali hizo kwa mara ya pili nchini Guinea ya Ikweta baadaye Novemba.

Ni jukumu letu watanzania wote wapenda michezo kujitokeza kwa wingi kuishangilia na kuitia hamasa za ushindi timu yetu itakaposhuka dimbani kesho.

Lakini wakati tukiomba mashabiki kujitokeza kuwaunga mkono dada zetu, mabinti au wadogo zetu tunashangazwa na kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania TF kushindwa kutenganeza mkakati kabambe wa kuhakikisha wanaitumia mechi hii kuwashawishi watu wengi kujitokeza kushangilia.
Tunaamini kuwa sehemu kubwa ya mapato ya kuendesha soka letu, iwe kwa vilabu au timu za taifa yanatokana na viingilio vya uwanjani.

Maana yetu ni kwamba, mapato yatakayopatikana katika mechi hiyo yasingestahili kugawanywa kwenda DRFA, BMT, TFF au Taasisi nyingine bali yote yangekuwa kwa ajili ya Twiga Stars.

Mapato hayo yalitakiwa kufunguliwa akaunti yake na kuwa chanzo cha mapato ya Twiga Stars, kwa sababu timu hiyo ipo katika mazingira magumu kifedha na tunafahamu ilienda kushindana Namibia katika hali ya kuombaomba.

Kwa ufupi maandalizi ya Twiga hayakuridhisha na hii ni kutokana na kukosa baadhi ya huduma muhimu za kuifanya timu kushiriki kiushindani kulinganisha na ukubwa wa mashindano yenyewe.

Tunaamini kama TFF wangefungua akaunti nyingine kwa ajili ya Twiga Stars na siyo akaunti ya TFF na kuweka fedha za zitakazopatikana katika mechi hiyo, basi hakika wadau wengi wangejitokeza kuichangia.

Pia tunaamini fedha zinazotolewa na watu mbalimbali hivi sasa wakiwamo wabunge zilitakiwa kuwekwa katika akaunti hiyo maalumu ya Twiga Stars ambayo ingekuwa endelevu kwa ajili ya kuisaidia timu.

Ni hakika yetu kuwa, TFF wamelisikia hili na watakuwa tayari kufungua akaunti hiyo ili wadau na wapenda michezo wajikitokeza kuichangia Twiga, ambayo kadri siku zinavyokwenda imezidi kuvuta mashabiki.

Hakuna shaka kwamba, kuna watanzania wengi wana uwezo wa hali na mali kuichangia timu hii na kupata huduma nzuri.Ukweli uko wazi kwamba, timu yenye wachezaji wenye vipaji, iliyoandaliwa vizuri na kupata huduma nzuri ndiyo yenye nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano.Ni vyema pia serikali ikatupia jicho na kuisaidia Twiga katika safari yake ya kusaka tiketi hiyo.

Makampuni pia yana fursa ya kusaidia katika kuhakikisha timu inapata maandalizi yote muhimu ili kila inapocheza basi ifanye hivyo kwa ushindani na siyo ushiriki.Tunashangazwa na hali hii ya serikali, makampuni na watu wenye uwezo kushindwa kuisaidia Twiga Stars, wakati ni timu iliyoonyesha inaweza kufika mbali.

Tunasema hivyo kwa sababu timu ya Twiga Stars ni timu inayoogopwa na timu nyingi za Kusini mwa Afrika, hasa ukizingatia kuwa Julai mwaka jana ilialikwa kwenye mashindano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) nchini Zimbabwe na kushika nafasi ya tatu.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner